Kiswahili

Unachangamana na Nani?

15 Januari 2022
Jumamosi ya Juma la Kwanza la Kipindi cha Mwaka
Masomo ya Leo

Video

Sikiliza kwa Kiingereza

“Kwa nini anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?”  Yesu alisikia hayo akawaambia, “Wenye afya hawahitaji tabibu, bali wagonjwa ndio wanaomhitaji.  Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”  Marko 2:16-17

Yesu alifanya hivyo; je, wewe?  Je, uko tayari kuonekana pamoja na wale walio “wenye dhambi?”  Jambo la kuvutia katika kifungu hiki cha Maandiko Matakatifu ni kwamba KILA MTU ni mwenye dhambi.  Kwa hiyo, ukweli ni kwamba kila mtu ambaye Yesu alichangamana naye alikuwa mwenye dhambi.

Lakini kifungu hiki na ukosoaji huu dhidi ya Yesu havikuhusu sana Yeye kuchangamana na watu waliotenda dhambi; badala yake, vilihusu zaidi Yeye kuchangamana na wale waliodharauliwa na watu wa tabaka la juu katika jamii.  Yesu alitumia muda kwa hiari pamoja na watu “wasiotakiwa.”  Hakuogopa kuonekana pamoja na wale waliodharauliwa na wengine. Waandishi na Mafarisayo waligundua upesi sana kwamba Yesu na wanafunzi Wake waliwakaribisha watu hao.  Walikula na kunywa pamoja na watoza ushuru, waliotenda dhambi za uasherati, wezi na wengine wa aina hiyo.  Zaidi ya hayo, yaonekana waliwakaribisha watu hao bila kuwahukumu.

Basi, turudi kwenye swali la mwanzo…Je, uko tayari kuonekana na kuchangamana na wale wasiopendwa na wengi, wenye maisha yaliyovurugika, wanaoumia, waliochanganyikiwa na wengine wa aina hiyo?  Je, uko tayari kukubali sifa yako iharibike kwa sababu unawapenda na kuwajali wenye uhitaji?  Je, uko tayari hata kufikia hatua ya kufanya urafiki na mtu ambaye ataharibu sifa yako katika jamii?

Tafakari leo kuhusu mtu katika maisha yako ambaye huenda unahisi kutaka kumwepuka.  Kwa nini unahisi hivyo?  Ni nani ambaye huenda hutaki kuonekana naye au ambaye huna utayari wa kuchangamana naye?  Huenda mtu huyu, kuliko mwingine yeyote, ndiye ambaye Yesu anataka utumie muda pamoja naye.

Bwana wangu mwenye upendo, Wewe unawapenda watu wote kwa upendo wa kina na mkamilifu.  Ulikuja hasa kwa ajili ya wale ambao maisha yao yalikuwa yamevunjika na yenye dhambi.  Nisaidie daima kuwatafuta wale wenye uhitaji na kuwapenda watu wote kwa upendo usioyumba wala kuwahukumu.  Yesu, nakutumainia.

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Tafakari za Maandiko Matakatifu kwa Kipindi cha Mwaka

Watakatifu/Sikukuu za Leo

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu

Picha kuu hapo juu: Karamu Nyumbani kwa Simoni na Paolo Veronese, kupitia Wikimedia Commons


Kitabu Kilichoangaziwa:

Tafakari za Kila Siku kwa Kipindi cha Kawaida:
Majuma 1-17

Tafakari za Kila Siku kwa Kipindi cha Mwaka: Wiki 1–17 kutoka katika Mfululizo wa Tafakari za Kila Siku za Kikatoliki ni kitabu cha ibada ya kila siku kinachotoa tafakari kuhusu Injili ya siku kwa namna ya vitendo, aminifu kwa imani na inayoendana na maisha ya kawaida.  Matoleo ya kitabu cha kielektroniki na kitabu chenye jalada laini yamepangwa kwa namna inayowezesha kitabu hiki kutumiwa mwaka baada ya mwaka. Tafakari hazijawekewa tarehe mahususi za Kipindi cha Mwaka cha 2022, bali zinajumuisha kila chaguo la masomo kwa mwaka huu wa kiliturujia na miaka ijayo, na hivyo kukifanya kuwa kitabu cha ibada kinachoweza kutumiwa mwaka baada ya mwaka.