Kiswahili

Kulipanda Neno la Mungu…Bila Kujali Matokeo

Januari 29, 2020
Jumatano ya Wiki ya Tatu ya Kipindi cha Kawaida
Masomo ya Leo

Sikiliza kwa Kiingereza

“Sikilizeni! Mpanzi alitoka kwenda kupanda.”  Marko 4:3

Maneno haya yanaanza Mfano wa Mpanzi tunaoufahamu.  Tunajua maelezo ya mfano huu: mpanzi anapanda mbegu njiani, penye miamba, kati ya miiba na hatimaye kwenye udongo mzuri.  Simulizi hili linafunua kwamba tunapaswa kujitahidi kuwa kama huo “udongo mzuri,” kwa kulipokea Neno la Mungu nafsini mwetu na kuliacha litunzwe ili likue kwa wingi.

Lakini mfano huu unafunua jambo jingine ambalo linaweza kupitwa kwa urahisi.  Unafunua ukweli rahisi kwamba mpanzi, ili apande angalau baadhi ya mbegu kwenye udongo mzuri wenye rutuba, lazima achukue hatua.  Lazima atoke na kutawanya mbegu kwa wingi.  Anapofanya hivyo, hapaswi kuvunjika moyo ikiwa mbegu nyingi alizopanda hazifiki kwenye huo udongo mzuri.  Njiani, penye miamba na penye miiba ni mahali ambapo mbegu hupandwa lakini hatimaye hufa.  Ni sehemu moja tu kati ya zile nne zilizotajwa katika mfano huu inayowezesha mbegu kukua.

Yesu ndiye Mpanzi wa Kimungu na Neno Lake ndilo Mbegu. Kwa hiyo, tunapaswa kutambua kwamba sisi pia tumeitwa kutenda kwa niaba Yake kwa kupanda mbegu ya Neno Lake katika maisha yetu wenyewe.  Kama Yeye alivyo tayari kupanda akijua kwamba si kila mbegu itazaa matunda, vivyo hivyo sisi pia lazima tuwe tayari na wenye hiari ya kuukubali ukweli huo.

Ukweli ni kwamba, mara nyingi sana, kazi tunazomtolea Mungu kwa ajili ya kuujenga Ufalme Wake hatimaye huzaa matunda machache yanayoonekana au hazizai matunda yanayoonekana hata kidogo.  Mioyo huwa migumu, na mema tunayofanya, au Neno tunalowashirikisha wengine, hayakui.

Somo moja tunalopaswa kujifunza kutokana na mfano huu ni kwamba kueneza Injili kunahitaji juhudi na kujitoa kwa upande wetu.  Tunapaswa kuwa tayari kutaabika na kufanya kazi kwa ajili ya Injili, iwe watu wako tayari kuipokea au la.  Wala tusikubali kuvunjika moyo ikiwa matokeo si yale tuliyoyatarajia.

Tafakari leo juu ya utume uliopewa na Kristo wa kulieneza Neno Lake.  Sema “Ndiyo” kwa utume huo, kisha tafuta njia, kila siku, za kulipanda Neno Lake.  Tarajia kwamba, kwa masikitiko, juhudi zako nyingi zitazaa matunda machache yanayoonekana.  Hata hivyo, uwe na matumaini makubwa na imani thabiti kwamba baadhi ya mbegu hizo zitafika kwenye udongo ambao Bwana wetu anataka zifike.  Jitoe kwa kazi ya kupanda; Mungu atashughulikia yaliyobaki.

Bwana, ninajiweka tayari kwa ajili Yako ili kuitumikia Injili.  Ninaahidi kukutumikia kila siku, nami ninajitoa kuwa mpanzi wa Neno Lako la kimungu.  Nisaidie nisikazie mno matokeo ya juhudi zangu; badala yake, nisaidie kuyakabidhi matokeo hayo Kwako Wewe tu na kwa maongozi Yako ya kimungu.  Yesu, nakutumainia.

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Watakatifu/Sikukuu za Leo