Mei 13, 2024
Jumatatu ya Juma la Saba la Pasaka
Masomo ya Leo
Mama Yetu wa Fatima—Kumbukumbu ya Hiari

Sikiliza kwa Kiingereza
“Nimewaambia haya ili mpate kuwa na amani ndani Yangu. Ulimwenguni mtapata dhiki, lakini jipeni moyo, nimeushinda ulimwengu.” Yohane 16:33
Yesu aliwaambia nini wanafunzi Wake kilichowaletea “amani” aliyozungumzia? Anarejelea hasa hotuba Yake yote ya Karamu ya Mwisho ambayo tumekuwa tukiisoma. Maneno aliyosema katika hotuba hii yote yanalenga kuwapa wanafunzi, na sisi pia, “ujasiri” na uwezo wa kushinda dhiki tunazoletewa na ulimwengu.
Katika hotuba Yake yote, Yesu anaelekeza fikra zetu hasa kwenye umoja alio nao na Baba Yake na ukweli kwamba tukibaki tumeungana na Yesu, tutakuwa pia tumeungana na Baba. Alijizungumzia kuwa Yeye ni mzabibu na sisi ni matawi ambayo lazima yabaki yameungana imara na Yesu. Alisema kwamba jambo hili linawezekana tu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu atakayekuja, ambaye Yeye atamtuma. Pia alizungumzia chuki ya ulimwengu dhidi ya wote wanaobaki wamejikita imara katika Ukweli. Kwa hiyo, ikiwa wewe ni mtu unayetafuta kubaki umekita mizizi ndani ya Kristo, ukiwa umejazwa Roho Mtakatifu na kujitenga na udanganyifu wa ulimwengu wenye mtazamo wa kidunia na usio wa Kikristo, basi ni wazi kwamba Yesu anazungumza nawe.
Katika kifungu hiki hapo juu, Yesu anataja zawadi moja itakayotusaidia katika safari hii. Zawadi hii ni amani Yake. Amani ni uwezo wa kubaki watulivu na makini katikati ya kila aina ya “dhiki” tunayokutana nayo. Dhiki ambazo Wakristo watakabili hasa ni mateso mbalimbali kutoka kwa ulimwengu tunapoishi kulingana na Ukweli. Na ingawa kuna kweli nyingi za kimaadili zinazofundishwa wazi na imani yetu ambazo ulimwengu unazishambulia, kuna pia aina nyingine za dhiki tutakazokutana nazo ulimwenguni leo.
Mojawapo ya taabu zilizo wazi zaidi ambazo ulimwengu unawasababishia watu wengi ni kukumbwa daima na vichocheo vya kuona, kusikia na vya kiakili. Ulimwengu wetu umejaa kelele. Vifaa vya kisasa vya elektroniki, vyombo vya habari, matangazo ya biashara, redio, Intaneti, mitandao ya kijamii na mambo mengine mengi ya maisha yetu ya kila siku vina athari ya hila ya kutukengeusha, kutuchochea na kutunyang’anya amani ya Kristo.
Fikiria, kwa mfano, kuingia katika ukimya wa mafungo kwa siku moja, mbili au zaidi. Ungejisikiaje kuzima simu yako janja, kishikwambi, kompyuta, televisheni na redio kwa muda mrefu? Je, ungepatwa na aina fulani ya mahangaiko kwa kuacha vitu ulivyovizoea? Watu wengi leo kwa kweli wangeona jambo hili kuwa gumu. Sababu yake ni kwamba “amani” ambayo Yesu anaizungumzia inapungua polepole katika maisha ya watu wengi. Badala ya amani ya Mungu, tumejaa kelele, vurugu na shughuli zisizokoma. Huu ndio “ulimwengu” unaotushambulia na kutunyang’anya amani ambayo Mungu anataka kutujalia.
Tafakari leo ukweli huu wenye umuhimu wa pekee—kwamba Yesu anataka uijue amani Yake moyoni mwako. Naye anataka amani hiyo ikutegemeze. Tafakari pambano la ndani linaloweza kutokea ndani yako kati ya ulimwengu na amani ya Kristo. Ni nani anayeshinda pambano hilo la kuipata nafsi yako? Je, ni ulimwengu au amani ya Kristo inayotawala zaidi ndani yako? Itafute amani ambayo Yesu pekee ndiye anayeitoa, nawe unapoigundua amani Yake, utagundua pia chanzo cha amani hiyo: Yesu mwenyewe.
Bwana wa amani yote, umetuita tutoke ulimwenguni ili amani Yako ikae ndani yetu, ikitutegemeza na kutupa ujasiri, hekima na nguvu. Ninayafungua maisha yangu Kwako, Bwana mpendwa, na ninaomba kwamba mambo mengi yanayonivuruga na misukosuko ninayoletewa na ulimwengu vianze kukoma. Daima niisikie sauti Yako ya upole na kukufuata hadi mahali pa pumziko la kimya panapopatikana ndani Yako tu. Yesu, nakutumainia.
Novena kwa Roho Mtakatifu
Husaliwa kwa ajili ya kujiandaa kwa Pentekoste
Ijumaa, Mei 10 – Jumamosi, Mei 18
Tafakari juu ya Huruma ya Mungu
Mtakatifu wa Siku – Mama Yetu wa Fatima
Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu




