Februari 24, 2022
Alhamisi ya Juma la Saba la Kipindi cha Kawaida
Masomo ya Leo

Sikiliza kwa Kiingereza
“Kila mtu atatiwa chumvi kwa moto. Chumvi ni nzuri, lakini chumvi ikipoteza ladha yake, mtairudishia ladha kwa kitu gani? Iweni na chumvi ndani yenu, nanyi mtakuwa na amani ninyi kwa ninyi.” Marko 9:49-50
Je, uko tayari “kutiwa chumvi kwa moto?” Yesu anaweka wazi kwamba kila mtu atapitia huku “kutiwa chumvi.” Basi, hili lina maana gani hasa?
Kuongeza chumvi kwenye chakula huleta ladha yake. Si kwamba hukibadilisha chakula kiwe kitu kingine; bali huboresha kilichopo, na kukifanya kiwe na ladha zaidi.
Chumvi pia husafisha. Hutumika kuhifadhi chakula kisiharibike na husaidia kukiondolea bakteria. Inafaa kutafakari mifano hii miwili ya kukoleza ladha na kuhifadhi chakula.
“Kutiwa chumvi kwa moto” maana yake ni kwamba tunatakaswa na Mungu. Moto hutakasa na kusafisha. Joto hutumika kuua vijidudu kwenye vyombo, moto hutumika kusafisha dhahabu, na pia hutumika kufinyanga madini ya thamani kuwa maumbo au vito.
Ndivyo ilivyo kwetu pia. Lazima tutakaswe na moto wa Mungu kwa kila namna. Dhambi lazima iondolewe, nasi lazima tulainishwe na moto wa Mungu ili tuweze kufinyangwa kwa mfano Wake wa kimungu.
Lakini hili hutokeaje? Njia moja ni pale tunapoondolewa tamaa na hamu zote za mwili zilizo za ubinafsi na zinazopingana na mapenzi ya Mungu. Hili linaweza kuwa lenye uchungu, na ndiyo sababu ya kutumia mfano wa moto. Njia nyingine ni pale tunapotakaswa katika kina cha roho yetu. Hili linaweza kutokea tunapopewa msalaba mzito wa kubeba, nasi tukafanya hivyo kwa saburi na kuukubali. Utashi wetu unapokabiliwa na changamoto na kujaribiwa, tunapata nafasi ya kuukabidhi kwa Mungu na kuchagua mapenzi Yake. Lakini mara nyingi mapenzi Yake yanajumuisha kukubali kikamilifu mateso yoyote tunayovumilia. Katika hali hiyo, mateso yanaweza kututakasa katika kina kabisa cha utashi wetu na, hivyo, kuwa njia ya ukombozi kwetu.
Tafakari leo juu ya kazi ya Mungu ya kutakasa maishani mwako. Tafakari hasa namna zozote unavyohisi uchungu wa mateso fulani ambayo hutaki kuyakubali. Jua kwamba kuyakubali kikamilifu mateso haya kunaweza kwa kweli kuleta utakaso ambao Mungu anautaka maishani mwako, ili kukufanya uwe mtakatifu na safi kweli.
Bwana wangu unayenitakasa, nakuomba uitakase roho yangu na kuiondolea dhambi zote. Kwanza, nisaidie kuwekwa huru kutoka katika mafungamano yote ya kimwili yanayozuia upendo wangu Kwako. Pia, nisaidie kutofungwa na matakwa yangu mwenyewe. Mateso na msalaba katika maisha yangu viwe neema ya kweli ambayo kwayo unaniweka huru na kunisaidia kuimarika katika saburi na kila fadhila. Najitoa Kwako, Bwana mpendwa. Yesu, nakutumainia.
Tafakari juu ya Huruma ya Mungu
Tafakari za Maandiko Matakatifu kwa Kipindi cha Mwaka
Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu
Vitabu viwili bora kwa Kwaresima:
Tafakari za Kwaresima na Pasaka
Zimesasishwa kwa ajili ya Kwaresima & Pasaka 2022 kwa kuongezwa tafakari nyingine na Orodha ya Yaliyomo yenye maelezo ya kina zaidi
Tafakari za Kwaresima na Pasaka ni kimoja kati ya vitabu vinne vinavyounda Mfululizo wa Tafakari za Kila Siku za Kikatoliki. Kikiwa kitabu cha kukuza maisha ya kiroho, ni nyenzo bora kwa tafakari na sala za kila siku, kikitoa tafakari kuhusu Injili ya siku kwa namna inayohusiana na maisha ya vitendo, iliyo aminifu kwa imani na inayoeleweka kwa urahisi. Kimepangwa kwa namna inayowezesha kutumiwa katika mwaka wowote wa kiliturujia, kikitoa tafakari kwa kila chaguo la Injili, yakiwemo yale ya Jumapili katika Miaka A, B & C, kila chaguo la Misa Takatifu ya kila siku, na Sikukuu na Sherehe zote. Ruhusu kifo na ufufuko wa Kristo viubadilishe moyo wako kwa ukamilifu zaidi katika Kwaresima na Pasaka hii! Kinapatikana pia katika mfumo wa kitabu chenye jalada laini & kitabu cha kielektroniki!
Siku 40 Chini ya Msalaba:
Mtazamo wa Upendo kutoka Moyoni mwa Mama Yetu Mwenye Heri
Kupitia kitabu hiki cha ibada ya kila siku, unaalikwa kutafakari kwa sala mawazo na moyo wa Mama yetu Mwenye Heri alipovumilia mateso makali aliyotendewa Mwanawe mwenyewe mpendwa. Mama Maria aliukabili Msalaba wa Mwanawe kwa imani, upendo na moyo wa kujitoa ulio kamili. Uaminifu wake kwa Mwanawe katika maisha Yake yote haukuyumba. Aliposimama mbele ya Msalaba katika muda ule mrefu wa saa tatu, uaminifu huo haukukoma kamwe.






