1 Februari 2023
Jumatano ya Juma la Nne la Kipindi cha Kawaida
Masomo ya Leo

Sikiliza kwa Kiingereza
“Je, huyu si yule seremala, mwana wa Maria, na ndugu yao Yakobo, Yosefu, Yuda na Simoni? Na dada zake hawapo hapa pamoja nasi?” Nao wakakwazika kwa sababu Yake. Marko 6:3
Baada ya kuzunguka vijijini akifanya miujiza, akifundisha umati wa watu na kupata wafuasi wengi, Yesu alirudi Nazareti ambako alikulia. Huenda wanafunzi Wake walifurahi kurudi pamoja na Yesu katika mji Wake wa asili, wakidhani kwamba watu wa mji Wake wangefurahi sana kumwona Yesu tena kwa sababu ya habari nyingi kuhusu miujiza Yake na mafundisho Yake yenye mamlaka. Lakini muda si muda, wanafunzi hao wangekutana na jambo la kushangaza sana.
Baada ya kufika Nazareti, Yesu aliingia katika sinagogi kufundisha, Naye akafundisha kwa mamlaka na hekima iliyowastaajabisha wenyeji. Wakaambiana, “Mtu huyu ameyapata wapi haya yote? Ni hekima gani hii aliyopewa?” Walichanganyikiwa kwa sababu walimjua Yesu. Alikuwa yule seremala wa hapo aliyefanya kazi kwa miaka mingi pamoja na baba Yake aliyekuwa seremala. Alikuwa mwana wa Maria, nao waliwajua ndugu Zake wengine kwa majina.
Kikwazo kikuu kwa watu wa mji wa Yesu kilikuwa kumzoea kwao. Walimjua. Walijua alikoishi. Walimfahamu alipokuwa akikua. Waliijua familia Yake. Walijua kila kitu kumhusu. Kwa hiyo, walijiuliza jinsi Yesu angeweza kuwa mtu wa pekee. Angewezaje sasa kufundisha kwa mamlaka? Angewezaje sasa kufanya miujiza? Hivyo, watu wa mji huo walistaajabu, nao wakaacha mshangao huo ugeuke kuwa shaka, hukumu na ukosoaji.
Sisi sote hukabiliana na jaribu hilo hilo mara nyingi zaidi kuliko tunavyoweza kutambua. Mara nyingi ni rahisi zaidi kuvutiwa na mtu tusiyemjua tukiwa mbali kuliko na mtu tunayemjua vizuri. Tunaposikia kwa mara ya kwanza habari za mtu anayefanya jambo la kupendeza, ni rahisi kuungana na wengine katika kuvutiwa naye. Lakini tunaposikia habari njema kuhusu mtu tunayemjua vizuri, tunaweza kushawishika kwa urahisi kuwa na wivu au husuda, na kuwa na mashaka na hata kumkosoa. Lakini ukweli ni kwamba kila mtakatifu ana familia. Na katika kila familia kunaweza kuwa na ndugu wa kiume na wa kike, binamu na jamaa wengine ambao Mungu atafanya mambo makuu kupitia kwao. Hili halipaswi kutushangaza—linapaswa kututia moyo! Nasi tunapaswa kufurahi wakati Mungu wetu mwema anapowatumia kwa nguvu wale walio karibu nasi na ambao tumewazoea.
Tafakari leo kuhusu watu uliowazoea maishani, hasa watu wa familia yako mwenyewe. Jichunguze uone kama unapata ugumu wa kuona zaidi ya yale yanayoonekana kwa nje na kukubali kwamba Mungu anakaa ndani ya kila mtu. Tunapaswa daima kutafuta kuutambua uwepo wa Mungu kila mahali tulipo, hasa katika maisha ya wale tunaowajua vizuri sana.
Bwana wangu uliyepo daima, nakushukuru kwa njia zisizohesabika ambazo kwa hizo upo katika maisha ya watu wote wanaonizunguka. Nipe neema ya kukuona na kukupenda katika maisha ya wale walio karibu nami zaidi. Kadiri ninavyotambua uwepo Wako wenye utukufu katika maisha yao, nijaze shukrani za dhati na unisaidie kuutambua upendo Wako unaodhihirika kupitia maisha yao. Yesu, nakutumainia.
Tafakari juu ya Huruma ya Mungu
Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu




