Kiswahili

Mamlaka ya Yesu Iko Wazi

11 Januari 2022
Jumanne ya Wiki ya Kwanza ya Kipindi cha Kawaida
Masomo ya Leo

Video

Sikiliza kwa Kiingereza

Yesu alifika Kafarnaumu pamoja na wafuasi wake, na siku ya sabato akaingia katika sinagogi na kufundisha. Watu walistaajabia mafundisho yake, kwa maana aliwafundisha kama mwenye mamlaka, wala si kama waandishi. Marko 1:21-22

Tunapoingia katika Wiki hii ya Kwanza ya Kipindi cha Kawaida, tunaoneshwa picha ya Yesu akifundisha katika sinagogi.  Naye anapofundisha, ni wazi kwamba kuna jambo la pekee kumhusu.  Yeye anafundisha kwa mamlaka mapya.

Kauli hii katika Injili ya Marko inaonesha tofauti kati ya Yesu na waandishi, ambao wanaonekana kufundisha bila mamlaka hii iliyo dhahiri. Hatupaswi kuipita kauli hii bila kuitilia maanani.

Yesu alitumia mamlaka Yake katika kufundisha, si hasa kwa sababu alitaka kufanya hivyo, bali kwa sababu ilimbidi. Ndivyo alivyo. Yeye ni Mungu, na anaposema, husema kwa mamlaka ya Mungu. Anasema kwa namna ambayo watu wanatambua kwamba maneno Yake yana maana yenye kuleta mabadiliko. Maneno Yake huleta mabadiliko katika maisha ya watu.

Hili linapaswa kumwalika kila mmoja wetu kutafakari juu ya mamlaka ya Yesu katika maisha yetu. Je, unatambua mamlaka Yake katika maneno anayokuambia? Je, unaona maneno Yake yaliyonenwa katika Maandiko Matakatifu yakileta mabadiliko katika maisha yako?

Tafakari leo juu ya taswira hii ya Yesu akifundisha katika sinagogi. Jua kwamba “sinagogi” linawakilisha nafsi yako mwenyewe, na kwamba Yesu anatamani kuwapo humo akisema nawe kwa mamlaka. Acha maneno Yake yaingie ndani mwako na kuyabadilisha maisha yako.

Bwana wangu mwenye mamlaka, ninajifungua Kwako na kwa sauti Yako yenye mamlaka.  Nisaidie nikuruhusu kusema kwa uwazi na ukweli.  Unapofanya hivyo, nisaidie niwe tayari kukuruhusu ubadilishe maisha yangu.  Yesu, nakutumainia.

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Tafakari za Maandiko Matakatifu kwa Kipindi cha Mwaka

Watakatifu/Sikukuu za Leo

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu

Picha iliyoangaziwa hapo juu: Kristo akifundisha Kapernaumu Imechorwa na Maurycy Gottlieb, kupitia Wikimedia Commons


Kitabu Kilichoangaziwa:

Tafakari za Kila Siku kwa Kipindi cha Kawaida:
Majuma 1-17

Tafakari za Kila Siku kwa Kipindi cha Mwaka: Wiki 1–17 kutoka katika Mfululizo wa Tafakari za Kila Siku za Kikatoliki ni kitabu cha ibada ya kila siku kinachotoa tafakari kuhusu Injili ya siku kwa namna ya vitendo, aminifu kwa imani na inayoendana na maisha ya kawaida.  Matoleo ya kitabu cha kielektroniki na kitabu chenye jalada laini yamepangwa kwa namna inayowezesha kitabu hiki kutumiwa mwaka baada ya mwaka. Tafakari hazijawekewa tarehe mahususi za Kipindi cha Mwaka cha 2022, bali zinajumuisha kila chaguo la masomo kwa mwaka huu wa kiliturujia na miaka ijayo, na hivyo kukifanya kuwa kitabu cha ibada kinachoweza kutumiwa mwaka baada ya mwaka.