21 Machi 2022
Jumatatu ya Juma la Tatu la Kwaresima
Masomo ya Leo

Nafsi yangu ina kiu ya Mungu aliye hai. Nitaenda lini kuuona uso wa Mungu? (Tazama Zaburi 42:3)
Ni maneno mazuri mno kuweza kuyatamka. Usemi “kuwa na kiu” hautumiwi mara nyingi hivyo, lakini unastahili kutafakariwa wenyewe tu. Unafunua shauku na hamu ya kutuliziwa kiu si na Mungu tu, bali na “Mungu Aliye Hai!” Na ya “kuuona uso wa Mungu.”
Ni mara ngapi unatamani jambo kama hilo? Ni mara ngapi unaiacha hamu ya Mungu iwake ndani ya nafsi yako? Ni jambo la ajabu kuwa na hamu na shauku hii. Kwa kweli, hamu yenyewe inatosha kuanza kuleta uradhi mkubwa na utimilifu maishani.
Kuna simulizi la mtawa mmoja mzee aliyeishi maisha ya upweke akiwa padre na mlezi wa kiroho wa kikundi cha masista wa maisha ya monasterini. Kwa sehemu kubwa ya maisha yake, mtawa huyu aliishi maisha ya utulivu mkubwa, upweke, sala, masomo na kazi. Siku moja, karibu na mwisho wa maisha yake, aliulizwa jinsi alivyoyafurahia maisha yake kwa miaka hiyo yote. Mara moja, bila kusita, uso wake ukang’aa na kujaa furaha ya kina. Naye akasema kwa usadikisho mkubwa kabisa, “Nina maisha matukufu kweli! Kila siku ninajiandaa kufa.”
Mtawa huyu alikuwa na lengo moja maishani. Alikaza fikira zake kwenye uso wa Mungu. Hakuna jambo jingine lililokuwa na umuhimu wa kweli kwake. Alichokitamani na kukitarajia kila siku kilikuwa wakati ule ambapo angeingia katika maono hayo matukufu ya heri na kumwona Mungu uso kwa uso. Na wazo hilo ndilo lililomwezesha kuendelea mbele, siku baada ya siku, mwaka baada ya mwaka, akiadhimisha Misa Takatifu na kumwabudu Mungu kwa kujiandaa kwa mkutano huo mtukufu.
Una kiu ya nini? Ungekamilishaje kauli hii? “Nafsi yangu ina kiu ya…?” Ya nini? Mara nyingi mno tunakuwa na kiu ya mambo yasiyo na uhalisi na ya muda tu. Tunajitahidi sana kuwa na furaha, lakini mara nyingi sana hatuifikii. Lakini tukiziacha mioyo yetu iwake kwa shauku ya kile kilicho cha msingi, kile tulichoumbiwa, basi mambo mengine yote maishani yatakaa mahali pake. Mungu akiwekwa katikati ya shauku zetu zote, matumaini yetu yote na matamanio yetu yote, tutaanza kweli “kuuona uso wa Mungu” hapa na sasa. Hata kuuona utukufu wa Mungu kwa kiasi kidogo kabisa kutatutosheleza sana kiasi cha kubadili mtazamo wetu wote wa maisha na kutupa mwelekeo ulio wazi na wa hakika katika yote tunayofanya. Kila uhusiano utaguswa, kila uamuzi tunaofanya utaongozwa na Roho Mtakatifu, nasi tutagundua kusudi na maana ya maisha tunayotafuta. Kila tunapofikiria maisha yetu, tutang’aa tunapotafakari safari yetu na kutamani kusonga mbele katika safari hiyo kwa nguvu zetu zote, tukitarajia thawabu ya milele inayotungoja mwishoni.
Tafakari leo juu ya “kiu” yako. Usipoteze maisha yako kwa ahadi tupu. Usinaswe na mifungamano ya mambo ya kidunia. Mtafute Mungu. Utafute uso Wake. Yatafute mapenzi Yake na utukufu Wake, nawe hutataka kamwe kurudi nyuma kutoka katika mwelekeo ambao shauku hii inakupeleka.
Yesu, Mungu wangu Aliye Hai, nijalie siku moja niutazame uzuri Wako wote na utukufu Wako. Nijalie niuone uso Wako na kulifanya lengo hilo kuwa kiini cha maisha yangu. Utu wangu wote utawaliwe na shauku hii inayowaka, nami nizame katika furaha ya safari hii. Yesu, nakutumainia.
Siku 40 Chini ya Msalaba:
Mtazamo wa Upendo Kutoka Moyoni mwa Mama Yetu Mbarikiwa
Tafakari ya Kumi na Saba – Kuingia Yerusalemu
(Jumatatu ya Juma la Tatu la Kwaresima)
Tafakari juu ya Huruma ya Mungu
Tafakari za Maandiko Matakatifu kwa Kipindi cha Kwaresima
Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu
Vitabu viwili bora kwa Kwaresima:
Tafakari za Kwaresima na Pasaka
Zimesasishwa kwa ajili ya Kwaresima & Pasaka 2022 kwa kuongezwa tafakari nyingine na Orodha ya Yaliyomo yenye maelezo ya kina zaidi
Tafakari za Kwaresima na Pasaka ni kimoja kati ya vitabu vinne vinavyounda Mfululizo wa Tafakari za Kila Siku za Kikatoliki. Kikiwa kitabu cha kukuza maisha ya kiroho, ni nyenzo bora kwa tafakari na sala za kila siku, kikitoa tafakari kuhusu Injili ya siku kwa namna inayohusiana na maisha ya vitendo, iliyo aminifu kwa imani na inayoeleweka kwa urahisi. Kimepangwa kwa namna inayowezesha kutumiwa katika mwaka wowote wa kiliturujia, kikitoa tafakari kwa kila chaguo la Injili, yakiwemo yale ya Jumapili katika Miaka A, B & C, kila chaguo la Misa Takatifu ya kila siku, na Sikukuu na Sherehe zote. Ruhusu kifo na ufufuko wa Kristo viubadilishe moyo wako kwa ukamilifu zaidi katika Kwaresima na Pasaka hii! Kinapatikana pia katika mfumo wa kitabu chenye jalada laini & kitabu cha kielektroniki!
Siku 40 Chini ya Msalaba:
Mtazamo wa Upendo kutoka Moyoni mwa Mama Yetu Mwenye Heri
Kupitia kitabu hiki cha ibada ya kila siku, unaalikwa kutafakari kwa sala mawazo na moyo wa Mama yetu Mwenye Heri alipovumilia mateso makali aliyotendewa Mwanawe mwenyewe mpendwa. Mama Maria aliukabili Msalaba wa Mwanawe kwa imani, upendo na moyo wa kujitoa ulio kamili. Uaminifu wake kwa Mwanawe katika maisha Yake yote haukuyumba. Aliposimama mbele ya Msalaba katika muda ule mrefu wa saa tatu, uaminifu huo haukukoma kamwe.






