Kiswahili

Taswira za Uongo Kujihusu

Novemba 5, 2022
Jumamosi ya Juma la Thelathini na Moja la Wakati wa Kawaida
Masomo ya Leo

Video

Sikiliza kwa Kiingereza

Mafarisayo, waliopenda fedha, walisikia mambo haya yote, wakamdhihaki. Yesu akawaambia, “Ninyi mnajihesabia haki mbele ya watu, lakini Mungu anaijua mioyo yenu; kwa maana kinachothaminiwa na wanadamu ni chukizo mbele ya Mungu.”  Luka 16:14-15

“Mungu anaujua moyo!”  Huu ni ukweli mkuu sana unaostahili kutambuliwa kwa kina.  Mara nyingi maishani tunakuwa na mawazo yasiyo sahihi kuhusu wengine, nao wengine wanakuwa na mawazo yasiyo sahihi kutuhusu.  Kifungu hiki kinagusa kiini cha mwelekeo huu wa Mafarisayo wa kujijengea taswira ya uongo ili wengine waione, huku wakijali kidogo ukweli wa ndani ambao Mungu pekee anaujua.

Basi, ni nini kilicho muhimu zaidi kwako?  Unapendelea nini?  Je, unajali zaidi maoni ya wengine au ukweli wa maisha yako machoni pa Mungu?

Mapambano haya yanaweza kuwa ya namna mbili.  Kwa upande mmoja, kama Mafarisayo, tunaweza kujitahidi kujionyesha kwa wengine jinsi tusivyo, ilhali Mungu anaujua ukweli wote na anaijua taswira ya uongo tunayojaribu kuonyesha.  Kwa upande mwingine, tunaweza kugundua kwamba wengine wana taswira isiyo sahihi kuhusu sisi ni nani, jambo linaloweza kutuumiza sana.  Hili linapotokea, tunaweza kuchochewa kuwakasirikia wengine na kuelekea kujitetea kupita kiasi bila kufikiri kwa busara.

Lakini ni nini kilicho muhimu?  Ni nini kinachopaswa kutushughulisha?  Ukweli ndio ulio muhimu, nasi hatupaswi kuyapa uzito mkubwa mambo ambayo Mungu hayapi uzito.  Tunapaswa kujali tu yale yaliyo katika mawazo ya Mungu na kile anachofikiri kuhusu sisi na maisha yetu.

Tafakari leo juu ya mwelekeo wako wa kuhangaika kuhusu wengine wanavyokuona.  Jua kwamba Mungu anataka uishi maisha ya uaminifu, ukijionyesha jinsi ulivyo kwa kweli.  Usiwe kama Mafarisayo waliohangaikia kupita kiasi taswira za uongo na za kuwasifu ambazo wengine walikuwa nazo kuwahusu.  Jishughulishe tu na kuishi katika ukweli na yale yaliyo moyoni mwa Mungu, kisha umwachie Yeye yaliyobaki.  Hatimaye, hayo tu ndiyo yaliyo muhimu.

Bwana, nisaidie kuona yaliyo moyoni Mwako na nisaidie kujali tu jinsi Wewe unavyoniona.  Ninajua kwamba unanipenda na ninajua kwamba unataka niishi kikamilifu katika ukweli.  Upendo Wako na uongoze maisha yangu katika mambo yote.  Yesu, nakutumainia.

Mapya kwa Majilio na Krismasi!

Tafakari za Majilio na Krismasi

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Watakatifu/Sikukuu za Leo

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu

Picha iliyoangaziwa hapo juu:  Kristo miongoni mwa Mafarisayo, iliyochorwa na Jacob Jordaens, kupitia Wikimedia Commons