Kiswahili

Mtu Mmoja Anapaswa Kufa

Aprili 4, 2020
Jumamosi ya Juma la Tano la Kwaresima
Masomo ya Leo

Mtakatifu Isidori, Askofu na Mwalimu wa Kanisa—Kumbukumbu ya Hiari

Sikiliza kwa Kiingereza

Lakini mmoja wao, Kayafa, aliyekuwa kuhani mkuu mwaka ule, akawaambia, “Ninyi hamjui kitu, wala hamfikirii kwamba ni afadhali kwenu mtu mmoja afe badala ya watu, ili taifa lote lisiangamie.”  Yohane 11:49–50

Kama katika tafakari ya siku iliyotangulia, ni muhimu kwetu kuanza kuelekeza fikira zetu kwenye mateso na kifo cha Yesu.  Juma Takatifu linaanza Jumapili hii, kwa hiyo huu ndio wakati wa mwaka ambapo Mungu anataka tuutazame kwa makini Msalaba Wake.  Ni muhimu kuutazama kwa kila upande, kujaribu kuelewa yaliyokuwa yakitokea, yale ambayo Yesu alikuwa akipitia, yale ambayo wanafunzi walikuwa wakipitia, na hata yale ambayo Mafarisayo na makuhani wakuu walikuwa wakipitia.

Katika Injili ya leo iliyonukuliwa hapo juu, tunaona mawazo ya Kayafa, kuhani mkuu.  Maneno yake yanavuta fikira kwa kuwa yanahuzunisha na wakati huohuo ni ya kinabii.  Yeye, pamoja na makuhani wakuu wengine na Mafarisayo, walikuwa wanaanza kupanga na kula njama za kumwua Yesu.  Lakini kinachotupa mwanga ni kile kinachoonekana kuwa msukumo wa Kayafa na wale wengine.

Yesu alikuwa akizidi kupendwa na watu, nao waliogopa kwamba hali hiyo ingezua matatizo na Waroma.  Pia waliona wivu kwa sababu Yesu alikuwa amewavutia watu wengi sana.  Kwa hiyo Kayafa anatoa hoja iliyopotoka kwamba ni afadhali mtu mmoja afe kuliko watu wote.  Kwa maneno mengine, alionekana kufikiri kwamba, kwa sababu Yesu alikuwa akizidi kupendwa sana na watu, nao walikuwa wakimsikiliza Yesu zaidi kuliko makuhani wakuu na Mafarisayo, ilikuwa afadhali kuondoa “tatizo” hilo ili mambo yaweze kurudi kama yalivyokuwa zamani.

Hili linafunua ukweli kwamba Mafarisayo walijali zaidi nafsi zao na hadhi yao kuliko Ukweli.  Inashangaza kwamba mojawapo ya mambo waliyomkosoa Yesu ilikuwa kwamba alikuwa akifanya ishara na maajabu mengi mno.  Ajabu iliyoje!  Kama makuhani wakuu na Mafarisayo wangekuwa wanajali Ukweli, wangeuona pia utukufu na mamlaka ya kimungu ya Yesu, wakamwamini na kumfuata.  Lakini hawakuweza kujishusha kutoka katika kiburi chao na kukubali mwito wa kumfuata mtu mwingine badala ya kujifuata wenyewe.  Hawakuweza kuachia nafasi yao ya mamlaka.

Mara nyingi tunaona hali hii katika maisha yetu ya kila siku.  Tunataka sisi ndio tuwe kitovu cha uangalifu wa watu.  Na mara nyingi tunapomwona mtu mwingine akifanikiwa au akisifiwa, tunaweza kuona wivu.  Na wivu wetu unaweza mara nyingi kugeuka kuwa husuda.  Husuda maana yake ni kukasirishwa na kuhuzunishwa na mema ya mtu mwingine.  Tunaweza kuendelea kuyawaza kwa uchungu na kutamani kumwona akishindwa.

Lengo bora ni kuwa mmoja wa wafuasi hao waaminifu wa Yesu.  Ni muhimu hasa kutafakari hili katika juma linalokuja unapoona uadui dhidi ya Bwana wetu ukiongezeka.  Ungefanya nini kama ungekuwa huko?  Je, ungeendelea kusimama pamoja na Yesu licha ya mashambulizi ya wengine?  Kadiri uadui dhidi ya Yesu ulivyoongezeka, je, ungejitenga Naye au ungekaribia zaidi Kwake kwa upendo na kujitoa?

Tafakari leo kuhusu ukumbusho unaokuja wa mateso aliyopata Bwana wetu kutokana na kuonewa.  Acha akili yako ianze kutafakari miitikio mingi na mambo ambayo watu walipitia katika lile Juma Takatifu la kwanza.  Jiweke katika hali yao na ujaribu kuipitia pamoja na Yesu.  Lengo ni kujikuta pale chini ya Msalaba pamoja Naye siku ya Ijumaa Kuu, tukiwa na upendo na ujasiri, tukisimama pamoja Naye na kumpenda katika kila hatua.

Bwana, naomba nikufuate katika Juma Takatifu linalokuja.  Naomba niwe na upendo ninaouhitaji ili nikupende hata unapokataliwa na unapokuwa katika maumivu.  Nisaidie kuondoa husuda yote na ubinafsi wote, na kukuona Wewe hasa katika mateso ya wengine na katika wema wao.  Yesu, nakutumainia.

Siku 40 Chini ya Msalaba – Tafakari ya Thelathini na Nane – Mkuki wa Askari

Nyenzo za Kwaresima

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Watakatifu/Sikukuu Zote

Mtakatifu wa Siku – Mtakatifu Isidori

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu