Kiswahili

Uaminifu kwa Mungu Baada ya Kuanguka

Jumatano, 24 Juni 2020

Sherehe ya Kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Mbatizaji

Masomo ya Leo

Sikiliza kwa Kiingereza

Aliomba kibao cha kuandikia, akaandika, “Jina lake ni Yohane,” nao wote wakastaajabu. Mara kinywa chake kikafunguliwa, ulimi wake ukafunguka, naye akaanza kusema akimtukuza Mungu.  Luka 1:63-64

Zakaria anatupa sisi sote ushuhuda mzuri wa mtu aliyetenda dhambi kwa kukosa imani kwa Mungu, lakini baada ya kupata fedheha kutokana na dhambi yake, akawa mwaminifu kweli na hatimaye akaanza “kumtukuza Mungu.”

Tunaifahamu habari yake.  Mke wake alipata mimba ya Yohane Mbatizaji kwa muujiza katika uzee wake.  Malaika alipomfunulia Zakaria kwamba jambo hili lingetokea, hakuamini ahadi hiyo, bali alitia shaka.  Matokeo yake yalikuwa kwamba alipatwa na ububu hadi wakati Yohane alipozaliwa.  Wakati huo ndipo Zakaria alipotenda kwa uaminifu kwa ufunuo wa Mungu kwa kumpa mtoto wake jina “Yohane” kama malaika alivyokuwa ameagiza.  Tendo hili la uaminifu la Zakaria liliufungua ulimi wake, naye akaanza kumsifu Mungu.

Ushuhuda huu wa Zakaria unapaswa kuwatia moyo wote wanaotafuta kufuata mapenzi ya Mungu katika maisha yao lakini wameshindwa.  Mara nyingi Mungu husema nasi, tunamsikia, lakini tunashindwa kuamini anayosema.  Tunashindwa kuwa waaminifu kwa ahadi Zake.  Matokeo yake ni kwamba tunapata madhara ya dhambi hiyo.

Mwanzoni, madhara ya dhambi katika maisha yetu yanaweza kuonekana kama adhabu.  Kwa kweli, kwa namna nyingi ni adhabu.  Si adhabu kutoka kwa Mungu; bali ni adhabu inayotokana na dhambi.  Dhambi ina matokeo yenye kuharibu sana maisha yetu.  Lakini habari njema ni kwamba Mungu huruhusu matokeo hayo ya dhambi kama njia ya kutuvuta turudi katika uaminifu Kwake.  Na tukiyaru­husu yatunyenyekeze na kutubadilisha kama Zakaria alivyofanya, tutaweza kuacha maisha ya kutokuwa waaminifu kwa mapenzi ya Mungu na kuingia katika maisha ya uaminifu.  Na maisha ya uaminifu yatatuwezesha hatimaye kuimba sifa za Mungu wetu.

Tafakari leo namna ambavyo hujakuwa mwaminifu kwa Mungu katika maisha yako.  Lakini yatazame hayo kwa matumaini.  Uwe na matumaini kwamba Mungu atakupokea tena na kuyabadilisha maisha yako ukimrudia.  Mungu anangoja, na huruma Yake ni tele.  Iruhusu huruma Yake ikujalie moyo unaousifu wema wa Mungu.

Bwana, nisaidie nisiangalie dhambi zangu zilizopita kwa kukata tamaa, bali zaidi nizione kuwa sababu za kukurudia Wewe kwa uaminifu mkubwa zaidi.  Haidhuru nimeanguka mara ngapi, nisaidie niinuke tena na kuimba sifa Zako kwa uaminifu.  Yesu, nakutumainia.

Video sasa inapatikana pia kwa Kireno!

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Watakatifu/Sikukuu za Leo

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu

Soma Zaidi – Kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Mbatizaji

Picha: Kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji, kazi ya Artemisia Lomi Gentileschi