Kiswahili

Kutumia Mamlaka

5 Juni 2023
Jumatatu ya Wiki ya Tisa ya Kipindi cha Kawaida
Masomo ya Leo

Mtakatifu Bonifasi, Askofu na Shahidi—Kumbukumbu

Video

Sikiliza kwa Kiingereza

Yesu alianza kusema na wakuu wa makuhani, waandishi na wazee kwa mifano. “Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu, akalizungushia ua, akachimba shimo la kukamulia zabibu, akajenga mnara. Kisha akalikodisha kwa wakulima wapangaji, akaenda safari. Wakati ulipofika, alimtuma mtumishi kwa wale wapangaji ili apokee kutoka kwao sehemu ya mazao ya shamba la mizabibu. Lakini wakamkamata, wakampiga, wakamrudisha mikono mitupu.” Marko 12:1–3

Huyu alikuwa wa kwanza kati ya watumishi “wengi” ambao mwenye shamba la mizabibu aliwatuma kwa wapangaji ili wapokee sehemu ya mazao ya shamba hilo. Baadhi ya watumishi walitendewa vibaya, wengine walipigwa na wengine waliuawa. Mwishowe, mwenye shamba alimtuma mwanawe. Wapangaji walimuua, wakidhani kwamba wangerithi shamba la mizabibu ikiwa mwana huyo angekufa.

Muktadha wa mfano huu ni muhimu. Yesu alikuwa ametoka tu kuingia Yerusalemu mwanzoni mwa Wiki Takatifu ya kwanza, ambayo hatimaye ingehitimishwa kwa kifo na ufufuko Wake. Siku iliyotangulia, Yesu alikuwa amelisafisha Hekalu kwa kuwafukuza wabadilishaji fedha. Wakuu wa makuhani, waandishi na wazee walikasirika sana, wakaanza kupanga njama za kumuua. Yesu aliwaelekezea wao hasa mfano huu.

Ili kuuelewa mfano huu, unahitaji kuelewa kila mhusika anamwakilisha nani. Viongozi wa kidini wa Israeli walikuwa wale wapangaji, shamba la mizabibu lilikuwa taifa la Wayahudi, Mungu Baba alikuwa yule mtu aliyepanda shamba la mizabibu, watumishi wengi waliotumwa kukusanya mazao walikuwa manabii wa kale, na Yesu alikuwa Mwana Mpendwa aliyeuawa. Mfano unahitimisha kwa kusema kwamba mwenye shamba la mizabibu (Mungu Baba) atawaua wapangaji na kuwapa wengine shamba hilo. Kwa maneno mengine, muda si mrefu waandishi, Mafarisayo, wakuu wa makuhani na wazee wangenyang’anywa mamlaka yao ya kidini, nayo yangepewa Mitume na waandamizi wao. Kwa hiyo, mfano huu unatupatia muhtasari wa jinsi Kanisa lilivyoanzishwa.

Ni vyema kutambua kwamba viongozi wa kidini wa wakati huo walijua kuwa Yesu alikuwa akiwaelekezea mfano huu, lakini hawakuzingatia fundisho lake. Kwa hakika, kama wangekuwa tayari kuipokea zawadi ya imani, wangetambua kwamba walikuwa wakijaribu kumwibia Mungu “shamba la mizabibu.” Walikuwa wakijaribu kuudhibiti Ufalme wa Israeli na kuuendesha kwa masilahi yao, kuufanya ufanane na wao wenyewe, na kupuuza mapenzi ya Mungu aliyeuanzisha.

Mfano huu ni muhimu hasa kwa yeyote aliye na aina fulani ya mamlaka matakatifu. Wazazi hutumia mamlaka nyumbani. Maaskofu na mapadre hutumia mamlaka ndani ya Kanisa. Nasi sote hutumia mamlaka fulani ya kiroho tunapojitahidi kutimiza utume wetu wa pekee maishani. Fundisho la mfano huu ni rahisi: usitumie mamlaka yako vibaya. Usitumie mamlaka kulingana na mapenzi yako mwenyewe; yatumie kwa unyenyekevu kulingana na mapenzi ya Mungu pekee. Kila kiongozi, daima na kila mahali, lazima aongoze kulingana na mawazo na mapenzi ya Mungu. Wakishindwa kufanya hivyo, watapata madhara yake.

Tafakari leo namna yoyote ambayo Mungu amekukabidhi wajibu wa kiroho wa kutimiza utume Wake katika ulimwengu huu. Mtu anapokabidhiwa wajibu wa kuongoza, anakabidhiwa pia mamlaka ya kiroho ya kutimiza wajibu huo kulingana na mawazo na mapenzi ya Mungu. Hili linahitaji unyenyekevu wa kudumu ili mapenzi ya Mungu pekee ndiyo yatimizwe. Jitahidi kutumia mamlaka yote kulingana na mawazo na mapenzi ya Mungu, na shamba la mizabibu ulilokabidhiwa kulitunza litazaa matunda mema kwa wingi.

Baba mwenye upendo, umechagua kunituma, kama mpangaji katika Ufalme Wako, nizae matunda mema kwa ajili ya uzima wa milele. Tafadhali nisaidie daima kutumia mamlaka na kutimiza wajibu niliokabidhiwa kwa unyenyekevu ili nijitahidi kutimiza mapenzi Yako, na mapenzi Yako pekee. Yesu, nakutumainia.

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Watakatifu/Sikukuu Zote

Mtakatifu wa Siku – Mtakatifu Bonifasi, Askofu na Shahidi

Tafakari za Maandiko Matakatifu kwa Kipindi cha Mwaka

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu

Picha iliyoangaziwa hapo juu: Mfano wa Shamba la Mizabibu (mojawapo ya mfululizo wa picha kumi na mbili za matukio ya Maisha ya Kristo) Msanii:Jan Rombouts, kupitia Wikimedia Commons