Kiswahili

Je, Wewe ni “Mkristo wa Kufuata Mkumbo?”

Julai 24, 2020
Ijumaa ya Wiki ya Kumi na Sita ya Kipindi cha Kawaida
Masomo ya Leo

Mtakatifu Sharbel Makhlūf, Padri, Mtawa wa Kujitenga—Kumbukumbu ya Hiari

Sikiliza kwa Kiingereza

“Mbegu iliyopandwa penye miamba ni yule anayelisikia neno na kulipokea mara moja kwa furaha. Lakini hana mizizi na hudumu kwa muda tu. Dhiki au mateso yanapotokea kwa sababu ya neno, mara moja huanguka.”  Mathayo 13:20-21

Je, wewe ni “Mkristo wa kufuata mkumbo?”  Huenda hii ni istilahi mpya.  Lakini inagusa kiini cha hali ya Mkristo huyu aliyeelezwa hapo juu.  Kifungu hiki kinaeleza mojawapo ya aina nne za Wakristo zinazotajwa katika Mfano wa Mpanzi.  Kuna walio kama mbegu iliyopandwa njiani, wengine kama mbegu iliyopandwa penye miamba, wengine kama mbegu iliyopandwa katikati ya miiba, na wengine kama mbegu iliyopandwa kwenye udongo wenye rutuba.  Kila moja ya maelezo haya hutupatia mengi ya kutafakari.

Tumtazame Mkristo aliye kama mbegu iliyopandwa penye miamba, yule asiye na mizizi.  Katika maisha ya kila siku, huyu ndiye mtu anayeweza kuitwa “Mkristo wa kufuata mkumbo.”  Ni mtu anayekiri imani katika Kristo wakati imani hiyo inapendwa na kukubalika sana na wengine.  Mambo yanapokuwa rahisi na yanapomfaa, mtu huyu hujitoa kikamilifu.  Lakini mara tu Injili, Neno la Mungu, linapopingwa kwa namna fulani, na ghafla kumfuata Kristo hakupendwi tena katika utamaduni unaomzunguka, mtu huyu hufanya haraka kuuchagua utamaduni badala ya Ukweli.

Hili ni jambo linalotokea kweli katika nyakati zetu.  Utamaduni na ulimwengu kwa ujumla vinazidi kuuchukia ukweli wa imani yetu ya Kikristo.  Ulimwengu unazidi kuwa na nguvu, kuwa na ushawishi mkubwa zaidi, na kuwa mnyanyasaji zaidi, na unaonekana kushinda pambano.  Hili ni tatizo.  Na tatizo hasa linatokana na Wakristo wengi mno kutokuwa na mizizi ya kina katika maisha yao ya imani.

Lililo bora ni Neno la Mungu kupandwa ndani kabisa ya mioyo yetu, penye udongo wenye rutuba.  Hilo linapotokea, Neno hukua na kuwa lenye nguvu na imara.  Na katikati ya “dhoruba” ya kitamaduni au kijamii, Mkristo mwenye mizizi ya kina na imani ya kina hatayumba.

Tafakari leo kama uko tayari kabisa au la kusimama pamoja na Kristo na kuutetea Ukweli, hata iwe vigumu kiasi gani au hata kama watu hawapendi msimamo huo.  Je, uko tayari kustahimili dhihaka na upotoshaji ambao ulimwengu unauelekezea Ukweli?  Je, uko tayari kubaki imara katika imani yako katikati ya jamii inayozidi kuyaweka kando mambo ya Mungu?  Ikiwa unapambana na hali ya kuwa “Mkristo wa kufuata mkumbo,” sali ili Mungu aizamishie mizizi Yake ndani kabisa ya moyo wako, ili usiyumbe hata ikugharimu kiasi gani.

Bwana, ninatamani Neno Lako lizame ndani kabisa ya moyo wangu.  Ninatamani kubaki imara katika imani yangu hata inigharimu kiasi gani.  Nisaidie kujitoa kikamilifu katika imani yangu na katika upendo wangu katika mambo yote.  Yesu, nakutumainia.

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Watakatifu/Sikukuu Zote

Mtakatifu wa Siku – Mtakatifu Sharbel Makhlūf, Padri, Mtawa wa Kujitenga

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu

Picha: Kutokea Mlimani huko Galilaya, kazi ya Duccio di Buoninsegna