Kiswahili

Kusihi Kupewa Huruma

Septemba 17, 2020
Alhamisi ya Wiki ya Ishirini na Nne ya Kipindi cha Mwaka
Masomo ya Leo

Mtakatifu Roberto Bellarmino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa—Kumbukumbu ya Hiari

Sikiliza kwa Kiingereza

Mfarisayo mmoja alimwalika Yesu ale pamoja naye, naye akaingia katika nyumba ya Mfarisayo huyo, akajiegemeza mezani. Basi, kulikuwa na mwanamke mwenye dhambi mjini humo, ambaye alipata habari kwamba Yesu alikuwa mezani katika nyumba ya Mfarisayo. Akaleta chupa ya alabasta yenye marhamu, akasimama nyuma Yake karibu na miguu Yake akilia, akaanza kuilowesha miguu Yake kwa machozi yake. Kisha akaipangusa kwa nywele zake, akaibusu na kuipaka marhamu.  Luka 7:36-38

Kwa sehemu, Injili hii inamhusu yule Mfarisayo.  Tukiendelea kusoma kifungu hiki, tunamwona Mfarisayo akiwahukumu na kuwalaumu sana mwanamke huyu na Yesu.  Yesu alimkemea, kama alivyowakemea Mafarisayo mara nyingi hapo awali.  Lakini kifungu hiki kina mengi zaidi ya kuwakemea Mafarisayo.  Kiini chake ni simulizi la upendo.

Upendo huo ni ule uliomo moyoni mwa mwanamke huyu mwenye dhambi.  Ni upendo unaodhihirishwa kwa majuto kwa ajili ya dhambi na unyenyekevu mkubwa.  Dhambi yake ilikuwa kubwa na, kwa sababu hiyo, unyenyekevu na upendo wake pia vilikuwa vikubwa.  Hebu tuangalie kwanza unyenyekevu huo.  Unaonekana katika matendo yake alipomjia Yesu.

Kwanza, “alisimama nyuma Yake…”
Pili, alianguka chini “miguuni Pake…”
Tatu, alikuwa “akilia…”
Nne, aliiosha miguu Yake “kwa machozi yake…”
Tano, aliikausha miguu Yake “kwa nywele zake…”
Sita, “aliibusu” miguu Yake.
Saba, “aliipaka” miguu Yake manukato yake ya gharama kubwa.

Tulia kwa muda na ujaribu kuwazia tukio hili.  Jaribu kumwona mwanamke huyu mwenye dhambi akijinyenyekeza kwa upendo mbele ya Yesu.  Ikiwa haya yote aliyoyafanya si tendo la majuto makubwa, toba na unyenyekevu, basi ni vigumu kujua ni nini kingine.  Ni tendo lisilopangwa mapema, lisilofanywa kwa mahesabu, wala kwa nia ya kumshawishi mwingine kwa hila.  Badala yake, ni tendo la unyenyekevu mkubwa, la dhati na la kujitoa kikamilifu.  Kwa tendo hili, anamlilia Yesu amhurumie na kumsikitikia, bila hata kulazimika kusema neno.

Tafakari leo kuhusu dhambi yako mwenyewe.  Usipoitambua dhambi yako, huwezi kuonyesha majuto ya namna hii yenye unyenyekevu.  Je, unaitambua dhambi yako?  Kisha, fikiria kupiga magoti chini, kuinamisha kichwa chako hadi ardhini mbele ya Yesu na kumsihi kwa dhati akusikitie na kukuhurumia.  Jaribu kufanya hivyo kwa vitendo.  Lifanye liwe tendo la kweli na la kujitoa kikamilifu.  Matokeo yake ni kwamba Yesu atakutendea kwa huruma ileile aliyomtendea mwanamke huyu mwenye dhambi.

Bwana, nakuomba unihurumie.  Mimi ni mwenye dhambi na ninastahili adhabu ya milele.  Ninaikiri dhambi yangu.  Nakuomba, kwa huruma Yako, unisamehe dhambi yangu na kunimiminia huruma Yako isiyo na kikomo.  Yesu, nakutumainia.

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Watakatifu/Sikukuu Zote

Mtakatifu wa Siku – Mtakatifu Roberto Bellarmino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu

Picha kuu hapo juu: Chakula cha Jioni katika Nyumba ya Mfarisayo, iliyochorwa na Maria Felice Tibaldi