Kiswahili

Vilele vya Utakatifu

Juni 12, 2023
Jumatatu ya Juma la Kumi la Kipindi cha Kawaida
Masomo ya Leo

Video

Sikiliza kwa Kiingereza

Yesu alipoona makutano, alipanda mlimani, naye alipokwisha kuketi, wanafunzi Wake walimjia. Akaanza kuwafundisha, akisema: “Heri walio maskini wa roho, kwa maana Ufalme wa mbinguni ni wao.” Mathayo 5:1–3

Leo tunapewa wito wa hali ya juu ajabu unaopatikana katika zile Heri ili tuutafakari. Yesu alifundisha masomo haya kwenye kilima kilichoko kaskazini kidogo ya Bahari ya Galilaya. Watu wengi walikuwa wakimjia Yesu ili kumsikiliza akihubiri na kushuhudia miujiza Yake mingi. Walimiminika Kwake katika eneo hili la mbali, na Yesu akawafanya waketi kwa kuegemea alipokuwa akihubiri yale ambayo sasa yanajulikana kama “Mahubiri ya Mlimani.” Mahubiri haya yanapatikana katika Sura ya 5 hadi 7 ya Injili ya Mathayo, na yalitolewa muda mfupi baada ya Yesu kuanza huduma Yake ya hadharani.

Ni mwanzo wa ajabu namna gani wa huduma Yake ya hadharani! Mafundisho haya ya Yesu yalikuwa mapya kabisa na bila shaka yaliwaacha watu wengi wakiwa wameshangaa sana. Yesu hakufundisha tena maagizo ya Agano la Kale pekee, kama vile Amri Kumi; sasa aliinua sheria ya maadili hadi kiwango ambacho hakikuwahi kufikiriwa hapo awali.

Watu walipokuwa wakimsikiliza mwalimu huyu mpya akizungumza kwa mamlaka na hekima mpya, huenda walisisimka na kuchanganyikiwa kwa wakati mmoja. Kuwa na njaa na kiu ya haki, kuwa wenye huruma na safi wa moyo, na kuwa wapatanishi huenda yalikuwa mambo yanayokubalika. Lakini kwa nini kuwa maskini, wenye huzuni na wapole kulihesabiwa kuwa baraka? Na jambo lililokuwa gumu hata zaidi kueleweka ni hili: kwa nini ilikuwa vizuri kuteswa kwa ajili ya haki au kutukanwa na kusingiziwa kwa sababu ya Yesu?

Fundisho jipya la Yesu linaloleta mabadiliko ya msingi linapoeleweka wazi, si wanafunzi Wake wa kwanza tu ambao huenda walichanganyikiwa na kusisimka kwa wakati mmoja. Wewe pia, ikiwa kweli unasikiliza mafundisho Yake na kuelewa anachomaanisha, utagundua kwamba yanaweza kukupa changamoto inayogusa kiini cha nafsi yako. Fundisho la Yesu lazima likubaliwe kikamilifu na bila kusita.

Mafundisho ya Heri ni wito wetu wa kuwa wakamilifu. Yanatuwekea wazi njia tunayopitia kufikia vilele vya utakatifu na kuupata utukufu wa Mbinguni. Ni ramani yetu ya njia iliyo sahihi na yenye maelezo ya kina, inayotuongoza kwenye utimilifu wa furaha na shangwe. Lakini pia yanatuita tufanye mabadiliko ya kina katika fikra zetu na matendo yetu. Si mafundisho yanayokubaliwa “kwa urahisi,” kwa maana yanatutaka tuache kila mwelekeo wa ubinafsi tulio nao na kuchagua kuishi tukiwa huru kutoka katika kila kishawishi cha kidunia, kila kifungo cha moyo na kila dhambi. Ukamilifu unawangoja wale wanaosikiliza, kuelewa na kukubali mafundisho ya Heri.

Tafakari leo juu ya mwanzo wa Mahubiri haya ya Mlimani yenye changamoto. Jitahidi kupata muda wa kusali ukitafakari kila tamko la Heri. Ni kwa sala na tafakari pekee ndipo maana kamili ya kila mojawapo ya mialiko hii ya kuwa watakatifu itakapoeleweka. Anza na wito wa kuwa maskini wa roho ndani ya moyo wako. Tamko hili la Heri linatuita tusifungamane kabisa na chochote kisicho sehemu ya mapenzi ya Mungu. Kutoka hapo, fikiria umuhimu wa kuiombolezea dhambi yako, wa kutafuta usafi wa moyo na unyenyekevu katika mambo yote. Tafakari kila tamko la Heri na utenge muda kwa lile linalokupa changamoto zaidi. Bwana wetu ana mengi ya kukuambia kupitia mahubiri haya. Usisite kumruhusu akuongoze hadi kwenye vilele vya utakatifu kupitia mahubiri haya.

Bwana wa utakatifu wote, Wewe ni mkamilifu kwa kila namna. Uliishi kila fadhila na kila tamko la Heri kwa ukamilifu. Unipe neema ya kufungua moyo wangu Kwako ili nikusikie ukiniita kwenye ukamilifu wa maisha, na ili niitikie kwa ukarimu kwa maisha yangu yote. Unifanye mtakatifu, Bwana mpendwa, ili niipate furaha na utimilifu unaotaka kunijalia. Yesu, nakutumainia.

Novena kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu
Tarehe za Novena: Juni 7-15, 2023
Juni 16, 2023: Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Tafakari za Maandiko Matakatifu kwa Kipindi cha Mwaka

Watakatifu/Sikukuu za Leo

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu

Picha kuu hapo juu: Flickr