Jumatatu, Agosti 19, 2019
Jumatatu ya Juma la Ishirini la Mwaka
Mtakatifu Yohane Eudes, Padri – Kumbukumbu ya Hiari

Sikiliza kwa Kiingereza
“Ukitaka kuwa mkamilifu, nenda, uza ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.” Kijana huyo aliposikia maneno haya, aliondoka akiwa na huzuni, kwa maana alikuwa na mali nyingi. Mathayo 19:21-22
Ni heri kwamba Yesu hakukuambia wewe wala mimi maneno haya! Sivyo? Au je, alituambia? Je, maneno haya yanatuhusu sisi sote ikiwa tunataka kuwa wakamilifu? Huenda jibu likakushangaza.
Ni kweli kwamba Yesu huwaita baadhi ya watu wauze mali zao zote na kuwagawia wengine mapato yake. Wale wanaoitikia wito huu hugundua uhuru mkubwa wanapoacha kushikamana na mali zote za ulimwengu. Wito wao ni ishara kwetu sote ya ule wito wa ndani unaodai kujitoa kikamilifu ambao kila mmoja wetu amepewa. Lakini sisi wengine je? Ni upi huo wito wa ndani unaodai kujitoa kikamilifu ambao Bwana wetu ametupa? Ni wito wa umaskini wa rohoni. Tunaposema “umaskini wa rohoni,” tunamaanisha kwamba kila mmoja wetu ameitwa kuacha kushikamana na vitu vya ulimwengu huu kwa kiwango kilekile kama wale walioitwa kuishi katika umaskini wa mali. Tofauti pekee ni kwamba wito mmoja unahusu maisha ya ndani na ya nje, na ule mwingine unahusu maisha ya ndani tu. Lakini nao unapaswa kuhusisha kujitoa kikamilifu kwa kiwango kilekile.
Umaskini wa ndani ukoje? Ni mojawapo ya Heri. “Heri maskini wa roho,” kama asemavyo Mtakatifu Mathayo, na “Heri maskini,” kama asemavyo Mtakatifu Luka. Umaskini wa rohoni unamaanisha kwamba tunagundua baraka ya utajiri wa rohoni tunapoacha kushikamana na vishawishi vya mali vya nyakati hizi. Hapana, “vitu” vya kimwili si viovu. Ndiyo maana si vibaya kuwa na mali binafsi. Lakini ni jambo la kawaida sana kwetu pia kushikamana sana na vitu vya ulimwengu huu. Mara nyingi mno tunataka kuwa na vitu vingi zaidi na zaidi, na tunaingia katika mtego wa kufikiri kwamba kuwa na “vitu” vingi zaidi kutatufanya tuwe na furaha. Hilo si kweli, nasi tunalijua hilo ndani kabisa ya mioyo yetu, lakini bado tunaingia moja kwa moja katika mtego wa kutenda kana kwamba fedha na mali nyingi zaidi zitatutosheleza. Kama katekisimu moja ya zamani ya Kirumi inavyosema, “Mwenye fedha kamwe hana fedha za kumtosha.”
Tafakari leo juu ya wito ulio wazi ambao umeupokea wa kuishi katika ulimwengu huu bila kushikamana na vitu vya ulimwengu huu. Mali ni njia tu ya kufikia lengo la kuishi maisha matakatifu na kutimiza kusudi lako maishani. Hilo litamaanisha kuwa na kile unachohitaji, lakini pia litamaanisha kujitahidi kuepuka kuwa na mali kupita kiasi na, hasa, kuepuka kushikamana moyoni na mali za ulimwengu.
Bwana, kwa hiari yangu ninaviacha vyote nilivyo navyo na ninavyovimiliki. Ninakutolea vyote kama sadaka ya kiroho. Pokea vyote nilivyo navyo na unisaidie kuvitumia tu kwa namna unavyotaka Wewe. Katika hali hiyo ya kutoshikamana na mali, nijalie nigundue utajiri wa kweli ulioniwekea. Yesu, nakutumainia.
Tafakari juu ya Huruma ya Mungu
Mtakatifu wa Siku – Mtakatifu Yohane Eudes




