Jumanne, Septemba 29, 2020
Sikukuu ya Watakatifu Mikaeli, Gabrieli na Rafaeli, Malaika Wakuu

Sikiliza kwa Kiingereza
“Amina, amina, nawaambia, mtaona mbingu imefunguka na malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Mtu.” Yohane 1:51
Ndiyo, malaika wapo kweli. Nao wana nguvu, utukufu, uzuri na fahari kwa kila namna. Leo tunawaheshimu watatu kati ya umati wa malaika wa Mbinguni: Mikaeli, Gabrieli na Rafaeli.
Malaika hawa ni “malaika wakuu.” Malaika wakuu wako katika daraja la pili la malaika, juu tu ya malaika walinzi. Kwa jumla, kuna madaraja tisa ya viumbe vya mbinguni ambavyo kwa kawaida tunaviita malaika, na kimapokeo madaraja hayo yote tisa yamegawanywa katika ngazi tatu. Mpangilio huo mzima wa madaraja kimapokeo uko hivi:
Ngazi ya Juu Zaidi: Maserafi, Makerubi na Viti vya Enzi.
Ngazi ya Kati: Utawala, Fadhila na Mamlaka.
Ngazi ya Chini: Enzi, Malaika Wakuu na Malaika (Malaika Walinzi).
Madaraja ya viumbe hawa wa mbinguni yamepangwa kulingana na kazi na makusudi yao. Viumbe wa daraja la juu zaidi, Maserafi, waliumbwa kwa kusudi moja tu: kukizunguka Kiti cha Enzi cha Mungu wakimwabudu na kumsujudia daima. Viumbe wa daraja la chini kabisa, Malaika Walinzi, waliumbwa kwa kusudi la kuwatunza wanadamu na kuwafikishia ujumbe wa Mungu. Malaika Wakuu, ambao tunawaheshimu leo, waliumbwa kwa kusudi la kutuletea ujumbe wenye umuhimu mkubwa na kutimiza kazi zenye umuhimu wa hali ya juu kabisa katika maisha yetu.
Mikaeli anajulikana sana kama malaika mkuu aliyepewa uwezo na Mungu wa kumfukuza Lusifa kutoka Mbinguni. Kimapokeo, Lusifa hudhaniwa kuwa wa ngazi ya juu zaidi ya viumbe vya mbinguni; kwa hiyo, kufukuzwa na malaika mkuu wa daraja la chini kulikuwa fedheha kubwa kwake.
Gabrieli anajulikana sana kama malaika mkuu aliyemletea Bikira Maria Mwenye Heri ujumbe wa Umwilisho.
Naye Rafaeli, ambaye jina lake linamaanisha “Mungu huponya,” anatajwa katika Kitabu cha Tobiti cha Agano la Kale, na inasemekana alitumwa kuponya macho ya Tobiti.
Ingawa hatujui mengi kuhusu malaika hawa wakuu, ni muhimu kuwaamini, kuwaheshimu na kusali kwao. Tunasali kwao kwa sababu tunaamini kwamba Mungu amewakabidhi utume wa kutusaidia kuleta uponyaji, kupambana na uovu na kulitangaza Neno la Mungu. Nguvu zao zinatoka kwa Mungu, lakini Mungu amechagua kuwatumia malaika wakuu, pamoja na viumbe wote wa mbinguni, kutimiza mpango na kusudi Lake.
Tafakari leo kuhusu ufahamu wako wa malaika. Je, unawaamini? Je, unawaheshimu? Je, unategemea maombezi na upatanishi wao wenye nguvu katika maisha yako? Mungu anataka kuwatumia, kwa hiyo unapaswa kutafuta kwa dhati msaada wao katika maisha yako.
Bwana, nakushukuru kwa zawadi ya Malaika Wakuu ambao tunawaheshimu leo. Nakushukuru kwa utendaji wao wenye nguvu katika maisha yetu. Utusaidie kuwategemea na kuwapenda kwa huduma yao. Malaika Wakuu, mtuombee, mtuponye, mtufundishe na mtulinde. Yesu, nakutumainia.
Siku ya Nane: Novena kwa Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu wa Lisieux – Ua Dogo
Tafakari juu ya Huruma ya Mungu
Sikukuu ya Leo– Watakatifu Mikaeli, Gabrieli na Rafaeli, Malaika Wakuu
Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu
Picha: Malaika Wakuu Watatu pamoja na Tobia, iliyochorwa na Francesco Botticini




