Kiswahili

Kutumwa na Kristo

Jumatatu, 28 Oktoba 2024

Sikukuu ya Watakatifu Simoni na Yuda, Mitume

Masomo ya Leo

Ugolino di Nerio, Mali ya umma, kupitia Wikimedia Commons

Video

Sikiliza kwa Kiingereza

Yesu alipanda mlimani kusali, akakesha usiku kucha akimwomba Mungu. Kulipopambazuka, aliwaita wanafunzi Wake, akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao pia aliwaita Mitume…  Luka 6:12

Simoni na Yuda walikuwa miongoni mwa wale wachache sana walioteuliwa na Yesu Mwenyewe kuwa Mitume Wake. Simoni tunayemkumbuka leo si Simoni Petro, wala Yuda tunayemkumbuka leo si Yuda Iskarioti. Ni machache yanayojulikana kuhusu Mitume hawa wawili. Katika Injili, Simoni anatajwa kuwa Mzelote, jambo ambalo huenda lilimaanisha kwamba alikuwa mwanachama wa kundi lenye msimamo mkali zaidi ndani ya dini ya Kiyahudi. Yuda anajulikana sana kama Mtakatifu Msimamizi wa Mambo Yasiyo na Matumaini. Wengine wanapendekeza kwamba hii ni kwa sababu mara nyingi alikuwa Mtume wa mwisho ambaye waamini wa kwanza Wakristo walimwomba awaombee, kwa kuwa jina lake lilikuwa sawa na la Yuda Iskarioti, na kumwomba Yuda awaombee kuliwakumbusha watu yule msaliti. Ikiwa ndivyo ilivyokuwa, basi katika maongozi ya Mungu, kwa kuwa Yuda akawa Mtume wa mwisho kuombwa awaombee, pia akawa tumaini la mwisho kwa wengi na, hivyo, mtakatifu msimamizi wa wale waliokuwa na mambo ambayo kwa kweli yalionekana kutokuwa na matumaini.

Mapokeo fulani yanaeleza kwamba Watakatifu Simoni na Yuda wanatajwa pamoja katika Kanuni ya Kirumi na pia wanaadhimishwa katika sikukuu moja kwa sababu wote wawili waliuawa kwa ajili ya imani pamoja siku ileile, huenda huko Siria, Lebanoni au Uajemi. Hata hivyo, habari halisi kuhusu safari zao za kimisionari na kuuawa kwao kwa ajili ya imani haziko wazi. Lakini jambo moja lililo hakika kuhusu Mitume hawa ni kwamba walikuwa Mitume. Walichaguliwa na Bwana wetu na kuwekwa Naye kuwa wawili kati ya maaskofu wa kwanza wa Kanisa letu, nao walipewa agizo la kueneza Injili hadi miisho ya dunia.

Kwa mtazamo wetu wa leo, kuwa mmoja wa wale Kumi na Wawili waliochaguliwa ni heshima ya ajabu. Huduma yao ya kuanzisha jumuiya za kwanza za Kikristo imezaa Kanisa letu Katoliki la ulimwengu mzima. Yaelekea watu hawa hawakutambua jinsi huduma yao ya uaminifu ingeugusa ulimwengu.

Tunapowaheshimu Mitume hawa wawili, tunakumbushwa pia kwamba kila mmoja wetu anaitwa kwenda kuitangaza Injili hadi miisho ya dunia. Kila mmoja wetu hufanya hivyo kwa namna inayolingana na wito na utume ambao Kristo ametukabidhi. Kila mmoja wetu anaitwa kuleta mabadiliko yenye kudumu milele katika maisha ya wale tunaowahudumia. Na ikiwa tutakuwa waaminifu kwa utume wetu, tunaweza kuwa na hakika kwamba matunda ya huduma yetu ya kitume yatagusa maisha ya wengine wasiohesabika hadi mwisho wa dunia.

Tafakari leo jinsi Yesu alivyowachagua watu hawa wawili na kuwaweka kuwa Mitume. Unapofanya hivyo, sikiliza sauti ya Mungu anapozungumza nawe pia. Usidharau umuhimu wa kuukubali utume ambao Yesu anakupa. Mwambie “Ndiyo” kwa kuwaiga Mitume hawa wawili, nawe ujue kwamba uamuzi wako wa kumtumikia Bwana wetu kwa namna hii hautakuwa na matokeo makubwa katika maisha yako tu, bali pia katika maisha ya wengine wengi kwa umilele wote.

Bwana wangu mwenye utukufu, uliwaita watu hawa wawili wa kawaida, Simoni na Yuda, kuwa Mitume Wako. Uliwajaza neema Yako, ukawafundisha kwa Neno Lako, na kuwatuma wahubiri hadi miisho ya dunia. Tafadhali unitume nami, Bwana mpendwa, kwa yeyote utakayemchagua. Unitumie kama chombo Chako na unisaidie kubaki daima mwaminifu na mwenye bidii, nikiwafikia wenye mahitaji, hasa wale wasio na imani na matumaini maishani mwao. Watakatifu Simoni na Yuda, mtuombee. Yesu, nakutumainia.

Mtakatifu wa Siku – Mtakatifu Simoni na Mtakatifu Yuda, Mitume

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Tafakari za Maandiko Matakatifu kwa Kipindi cha Mwaka

Watakatifu/Sikukuu Zote

Sala kwa ajili ya Uchaguzi na Taifa
Novena ya majuma tisa kuanzia 3 Septemba hadi 4 Novemba

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu