Kiswahili

Kujitumainia Kupita Kiasi

Jumatano, 30 Oktoba 2019

Jumatano ya Juma la Thelathini la Kipindi cha Mwaka

Masomo ya Leo

Watakatifu Wote wa Leo

Sikiliza kwa Kiingereza

“Ndipo atawaambia, ‘Sijui mnakotoka.  Ondokeni Kwangu, ninyi nyote mtendao maovu!’”  Luka 13:27

Yesu anaweka wazi kwamba kuna watu watakaomjia wakidhani kwamba hakika wataingia Mbinguni, lakini kujitumainia kwao kupita kiasi kutakabiliwa na maneno haya ya kutisha: “Sijui mnakotoka.  Ondokeni Kwangu.”

Kujitumainia kupita kiasi ni dhambi hatari.  Ni hatari kwa sababu mbili.  Kwanza, watu wanapojitumainia kupita kiasi, wanaishi huku wakikataa kuutambua ukweli.  Kuhusiana na Mungu, kujitumainia kupita kiasi kunamaanisha kwamba watu wanatenda kana kwamba wana uhusiano na Mungu ilhali hawana.  Wanaweza kusema mambo matakatifu, kutenda kana kwamba ni watakatifu na hata kuamini kwamba ni watakatifu, ilhali kwa kweli hawamjui Bwana wetu hata kidogo.  Hivyo, kujitumainia kupita kiasi ni kuishi huku mtu akikataa kuutambua ukweli.

Pili, kujitumainia kupita kiasi ni hatari kwa sababu mtu anayejitumainia hivyo hatatubu dhambi yake mwenyewe. Hii ni kwa sababu kukataa kwake kuutambua ukweli kunamfanya asiweze kukiri dhambi yake.  Bila kukiri dhambi yake, hawezi kisha kukiri kwamba anahitaji kubadilika.  Anaendelea kuzama katika mawazo yake potovu na dhambi yake.

Yesu anatoa fundisho hili si ili kuonyesha kwamba Yeye ni mkali kwa wale wanaojitumainia kupita kiasi; bali, analitoa kama tendo la huruma kubwa kwa wale waliokwama katika dhambi hii.  Ufunuo huu wa kushtua unahitajika ili kumzindua mtu ajinasue katika dhambi hii.  Katika hali hii, hofu ya siku moja kusikia maneno haya kutoka kwa Yesu ndiyo itakayowasaidia wale waliokwama katika kujitumainia kupita kiasi kujinasua na kuukabili ukweli.

Tafakari leo kuhusu namna yoyote ambayo husemi au kuukubali ukweli kuhusu wewe mwenyewe, iwe kwako mwenyewe au kwa wengine.  Acha mshtuko wa matokeo ya mwisho ya kujitumainia kokote kupita kiasi maishani mwako ukuzindue ujinasue katika dhambi hii, ili uweze kujinyenyekeza mbele za Mungu sasa, kabla hujachelewa mno.  Kumbuka jinsi Bwana wetu anavyokupenda kwa dhati, na uruhusu upendo huo ukusaidie kuyakabili maisha yako kwa unyofu na uadilifu.

Bwana, ninakupenda kwa dhati na ninaomba kwamba upendo wangu uwe daima mnyofu, wa kweli na kamili.  Nisaidie kuona namna zozote katika maisha yangu ambazo nashindwa kukupenda kwa moyo wangu wote.  Ninakukabidhi maisha yangu bila kujibakizia chochote, Bwana mpendwa.  Yesu, nakutumainia.

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

MPYA – Jisajili kwenye chaneli yetu ya YouTube!