Oktoba 27, 2020
Jumanne ya Wiki ya Thelathini ya Mwaka
Masomo ya Leo

Sikiliza kwa Kiingereza
Akasema tena, “Nitaufananisha Ufalme wa Mungu na nini? Ni kama chachu ambayo mwanamke aliichukua akaichanganya na vipimo vitatu vya unga wa ngano mpaka donge lote la unga likachachuka.” Luka 13:20-21
Chachu ni kitu cha kuvutia sana. Ni ndogo sana, lakini ina athari kubwa sana kwa donge la unga. Chachu hufanya kazi polepole na kwa namna inayoonekana kuwa ya kimiujiza. Kidogo kidogo donge la unga hufumuka na kubadilika. Daima watoto huvutiwa kutazama jambo hili wakati wa kutengeneza mkate.
Hii ndiyo namna bora ya Injili kufanya kazi katika maisha yetu. Hivi sasa, Ufalme wa Mungu uko hai kwanza kabisa ndani ya mioyo yetu. Ni mara chache tu kuongoka kwa mioyo yetu kunapotokea kwa ufanisi ndani ya siku moja au kwa muda mfupi. Bila shaka, kila siku na kila dakika ni muhimu, na hakika kuna nyakati zenye nguvu za kuongoka ambazo sote tunaweza kuzitaja. Lakini kuongoka kwa moyo kunafanana zaidi na chachu inayolifanya donge la unga lifumuke. Kwa kawaida, kuongoka kwa moyo ni jambo linalotokea kidogo kidogo na hatua kwa hatua. Tunamruhusu Roho Mtakatifu ayaongoze maisha yetu kwa namna inayozidi kuwa ya kina, na tunapofanya hivyo, tunazidi kukua katika utakatifu kama vile donge la unga linavyofumuka polepole lakini kwa hakika.
Tafakari leo mfano huu wa chachu inayolifanya donge la unga lifumuke. Je, unaona huu kuwa mfano wa nafsi yako? Je, unamwona Roho Mtakatifu akifanya kazi ndani yako kidogo kidogo? Je, unajiona ukibadilika polepole lakini bila kukoma? Tunatumaini kwamba jibu ni “Ndiyo.” Ingawa kuongoka huenda kusitokee daima kwa mara moja, lazima kuwe endelevu ili kuiwezesha nafsi kusonga mbele kuelekea mahali ilipoandaliwa na Mungu.
Bwana, ninatamani kweli kuwa mtakatifu. Ninatamani kubadilishwa kidogo kidogo kila siku. Nisaidie nikuruhusu unibadilishe kila dakika ya maisha yangu ili niweze kuendelea kutembea katika njia uliyoniwekea. Yesu, nakutumainia.
Sala & Nyenzo kwa ajili ya Uchaguzi wa Marekani
Tafakari juu ya Huruma ya Mungu
Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu




