Kiswahili

Utuokoe, Bwana!

Julai 2, 2024
Jumanne ya Wiki ya Kumi na Tatu ya Kipindi cha Mwaka
Masomo ya Leo

Video

Sikiliza kwa Kiingereza

Yesu alipopanda mashuani, wanafunzi wake walimfuata. Ghafla dhoruba kali ikatokea baharini, hata mashua ikawa inafunikwa na mawimbi; lakini Yeye alikuwa amelala. Mathayo 8:23–24

Tukio hili liliwagusa sana wanafunzi, kama inavyothibitishwa na ukweli kwamba limeandikwa katika Injili zote tatu za Sinoptiki. Tunaona hili pia katika maneno ya mwisho ya simulizi hili baada ya Yesu kuituliza dhoruba: “Watu hao walishangaa, wakasema, ‘Huyu ni mtu wa namna gani, ambaye hata pepo na bahari vinamtii?’”

Kwa mapokeo, simulizi hili limefasiriwa kuwa taswira ya Kanisa kwa ujumla na pia ya nafsi ya kila mmoja. Mashua ni taswira ya Kanisa ambalo ndani yake sisi Wakristo tunapita katikati ya hatari za maisha haya. Ni lazima tubaki ndani ya Kanisa ili tusipotee. Kila mtu ndani ya mashua anamwakilisha kila mmoja wetu aliye mshiriki wa Kanisa. Dhoruba kali ni taswira ya mahangaiko mengi ya binafsi tunayovumilia maishani, na pia ya mateso ambayo Kanisa limevumilia na litaendelea kuvumilia mpaka mwisho wa nyakati.

Dhoruba ilipoikumba mashua, Yesu alikuwa amelala. Lakini alikuwa amelala kwa sababu fulani. Tunapotazama historia ya wanadamu, hasa historia ya Kanisa, tunaona nyakati nyingi ambapo Mungu ameonekana kutokuwapo au kuwa “amelala” wakati misukosuko, mateso na taabu zilipojitokeza. Watu wengi, kama si wote, wamepatwa na hali kama hiyo wakati fulani maishani. Wanafunzi wanapokumbwa na dhoruba hii, wanatuonesha njia bora ya kusali tunapojaribiwa kukata tamaa maishani. Wanamwamsha Yesu na kusema, “Bwana, utuokoe! Tunaangamia!” Na ingawa Yesu anawakemea kwa kukosa imani na kwa hofu yao, pia anaitikia vilio vyao na kuituliza dhoruba.

Wanafunzi walipaswa kufanya nini katika hali hii? Je, walipaswa kutumaini na kumwacha Yesu aendelee kulala? Ingawa Bwana wetu aliwakemea kwa kukosa imani, simulizi hili kimsingi linafunua huruma ya Mungu tunapojaribiwa kuogopa. Mungu anajua kwamba nyakati fulani sote tutajihisi kulemewa na kujikuta tukijaribiwa kwa namna hii. Anajua kwamba imani yetu si kamilifu, na kwa hiyo aliwaruhusu wanafunzi Wake watuwekee mfano huu. Hivyo, kila tunapojikuta tumelemewa na kujawa na hofu maishani, tunapaswa kumlilia atuokoe. Anataka tumgeukie.

Tafakari leo juu ya sala hii ya wanafunzi. Ukijikuta unakabiliwa na hali fulani ngumu sana katika maisha yako binafsi, au tatizo kubwa zaidi la kifamilia ambalo bado halijatatuliwa, au unazidi kutambua mahangaiko mengine yanayolikumba Kanisa au jamii kwa ujumla, basi jaribu kuiga sala hii ya wanafunzi: “Bwana, utuokoe! Tunaangamia!” Ingawa mwanzoni maneno haya yanaweza kuonekana kuwa maneno ya kukata tamaa, kwa kweli ni maneno ya matumaini na kutumaini. Yanatuelekeza Kwake Yeye aliye chanzo pekee cha amani tunayoitafuta katika nafsi zetu, familia zetu, Kanisa na ulimwengu wetu. Tambua namna mbalimbali ambazo wewe na wengine mnahisi kuwa “mnaangamia,” na umlilie Bwana wetu kwa moyo wako wote akuokoe wewe na wote wenye uhitaji.

Bwana mwenye nguvu kuu, ninastaajabia uwezo Wako wa kimungu na jinsi unavyoweza kutuliza kabisa dhoruba zinazowatesa watu Wako. Tafadhali nijaze matumaini na unyenyekevu ili nisisite kamwe kukugeukia ninapokuwa na uhitaji, na pia kukulilia ili uendelee kuingilia kati katika maisha ya wengine. Amka, ee Bwana, uwaokoe watu Wako, kwa maana bila Wewe hakika tutaangamia! Yesu, nakutumainia.

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Tafakari za Maandiko Matakatifu kwa Kipindi cha Mwaka

Watakatifu/Sikukuu za Leo

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu

Picha: Yesu Anatuliza Dhoruba – Mchoro wa fresko uliochorwa na Silvestro Pistolesi katika sehemu ya juu yenye madirisha ya Kanisa la Kugeuka Sura kwa Yesu katika Community of Jesus, kupitia Wikimedia Commons