Kiswahili

Kina Kipya cha Huruma

19 Juni 2023
Jumatatu ya Juma la Kumi na Moja la Kipindi cha Mwaka
Masomo ya Leo

Mtakatifu Romualdo, Abate—Kumbukumbu ya Hiari

Video

Sikiliza kwa Kiingereza

Mtu akikulazimisha kumtumikia kwa kwenda maili moja, nenda naye maili mbili. Mpe anayekuomba, wala usimpe kisogo anayetaka kukopa kwako.” Mathayo 5:41–42

Kadiri imani ya Israeli ilivyokua kwa karne nyingi kabla ya kuja kwa Kristo, kulikuwa na hatua mbalimbali za maendeleo katika maadili. Kabla ya kuwekwa kwa sheria za maadili katika Agano la Kale, ilikuwa kawaida kwa familia kulipiza kisasi kikali dhidi ya familia nyingine zilizokuwa zimewadhuru. Hilo lilisababisha vurugu na uhasama usiokoma. Lakini hatua ya maendeleo ilifikiwa ilipowekwa sheria ya kulipiza kisasi iliyosema, “Mtu akimtia jirani yake kilema, atatendewa kama alivyotenda: mvunjiko kwa mvunjiko, jicho kwa jicho, jino kwa jino; kama alivyomtia mtu kilema, ndivyo naye atakavyotiwa kilema” (Mambo ya Walawi 24:19–20). Huu ulikuwa mfumo mpya wa haki uliokataza kisasi kuwa kikali kuliko kosa lililokuwa likilipiziwa kisasi. Wakati huo, hili lilisaidia kukomesha uhasama wa kudumu kati ya familia uliokuwa ukizidi kuwa mkali.

Ni sheria hii ya kulipiza kisasi ambayo Yesu anaizungumzia katika Injili yetu ya leo. Mfumo mpya wa maadili ulio bora zaidi sana ambao Yesu alifundisha uliwataka wanafunzi Wake “wasimpinge mtu mwovu” na wageuze shavu la pili walipotendewa uovu. Ingawa haki kwa ukamilifu wake inadai malipizi kwa ajili ya dhambi, fundisho jipya la Yesu lilikuwa kwamba huruma hulipa kila deni. Kwanza, huruma Yake tunayopewa kwa ajili ya msamaha wa dhambi zetu hulipa deni la dhambi zetu tunapotubu kwa kweli na kubadilika. Lakini ikiwa tunatamani madeni yetu kwa Mungu kutokana na dhambi zetu yasamehewe na kulipwa, basi ni lazima sisi pia tuwatendee wengine vivyo hivyo, bila kuweka kinyongo chochote dhidi yao.

Lakini Yesu anaenda mbali zaidi. Katika kifungu kilichonukuliwa hapo juu, Yesu anawahimiza wanafunzi Wake kuishi mapendo na ukarimu kwa namna mpya na yenye kuleta mabadiliko ya msingi. Kanuni hizi mpya za maadili zilielekeza jinsi watoto wa Ufalme wa Mungu walivyoitwa sasa kuishi. Haikutosha tu kusamehe na kusahau deni ambalo mtu anadaiwa nawe kwa sababu ya dhambi yake. Sasa huruma inatutaka “tumpe anayeomba” na kutembea “maili mbili” na mtu anayekuomba utembee naye maili moja tu. Kwa maneno mengine, mapendo ya Kikristo yanazidi kwa mbali kila dhana ya haki kwa ukamilifu wake, na hata yanavuka mipaka ya msamaha wa msingi. Hakika hili lilikuwa fundisho jipya kutoka kwa Bwana wetu, lenye kuleta mabadiliko ya msingi.

Fikiria sheria hii mpya ya maadili katika maisha yako mwenyewe. Ni kiwango gani cha “haki” ambacho kwa kawaida zaidi unakifuata maishani? Mtu anapokukosea, je, unaishi kama wale walioishi kabla ya sheria za Agano la Kale, kwa kutafuta kulipiza kisasi kwa kiwango kikubwa hata kuliko madhara uliyotendewa? Je, unaishi kwa kufuata sheria inayotafuta haki ya kulipa sawa kwa sawa, jicho kwa jicho? Je, unatafuta kusamehe na kuonyesha huruma kama malipo ya deni ambalo mwingine amejitwika kwa dhambi aliyokutendea? Au, kama inavyopasa hasa, je, unajitahidi kwenda hata zaidi ya tendo la kusamehe na kutoa huruma kwa namna mpya, ya ukarimu na yenye wingi usio na kipimo? Kiwango hiki cha mwisho cha upendo ni kigumu kukifikia na kukiishi, lakini hivi ndivyo Bwana wetu anavyotutendea, na ndivyo anavyotuita tuwatendee wengine.

Tafakari leo juu ya uchungu wowote ambao huenda unapambana nao kwa sasa. Pia fikiria jinsi ambavyo umekuwa ukikabiliana na uchungu huo. Unapotafuta kuielewa sheria hii mpya ya upendo na huruma iliyotolewa na Bwana wetu, mwombe akupe neema unayohitaji ili kuwaonyesha wengine huruma kwa kiwango kilekile ambacho Mungu anakuonyesha wewe.

Bwana wangu mkarimu, unatoa huruma Yako kwa wingi usio na kipimo. Hutusamehi tu tunapotubu, bali pia unaturejesha kwenye viwango vya juu vya utakatifu vinavyozidi sana vile ambavyo tungeweza kustahili. Unipe neema ninayohitaji, Bwana mpendwa, ili kuwaonyesha wale walionikosea huruma na upendo kwa kiwango hichohicho. Ninawasamehe wote walioniumiza. Tafadhali unisaidie pia kuwapenda kwa moyo wangu wote. Yesu, nakutumainia.

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Tafakari za Maandiko Matakatifu kwa Kipindi cha Mwaka

Watakatifu/Sikukuu Zote

Mtakatifu wa Siku – Mtakatifu Romualdo, Abate

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu

Picha zilizoangaziwa hapo juu:  Madirisha yanayoonyesha Mahubiri ya Mlimani katika kanisa la Kireformati la Herzogenbuchsee karibu na Berne. Mchoro wa Eugène Burnand, kazi ya kioo ya Emil Gerster wa Basel, kupitia Wikimedia Commons