Kiswahili

Tunu ya Mungu

Desemba 7, 2019
Jumamosi ya Wiki ya Kwanza ya Majilio
Masomo ya Leo

Mtakatifu Ambrosi, Askofu na Mwalimu wa Kanisa—Kumbukumbu

Sikiliza kwa Kiingereza

“Mmepokea bure; toeni bure.” Mathayo 10:8b

Ni nini ambacho tumepokea “bure?” Naam, tumepokea kila kitu chema bure. Ni kweli! Kila kilicho chema ni tunu kutoka kwa Mungu. Nayo ni tunu ya bure kutoka Kwake. Hakuna tunachoweza kufanya ili kustahili baraka Zake katika maisha yetu. Je, unaamini hivyo?

Nukuu hiyo ya Maandiko Matakatifu hapo juu ni sehemu ya mawaidha ya Yesu kwa Mitume Wake Kumi na Wawili anapowatuma kuhubiri, kuponya na kufukuza pepo kwa jina Lake. Anawakumbusha kwamba yote waliyopokea kutoka Kwake ni tunu ya bure na kwamba wao pia wanapaswa kuwapa wote Injili bila malipo.

Majilio ni wakati ambao tunapaswa kuelekeza mawazo yetu hasa kwenye maadhimisho yajayo ya Tunu ya Noeli. Noeli ni wakati wa kupeana na kupokea zawadi, lakini ni muhimu kuelewa tofauti kati ya “tunu” na “zawadi.” Zawadi ni kitu kinachotarajiwa. Kwa mfano, mwenzi wako wa ndoa au mtoto wako hutarajia zawadi katika siku yake ya kuzaliwa au wakati wa Noeli. Lakini tunu ni kitu chenye maana kubwa zaidi. Tunu ni kitu kinachotolewa kwa hiari, ambacho mtu hajakipata kwa juhudi zake wala hakustahili kupewa. Hutolewa kwa upendo bila masharti yoyote. Hiyo ndiyo maana hasa ya Umwilisho.

Majilio yanapaswa kuwa wakati wa kutafakari ukweli kwamba Mungu alikuja duniani ili kujitoa kwetu bure, bila sisi kustahili. Maisha Yake ni Tunu ya bure kabisa kwetu, nayo ndiyo Tunu kuu kuliko zote tulizowahi kupokea. Vilevile, Majilio yanapaswa kuwa wakati wa kutafakari pia wito wetu wa kuwapelekea wengine Tunu ya Kristo Yesu.

Tafakari leo juu ya kumpokea Yesu katika maisha yako na kuwapa wengine Tunu hiyo. Moyo wako ujazwe shukrani katika Majilio haya ili nawe uweze kuwapa wengine Tunu ya Yesu.

Bwana, nakushukuru kwa Tunu ya maisha Yako. Nakushukuru kwa kuja duniani ili uingie katika maisha yangu. Nakushukuru kwa furaha ya kukujua na kukupenda. Niiache furaha hii iyabadilishe maisha yangu kiasi cha kunifanya nitafute daima kukutoa Wewe kwa wengine. Yesu, nakutumainia.

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Nyenzo za Majilio

Mtakatifu wa Siku – Mtakatifu Ambrosi, Askofu na Mwalimu wa Kanisa—Kumbukumbu

Tazama kwenye YouTube