Machi 14, 2021
Jumapili ya Nne ya Kwaresima (Mwaka B)
Masomo ya Leo
Tanbihi: Huu ni Mwaka B wa Liturujia. Hata hivyo, masomo ya Mwaka A yanaweza kutumiwa badala yake zinapofanyika ibada za uchunguzi kwa wale wanaojiandaa kupokea Sakramenti siku ya Pasaka.
Masomo ya Mwaka A (Zinapofanyika ibada za uchunguzi)

Sikiliza kwa Kiingereza
“Kwa maana Mungu aliupenda ulimwengu hivi hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila anayemwamini asiangamie bali awe na uzima wa milele.” Yohane 3:16
Kifungu hiki cha Maandiko Matakatifu kutoka Injili ya Yohane kinafahamika sana. Mara nyingi, katika mikusanyiko mikubwa ya umma kama vile mashindano ya michezo, tunaweza kumwona mtu akiwa ameinua bango linalosema, “Yohane 3:16.” Sababu yake ni kwamba kifungu hiki kinatoa muhtasari rahisi lakini ulio wazi wa Injili nzima.
Kuna kweli nne za msingi tunazoweza kujifunza kutokana na kifungu hiki cha Maandiko Matakatifu. Hebu tuangalie kila moja kwa ufupi.
Kwanza, inawekwa wazi kwamba Baba wa Mbinguni anatupenda. Tunajua hili, lakini hatutaweza kamwe kuelewa kikamilifu kina cha ukweli huu. Mungu Baba anatupenda kwa upendo wa kina na mkamilifu. Ni upendo wenye kina kuliko kitu kingine chochote tunachoweza kukipitia maishani. Upendo Wake ni mkamilifu.
Pili, upendo wa Baba ulidhihirishwa kwa zawadi ya Mwanawe Yesu. Baba kutupatia Mwanawe ni tendo la upendo mkuu. Mwana alikuwa kila kitu kwa Baba, na zawadi ya Mwana kwetu ina maana kwamba Baba anatupatia kila kitu. Anatupatia uhai Wake mwenyewe katika Nafsi ya Yesu.
Tatu, mwitikio pekee unaofaa kwa zawadi kama hiyo ni imani. Lazima tuamini kwamba kumpokea Mwana katika maisha yetu kuna nguvu ya kutubadilisha. Lazima tuione zawadi hii kuwa zawadi inayotupatia yote tunayohitaji. Lazima tumpokee Mwana katika maisha yetu kwa kuamini utume Wake na kujitoa Kwake kwa maisha yetu pia.
Nne, matokeo ya kumpokea na kujitoa Kwake kwa maisha yetu pia ni kwamba tunaokolewa. Hatutaangamia katika dhambi yetu; bali tutapewa uzima wa milele. Hakuna njia nyingine ya wokovu isipokuwa kwa njia ya Mwana. Lazima tuujue ukweli huu, tuuamini, tuukubali na kuushikilia kwa moyo wote.
Tafakari leo juu ya muhtasari huu wa Injili nzima. Usome tena na tena na kuukariri. Onja utamu wa kila neno na ujue kwamba kwa kukikubali kwa moyo wote kifungu hiki kifupi cha Maandiko Matakatifu, unaukubali ukweli wote wa Mungu.
Baba wa Mbinguni, nakushukuru kwa zawadi kamilifu ya Kristo Yesu, Mwana Wako. Kwa kutupatia Yesu, unatupatia Moyo Wako na Nafsi Yako yenyewe. Nijifungue Kwako kikamilifu zaidi na kuipokea zawadi kamilifu ya Yesu katika maisha yangu. Ninakuamini Wewe, Mungu wangu. Tafadhali niongezee imani na upendo. Yesu, nakutumainia.
Siku 40 Chini ya Msalaba – Tafakari ya Ishirini na Tano – Yesu Anaanguka
Novena kwa Mtakatifu Yosefu
Machi 10–18
Tafakari juu ya Huruma ya Mungu
Tafakari za Maandiko Matakatifu kwa Kipindi cha Kwaresima
Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu
Picha zilizoangaziwa hapo juu: Kusulubiwa, kazi ya Anthony van Dyck





