Kiswahili

Unyenyekevu wa Maombezi

Septemba 18, 2023
Jumatatu ya Wiki ya Ishirini na Nne ya Kipindi cha Kawaida
Masomo ya Leo

Video

Sikiliza kwa Kiingereza

“Bwana, usijisumbue, kwa maana sistahili Wewe kuingia chini ya dari yangu. Kwa hiyo, sikujiona ninastahili kuja Kwako; lakini sema neno, na mtumishi wangu apone.” Luka 7:6–7

Jambo la kuvutia ni kwamba maneno haya ya unyenyekevu ya akida wa Kirumi hayakusemwa na akida huyo mwenyewe kwa Yesu. Hii ni kwa sababu akida huyo hakuamini kwamba alistahili hata kwenda kwa Yesu yeye mwenyewe. Kwa hiyo, aliwatuma baadhi ya rafiki zake wamwambie Yesu maneno haya kwa niaba yake. Kwa hakika, rafiki za akida huyu walikuwa waombezi mbele ya Yesu. Yesu alijibu kwa kuonyesha jinsi alivyostaajabia imani ya akida huyo. Yesu akauambia umati uliokuwa pamoja Naye, “Nawaambieni, hata katika Israeli sijapata imani kama hii.” Na wakati huo, Yesu alimponya mtumishi huyo akiwa mbali.

Mara nyingi, tunapokuwa na ombi muhimu la kumwomba mtu mwingine, tunafanya hivyo sisi wenyewe. Tunamwendea mtu huyo na kuzungumza naye ana kwa ana. Na ingawa kwa hakika tunaweza kumwendea Bwana wetu katika sala, ana kwa ana, sisi wenyewe mbele Yake, kuna unyenyekevu mkubwa katika kupeleka mahitaji yetu kwa Bwana wetu kwa njia ya maombezi ya mtu mwingine. Hasa, kuna unyenyekevu mkubwa katika kuomba maombezi ya watakatifu.

Kutafuta maombezi ya watakatifu mbele ya Bwana wetu hakufanywi kwa sababu tunamwogopa Bwana wetu au kwa sababu angechukizwa nasi kumwendea moja kwa moja. Kwa namna iliyo bora, hufanywa kama tendo la unyenyekevu wa hali ya juu kabisa. Tunapowakabidhi sala yetu wale walio Mbinguni, wanaoutazama uso wa Mungu, kwa kweli tunamkabidhi Mungu sala yetu. Lakini kutegemea maombezi ya watakatifu pia ni njia ya kukiri kwamba kwa mastahili yetu wenyewe hatustahili kusimama mbele ya Bwana na kumpelekea ombi letu. Nyakati fulani inaweza kuwa vigumu kuelewa unyenyekevu huu, lakini ni muhimu kujaribu.

Ni jambo gani katika maisha yako unalohitaji kuliombea sasa hivi? Unapolikumbuka jambo hilo, chagua mtakatifu awe rafiki yako na mwombezi wako mbele ya Mungu. Mwelekee mtakatifu huyo kwa unyenyekevu na umwombe, ukikiri kwamba hustahili kumwendea Bwana wetu wewe mwenyewe. Kisha mkabidhi mtakatifu huyo ombi lako na umwombe awasilishe sala hiyo kwa Bwana wetu kwa niaba yako. Kusali kwa Bwana wetu kwa njia ya maombezi ya mtakatifu ni njia pia ya kusema kwamba unatambua kuwa jibu la Yesu kwako linatokana na huruma Yake tu. Na habari njema ni kwamba Yesu anatamani sana kutumiminia huruma Yake tunapojinyenyekeza mbele Yake, hasa tunapomwendea kwa njia ya upatanishi wa watakatifu.

Tafakari leo juu ya unyenyekevu wa akida huyu wa Kirumi aliyeheshimiwa sana. Jaribu kuelewa nguvu ya njia yake ya unyenyekevu, alipotuma rafiki zake kwa Yesu kwa niaba yake. Unapofanya hivyo, chagua mtakatifu aliye Mbinguni na umwombe aende kwa Bwana wetu kwa niaba yako, akamwombe Bwana wetu akujalie unyenyekevu na imani kama za akida huyu. Kufanya hivyo kutamfanya Bwana wetu astaajabie pia imani na unyenyekevu wako.

Watakatifu wa Mungu, tafadhali mtolee Yesu ombi langu la unyenyekevu kwamba nizidi kukua katika unyenyekevu na imani. Bwana wangu mpendwa, ninaleta ombi hili na sala zangu zote Kwako. Ninapofanya hivyo, ninakiri kwamba sistahili Huruma Yako ya Kimungu. Lakini kwa njia ya upatanishi wa watakatifu walioko Mbinguni, ikiwa ni mapenzi Yako kunijalia huruma Yako, basi ninakuomba hili kwa unyenyekevu kupitia kwao. Mama Maria, ninakabidhi hasa sala zangu zote kwa maombezi Yako matakatifu. Yesu, nakutumainia.

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Tafakari za Maandiko Matakatifu kwa Kipindi cha Mwaka

Watakatifu/Sikukuu za Leo

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu

Picha iliyoangaziwa hapo juu: Yesu na Akida, iliyochorwa na Paolo Veronese, kupitia Wikimedia Commons