Aprili 29, 2024
Kumbukumbu ya Mtakatifu Katarina wa Siena, Bikira na Mwalimu wa Kanisa
Masomo ya Leo
Masomo ya Jumatatu ya Wiki ya Tano ya Pasaka

Sikiliza kwa Kiingereza
“Nimewaambia haya nikiwa pamoja nanyi. Mtetezi, Roho Mtakatifu ambaye Baba atamtuma kwa jina langu—Yeye atawafundisha kila kitu na kuwakumbusha yote niliyowaambia.” Yohane 14:25–26
Wakati mwingine tunasahau yote ambayo Mungu ametuambia. Kwa mfano, tunaweza kuutambua wazi uwepo wa Mungu maishani mwetu kupitia mambo fulani, kama vile ufahamu wa kina wa kiroho tunaoupata katika sala, usadikisho wa ndani kwamba tumesikia sauti Yake kupitia mahubiri, uhuru unaotubadilisha tunaoupata kupitia Sakramenti ya Upatanisho, au kuelewa jambo kwa uwazi usio na shaka tunaposoma Maandiko Matakatifu. Mungu anaposema nasi, akitujalia Ukweli Wake, nguvu, msamaha na kila namna nyingine ya neema, tunafarijiwa kiroho tunapohisi ukaribu Wake. Lakini tunapopatwa na matatizo, tunaweza kusahau kwa urahisi nyakati hizo tulipoelewa mambo kwa uwazi.
Bila shaka wanafunzi walipata matukio mengi yaliyowasaidia kuelewa mambo kwa uwazi katika miaka mitatu ya huduma ya Yesu hadharani. Walistaajabia mamlaka ya kiroho waliyotambua katika mahubiri Yake, walishuhudia miujiza isiyohesabika, walitazama wenye dhambi wakiwekwa huru, walimwona Yesu akigeuka sura katika utukufu, na walimwona Bwana wetu akisali kwa kina kwa Baba. Kila mara walipoona nguvu ya Mungu ikitenda kazi, bila shaka usadikisho wao uliongezeka kwamba Yesu alikuwa Masihi, Mwana wa Mungu, Mwokozi wa Ulimwengu. Lakini Yesu alijua pia kwamba imani ya wanafunzi hao Kwake ingetetereka muda si mrefu. Alijua kwamba, walipokuwa wakitazama kwa hofu kutoka mbali Yesu akikamatwa, akipigwa na kuuawa, wangeanza kusahau yote waliyokuwa wameyaona na kuyapitia hapo awali. Hofu inaweza kusababisha mkanganyiko, na Yesu alijua kwamba wanafunzi Wake wangeanguka katika mtego huo muda si mrefu. Kwa sababu hiyo, Yesu aliwaambia wanafunzi Wake maneno yaliyo hapo juu. Aliwaahidi kwamba Roho Mtakatifu angewashukia hivi karibuni ili awafundishe kila kitu na kuwakumbusha yote aliyowaambia.
Ingekuwa vizuri sana kama kila somo tulilowahi kujifunza kutoka kwa Mungu lingeendelea kuwa kipaumbele chetu maishani. Ingekuwa vizuri sana kama tusingeruhusu kamwe hofu ituchanganye na kutufanya tusahau yote ambayo Mungu ametuambia kwa njia mbalimbali. Kama vile Yesu alivyojua kwamba wanafunzi wangehitaji msaada wa Roho Mtakatifu ili wakumbuke, anajua pia kwamba sisi tunahitaji msaada huohuo wa Roho Mtakatifu. Kwa hiyo, maneno yaliyo hapo juu waliyoambiwa wanafunzi yanaelekezwa kwetu pia. “Mtetezi, Roho Mtakatifu ambaye Baba atamtuma kwa jina langu—Yeye atawafundisha kila kitu na kuwakumbusha yote niliyowaambia.”
Ni masomo gani ya imani uliyojifunza zamani ambayo unahitaji kukumbushwa? Ni kazi ya Roho Mtakatifu kutukumbusha masomo hayo kila tunapoyahitaji. Kwa hiyo, tunapokaribia adhimisho tukufu la Sherehe ya Pentekoste, huu ni wakati mzuri wa kusali kwa Roho Mtakatifu na kuomba kipawa cha kukumbuka njia nyingi ambazo Mungu amejifunua kwetu. Baba, Mwana na Roho Mtakatifu hutenda kazi kwa upatano mkamilifu, lakini kila mmoja ana jukumu la pekee katika maisha yetu. Jukumu la Roho Mtakatifu ni hasa kutuongoza siku kwa siku katika kutimiza mapenzi ya Baba, yaani tufananishwe kikamilifu na Nafsi ya Kristo Yesu.
Tafakari leo juu ya ahadi hii yenye nguvu ambayo Bwana wetu aliwapa wanafunzi Wake na sisi pia. Sali kwa Roho Mtakatifu. Kuwa tayari kupokea mwongozo wa Roho unaoendelea katika maisha yako, wala usiruhusu kamwe hofu ikuletee mkanganyiko. Badala yake, mruhusu Mungu aondoe mkanganyiko wote na akukumbushe yote ambayo amekuambia katika maisha yako yote.
Bwana Yesu mwenye utukufu mkuu, uliwaahidi wanafunzi na watu Wako wote kwamba Roho Mtakatifu angetumwa kwetu kutukumbusha yote uliyoyafunua. Roho Mtakatifu, tafadhali endelea kunishukia, kunifundisha na kuniongoza. Unisaidie nisisahau kamwe masomo mengi niliyofundishwa, ili nisiruhusu kamwe hofu iniletee mkanganyiko. Yesu, nakutumainia.
Tafakari juu ya Huruma ya Mungu
Tafakari za Maandiko Matakatifu kwa Kipindi cha Pasaka
Mtakatifu wa Siku – Mtakatifu Katarina wa Siena, Bikira na Mwalimu wa Kanisa
Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu




