(Tanbihi: Kuna tafakari mbili hapa chini: ‘Alhamisi ya Juma la Sita la Pasaka hutumika katika majimbo ambako Sherehe ya Kupaa kwa Bwana Mbinguni huhamishiwa Jumapili ya Saba ya Pasaka. Kwa majimbo yanayoadhimisha Kupaa kwa Bwana Mbinguni leo, bofya hapa au sogeza ukurasa chini.)
Kutoka Huzuni hadi Furaha
Mei 26, 2022
Alhamisi ya Juma la Sita la Pasaka (Sherehe ya Kupaa kwa Bwana Mbinguni inapohamishiwa Jumapili)
Masomo ya Leo
Mtakatifu Filipo Neri, Padre—Kumbukumbu

Sikiliza kwa Kiingereza
“Amina, amina, nawaambia, mtalia na kuomboleza, huku ulimwengu ukifurahi; mtahuzunika, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha.” Yohane 16:20
Huzuni, maombolezo na hata kulia ni sehemu ya maisha. Mara nyingi watoto hulia wanapokabiliwa na shida ndogo tu, lakini sisi sote hukabili huzuni na uchungu katika maisha yetu yote.
Katika kifungu hicho hapo juu, Yesu anawaambia Mitume Wake kwamba huzuni na uchungu vitakuwa sehemu ya maisha yao. Haya ni maneno mazito sana kutoka kwa Bwana wetu, lakini yanaeleza hali halisi. Kuwambia Mitume Wake waziwazi kuhusu taabu zitakazowakabili ni tendo la upendo kwa upande Wake.
Habari njema ni kwamba Yesu anafuatisha kauli hii kwa habari yenye matumaini kwamba “huzuni yao itageuka kuwa furaha.” Hii ndiyo sehemu muhimu zaidi ya yale anayosema Yesu.
Ndivyo ilivyo pia katika maisha yetu. Yesu hatuahidi kwamba maisha yetu hayatakuwa na taabu na maumivu. Hatuambii kwamba kumfuata kunamaanisha kuwa kila kitu kitakuwa rahisi maishani. Badala yake, anataka tujue kwamba tukichagua kumfuata, tutatembea katika nyayo Zake. Aliteseka, alitendewa vibaya na hatimaye akauawa. Na huo ungekuwa msiba kama hatimaye asingefufuka kutoka kwa wafu, kupaa Mbinguni na kugeuza huzuni na maumivu yote yaliyotangulia kuwa njia yenyewe ya wokovu wa ulimwengu.
Tukitembea katika nyayo Zake, tunahitaji kuona kwamba kila huzuni katika maisha yetu inaweza kuwa njia ya neema kwa wengi. Tukiweza kukabiliana na taabu za maisha kwa imani na matumaini, hatimaye hakuna kitakachoweza kutushinda, na kila kitu kitaweza kutumika kwa utukufu wa Mungu na kuleta furaha kuu.
Tafakari leo juu ya maneno haya ya Yesu. Jua kwamba hakuwa akiwaambia Mitume Wake tu, bali pia wewe. Usikwazike wala kushtuka unapokumbana na shida fulani maishani. Usikate tamaa unapokabiliwa na mateso. Yakabidhi mambo yote kwa Bwana wetu na umruhusu ayageuze kuwa furaha anayoahidi mwishoni.
Bwana wa matumaini yote, nakukabidhi mateso yote katika maisha yangu. Naweka mikononi Mwako majonzi yangu, taabu, huzuni na fadhaa. Ninaamini kwamba Wewe ni mwenyezi na unatamani kuvigeuza vitu vyote viwe njia ya kuudhihirisha utukufu Wako. Nijalie matumaini ninapokata tamaa, na nikutumainie maisha yanapokuwa magumu. Yesu, nakutumainia.
Novena kwa Roho Mtakatifu
Husaliwa kujiandaa kwa Pentekoste
Kuanzia Ijumaa, Mei 27
Tafakari juu ya Huruma ya Mungu
Mtakatifu wa Siku – Mtakatifu Filipo Neri, Padre
Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu
+++
(Katika majimbo mengi ulimwenguni kote, Sikukuu ya Kupaa kwa Bwana Mbinguni huhamishiwa Jumapili hii ijayo)
Kutoa Ushuhuda kwa Injili
Sherehe ya Kupaa kwa Bwana Wetu Mbinguni (Mwaka C)

Sikiliza kwa Kiingereza
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Ndivyo ilivyoandikwa kwamba Kristo atateswa na kufufuka kutoka kwa wafu siku ya tatu, na kwamba toba kwa ajili ya msamaha wa dhambi itahubiriwa kwa jina lake kwa mataifa yote, kuanzia Yerusalemu. Ninyi ni mashahidi wa mambo haya. Na tazameni, ninawapelekea ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni mjini mpaka mvikwe nguvu kutoka juu.” Luka 24:46–49
Na kwa hayo, utume wa Yesu hapa duniani ulikamilika, Naye akapaa Mbinguni. Au kweli ulikamilika? Je, utume Wake ulikamilika? Ndiyo, lakini tu kwa maana kwamba kazi ya Bwana wetu ya kuangamiza mauti na kutoa uzima mpya ilitimizwa kwa maisha Yake, kifo Chake na ufufuko Wake. Asili ya kibinadamu sasa ilialikwa kushiriki katika uzima mpya wa neema.
Katika sala, jiwazie umesimama pamoja na Bwana wetu juu ya mlima wa Kupaa Mbinguni. Unapomtazama, wazia kwamba ulikuwa pia pamoja Naye katika kipindi chote cha huduma Yake ya hadharani. Wazia ukishuhudia miujiza Yake mingi, jinsi alivyoziongoa hata mioyo migumu kuliko yote, mamlaka aliyosema nayo, kukamatwa Kwake, kuteswa Kwake, kifo Chake na kisha Ufufuko Wake. Wazia ukiiona mikono na miguu Yake, iliyotobolewa hapo awali, sasa iking’aa kwa utukufu kutoka katika majeraha hayo. Unapomwona Bwana wetu namna hii, wazia akikutazama kwa upendo na kukuambia kwamba amechagua kukutuma ulimwenguni uwe shahidi Wake na wa yote uliyoyaona na kuyapitia. Unapaswa kwenda ukishiriki Habari Njema ya maisha Yake, kifo Chake na ufufuko Wake na wote unaokutana nao.
Kwanza, Bwana wetu kwa hakika amekushirikisha maisha Yake yote. Kwa kusoma Injili, unakuwa shahidi wa moja kwa moja wa yote Yesu aliyoyafanya na kuyatimiza. Neno Lake ni hai, na linakufunulia Nafsi Yake mwenyewe, kama lilivyofanya kwa wafuasi Wake wa kwanza. Pili, kwa kweli Yesu anakuita uende ukashiriki Injili hii hai na ulimwengu. Kwa hiyo, ni muhimu kutafakari jinsi unavyoweza kufanya jambo hilo. Unawezaje kutoa ushuhuda wa Ufufuko wa Kristo? Unawezaje kubadili maisha ya watu? Unawezaje kuendeleza utume wa Yesu mwenyewe?
Ahadi ambayo Bwana wetu aliwapa wanafunzi juu ya mlima wa Kupaa Mbinguni ni ahadi uliyopewa wewe pia. Anaahidi kumtuma Roho Mtakatifu juu yako ili akuvike “nguvu kutoka juu.” Ni kwa kuzipokea nguvu hizo na kuzitumia kikamilifu tu ndipo utaweza kutimiza utume ambao Bwana wetu amekupa. Kwa hiyo, je, utakuwa tayari kumpokea Roho Mtakatifu na kujitoa kuendeleza utume wa Kristo?
Kama tungeuelewa kikamilifu utume tulioupokea kutoka kwa Yesu, ungetujaza kicho kitakatifu. Lakini mara nyingi sana, kutambua kile Mungu anachotaka kwetu hutujaza badala yake hofu isiyo takatifu. Tunafikiria kuwainjilisha wengine, kushiriki imani yetu nao, kuushuhudia ukweli kwa matendo yetu, kuwapenda adui zetu na kuishi kwa ajili ya Injili pekee, na yote hayo yanaweza kuonekana kuwa yanazidi uwezo wetu. Ikiwa ndivyo ilivyo kwako, basi ujue kwamba hofu hii isiyo takatifu inaweza kuondolewa ili nafasi yake ichukuliwe na kipawa cha kicho kitakatifu. Kicho kitakatifu ni kipawa cha Roho Mtakatifu kinachotuchochea kutambua ukuu wa Mungu unaostahili kicho na utume tunaopewa, kwa kukutana nao moja kwa moja. Kinatuhamasisha, kinatutia moyo na kutuacha tukiwa tumejaa mshangao na kicho. Kutoka hapo, kipawa hiki na kila kipawa kingine cha Roho Mtakatifu hutuwezesha kutimiza utume wa Kristo usio na mwisho.
Tafakari leo juu ya utume maalumu ambao Mungu amekupa. Katika sala, mtazame Yesu akiwa amesimama juu ya mlima wa Kupaa Mbinguni na kukutazama. Anapofanya hivyo, mwache akufunulie si Nafsi Yake mwenyewe tu, bali pia namna yako maalumu ya kushiriki katika utume Wake unaoendelea wa kushirikisha Habari Njema hadi miisho ya dunia. Pokea utume huo kwa ujasiri, furaha na kicho kitakatifu. Uuheshimu, uufurahie kwa kina, uutafakari na kuukubali. Jitoe katika ushiriki huu wenye utukufu katika maisha ya Kristo kwa kujitoa kuwa shahidi wa Kristo hadi mwisho wa maisha yako duniani.
Bwana wangu uliyepaa mbinguni, ulipoingia kwa mwili na roho katika uwepo kamili na wenye utukufu wa Baba Yako, uliwakabidhi wanafunzi Wako wajibu wa kukamilisha utume Wako duniani. Ninaisikia miito Yako maishani mwangu, Bwana mpendwa, nami ninajitoa kwa kazi tukufu ya kuendeleza utume huo duniani. Tafadhali nitumie utakavyo na unijaze nguvu kutoka juu ili niweze kusaidia kulieneza Neno Lako la wokovu hadi miisho ya dunia. Yesu, nakutumainia.
Novena kwa Roho Mtakatifu
Husaliwa kujiandaa kwa Pentekoste
Kuanzia Ijumaa, Mei 27
Tafakari juu ya Huruma ya Mungu
Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu
Soma Zaidi – Kupaa Mbinguni
Tafakari ya Sala kwa ajili ya Kupaa Mbinguni
Picha: Kupaa Mbinguni, kazi ya Benjamin West, kupitia Wikipedia





