Kiswahili

Kuwa Huru na Hofu

17 Februari 2022
Alhamisi ya Juma la Sita la Kipindi cha Mwaka
Masomo ya Leo

Watakatifu Saba Waanzilishi wa Shirika la Watumishi wa Maria—Kumbukumbu Isiyo ya Lazima

Video

Sikiliza kwa Kiingereza

Yesu alianza kuwafundisha Mitume kwamba Mwana wa Mtu lazima ateseke sana na kukataliwa na wazee, wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa, na kufufuka baada ya siku tatu.  Alisema hayo waziwazi.  Ndipo Petro akamchukua kando na kuanza kumkemea.  Marko 8:31-32

Kwa nini Petro alimchukua Yesu kando na kumkemea?  Je, alimkemea kwa sababu alikuwa amemkasirikia Yesu?  Hapana, inaelekea zaidi kwamba alimkemea kwa sababu ya hofu aliyokuwa nayo moyoni mwake.

Kifungu hiki kinasema kwamba Yesu “alianza kuwafundisha” Mitume kwamba hivi karibuni angepata mateso makali, angekataliwa na kuuawa.  Ingekuwa vigumu kwa Mitume kukubali na kuelewa jambo hili.  Mwanzoni, huenda wangepatwa na hisia na mawazo yote ambayo sisi sote huwa nayo tunapojaribu kuelewa na kukubali habari fulani ngumu.  Tunaweza kuanza kwa kukataa kuamini, kisha kukasirika, kutafuta njia ya kuepuka hali hiyo, kupatwa na hofu kuu, kuchanganyikiwa, na kadhalika.  Kupitia hatua za majonzi na kukubali hali ni jambo la kawaida, na inaonekana kwamba hicho ndicho kilichokuwa kikimpata Petro.

Kutokana na mapambano yake ya ndani ya kujaribu kukubali yale ambayo Yesu alikuwa anaanza kuwafunulia, Petro alijaribu kuweka kizuizi.  Katika simulizi la Mathayo kuhusu tukio hili, tunasikia maneno halisi ya Petro: “Mungu apishilie mbali, Bwana! Jambo kama hilo halitakupata kamwe” (Mt. 16:22).

Hakika maneno ya Petro yalionyesha kwamba alimjali Yesu, lakini ni muhimu kutambua kwamba kumjali kwake Yesu hakumaanishi kwamba maneno yake yalikuwa ya msaada.

Simulizi linapoendelea, Yesu anamkemea Petro kwa ukali, lakini anafanya hivyo kwa kumpenda Petro ili kumsaidia kuondokana na hofu na kuchanganyikiwa kwake.  Inaeleweka kwamba Petro anaogopa utabiri kuhusu Msalaba.  Inaeleweka pia yeyote kati yetu anapohisi hofu anapokabiliwa na msalaba mzito au shida kubwa.  Jambo kuu hapa ni kujua kwamba Yesu hataki tuendelee kuishi katika hofu.  Hataki tuikimbie misalaba tunayopewa kwa sababu ya udhaifu wetu wa kibinadamu.  Badala yake, anataka tumgeukie na tujaribu kufikiri kama Yeye anavyofikiri, kutenda kama Yeye anavyotenda, na kukabiliana na shida zetu kama Yeye alivyofanya kwa kuukumbatia Msalaba Wake.

Tafakari leo jinsi unavyoitikia mambo magumu ambayo Mungu anakuita uyafanye.  Ndiyo, unaweza kuwa na hakika kwamba kila siku anakuita kutenda mambo yanayohitaji kujitoa sana na upendo mkuu.  Hilo linaweza kuleta maumivu.  Lakini hupaswi kamwe kuruhusu maumivu ya msalaba wowote yakuzuie kuubeba.  Sali ili uwe na ujasiri wa kukabiliana na misalaba yako na, ikihitajika, uwe tayari kukubali karipio la upendo la Yesu unapotambua kwamba unahitaji kukemewa ili uanze kufuata njia ya kuwa huru na hofu.

Bwana mwenye nguvu, ninajua kwamba uliikabili sadaka takatifu ya Msalaba Wako mtukufu kwa ujasiri na bila hofu.  Ninapoalikwa kufuata nyayo Zako, ninatambua kwamba hofu inaweza kunizidi kama ilivyomzidi Petro.  Tafadhali unitie nguvu katika nyakati hizo na unipe neema ninayohitaji ili nikuambie “Ndiyo” bila kujali unachoniomba.  Yesu, nakutumainia.

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Tafakari za Maandiko Matakatifu kwa Kipindi cha Mwaka

Watakatifu/Sikukuu Zote

Mtakatifu wa Siku – Waanzilishi Watakatifu Saba wa Shirika la Watumishi wa Maria—Kumbukumbu ya Hiari

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu

Picha kuu hapo juu: Fedha ya Kodi, kazi ya Masaccio, kupitia Wikimedia Commons


Vitabu viwili bora kwa Kwaresima:

Tafakari za Kwaresima na Pasaka
Zimesasishwa kwa ajili ya Kwaresima & Pasaka 2022 kwa kuongezwa tafakari nyingine na Orodha ya Yaliyomo yenye maelezo ya kina zaidi

Tafakari za Kwaresima na Pasaka ni kimoja kati ya vitabu vinne vinavyounda Mfululizo wa Tafakari za Kila Siku za Kikatoliki. Kikiwa kitabu cha kukuza maisha ya kiroho, ni nyenzo bora kwa tafakari na sala za kila siku, kikitoa tafakari kuhusu Injili ya siku kwa namna inayohusiana na maisha ya vitendo, iliyo aminifu kwa imani na inayoeleweka kwa urahisi. Kimepangwa kwa namna inayowezesha kutumiwa katika mwaka wowote wa kiliturujia, kikitoa tafakari kwa kila chaguo la Injili, yakiwemo yale ya Jumapili katika Miaka A, B & C, kila chaguo la Misa Takatifu ya kila siku, na Sikukuu na Sherehe zote. Ruhusu kifo na ufufuko wa Kristo viubadilishe moyo wako kwa ukamilifu zaidi katika Kwaresima na Pasaka hii!  Kinapatikana pia katika mfumo wa kitabu chenye jalada laini & kitabu cha kielektroniki!

Siku 40 Chini ya Msalaba:
Mtazamo wa Upendo kutoka Moyoni mwa Mama Yetu Mwenye Heri

Kupitia kitabu hiki cha ibada ya kila siku, unaalikwa kutafakari kwa sala mawazo na moyo wa Mama yetu Mwenye Heri alipovumilia mateso makali aliyotendewa Mwanawe mwenyewe mpendwa.  Mama Maria aliukabili Msalaba wa Mwanawe kwa imani, upendo na moyo wa kujitoa ulio kamili. Uaminifu wake kwa Mwanawe katika maisha Yake yote haukuyumba. Aliposimama mbele ya Msalaba katika muda ule mrefu wa saa tatu, uaminifu huo haukukoma kamwe.