Aprili 30, 2021
Ijumaa ya Wiki ya Nne ya Pasaka
Masomo ya Leo
Mtakatifu Pio V, Papa—Kumbukumbu ya Hiari
Sikiliza kwa Kiingereza
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Mioyo yenu isifadhaike. Mnamwamini Mungu; niaminini pia Mimi.” Yohane 14:1
Katika Injili ya Yohane, Sura 14–17 zinatuletea yale yanayoitwa “Hotuba za Yesu za Karamu ya Mwisho,” au “Hotuba Zake za Mwisho.” Hizi ni hotuba kadhaa ambazo Bwana wetu aliwapa wanafunzi usiku aliokamatwa. Hotuba hizi zina maana ya kina na zimejaa mifano ya kiishara. Anazungumza juu ya Roho Mtakatifu, Msaidizi, mzabibu na matawi, chuki ya ulimwengu, na hotuba hizi zinahitimishwa kwa Sala ya Yesu kama Kuhani Mkuu. Hotuba hizi zinaanza na Injili ya leo, ambamo Yesu anazungumzia hofu itakayokuja, au mfadhaiko wa mioyo, ambao anajua wanafunzi Wake watapata.
Tuanze kwa kutafakari maneno haya ya kwanza aliyosema Yesu hapo juu: “Mioyo yenu isifadhaike.” Hii ni amri. Ni amri ya upole, lakini bado ni amri. Yesu alijua kwamba muda si mrefu wanafunzi Wake wangemwona akikamatwa, akisukiwa mashtaka ya uongo, akidhihakiwa, akipigwa na kuuawa. Alijua kwamba wangelemewa na yale ambayo wangepitia muda si mrefu, kwa hiyo alitumia nafasi hii kuikemea kwa upole na upendo hofu ambayo wangekabiliana nayo karibuni.
Hofu inaweza kutokana na vyanzo vingi tofauti. Hofu fulani hutusaidia, kama vile hofu tunayopata tunapokuwa katika hali ya hatari. Katika hali hiyo, hofu hiyo inaweza kutufanya tutambue hatari zaidi ili tuendelee kwa tahadhari. Lakini hofu ambayo Yesu alikuwa akiizungumzia hapa ilikuwa ya aina nyingine. Ilikuwa hofu ambayo ingeweza kusababisha maamuzi yasiyo na mantiki, kuchanganyikiwa, na hata kukata tamaa. Hii ndiyo aina ya hofu ambayo Bwana wetu alitaka kuikemea kwa upole.
Ni nini kinachokufanya uwe na hofu nyakati fulani? Watu wengi wanapambana na mahangaiko, wasiwasi na hofu kwa sababu nyingi tofauti. Ikiwa unapambana na hali hii, ni muhimu kuruhusu maneno ya Yesu yapenye akilini na moyoni mwako. Njia bora ya kuishinda hofu ni kuikemea katika chanzo chake. Msikie Yesu akikuambia, “Moyo wako usifadhaike.” Kisha sikiliza amri Yake ya pili: “Unamwamini Mungu; niamini pia Mimi.” Imani kwa Mungu ndiyo tiba ya hofu. Tunapokuwa na imani, tunaongozwa na sauti ya Mungu. Ukweli wa Mungu ndio unaotuongoza badala ya shida tunayokabiliana nayo. Hofu inaweza kutufanya tufikiri bila mantiki, na kufikiri bila mantiki kunaweza kutuzamisha zaidi na zaidi katika kuchanganyikiwa. Imani hupenya na kuyashinda mawazo yasiyo na mantiki tunayoshawishiwa kuwa nayo, na kweli ambazo imani inatuonyesha hutuletea uelewa ulio wazi na nguvu.
Tafakari leo juu ya chochote kinachokusababishia mahangaiko, wasiwasi na hofu nyingi zaidi maishani mwako. Mruhusu Yesu aseme nawe, akuite uwe na imani na akemee mahangaiko hayo kwa upole lakini kwa uthabiti. Unapokuwa na imani kwa Mungu, unaweza kustahimili mambo yote. Yesu aliustahimili Msalaba. Hatimaye wanafunzi waliistahimili misalaba yao. Mungu anataka kukuimarisha wewe pia. Mwache aseme nawe ili ushinde chochote kinachoufadhaisha zaidi moyo wako.
Mchungaji wangu mwenye upendo, Wewe unajua mambo yote. Unaujua moyo wangu na shida ninazokabiliana nazo maishani. Unipe ujasiri ninaouhitaji, Bwana mpendwa, ili nikabiliane na kila kishawishi cha kuogopa nikiwa na hakika na nikikutumainia Wewe. Ujalie akili yangu uelewa ulio wazi na moyo wangu uliofadhaika amani. Yesu, nakutumainia.
Tafakari juu ya Huruma ya Mungu
Mtakatifu wa Siku – Mtakatifu Pius V, Papa
Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu
Picha zilizoangaziwa hapo juu: Kristo Akiwaaga Mitume, kazi ya Duccio di Buoninsegna





