Kiswahili

Kutambua Mapenzi ya Mungu

Januari 16, 2021
Jumamosi ya Juma la Kwanza la Kipindi cha Mwaka
Masomo ya Leo

Sikiliza kwa Kiingereza

Alipokuwa akipita, alimwona Lawi, mwana wa Alfayo, ameketi katika kituo cha ushuru. Yesu akamwambia, “Nifuate.” Naye akainuka, akamfuata Yesu. Marko 2:14

Unajuaje mapenzi ya Mungu kwa maisha yako? Katika kitabu chake maarufu cha kiroho, Mazoezi ya Kiroho, Mtakatifu Ignasi wa Loyola alieleza njia tatu ambazo kwazo tunapata kuyajua mapenzi ya Mungu. (Tazama mycatholic.life/ignatius kwa maelezo zaidi.) Njia ya kwanza ndiyo iliyo wazi zaidi na yenye uhakika zaidi. Huu ni wakati ambapo mtu anapata “ufahamu ulio wazi usioacha nafasi ya shaka” kutokana na neema maalumu ya Mungu. Akielezea hali hii, Mtakatifu Ignasi anataja kifungu kilichonukuliwa hapo juu kama mfano wa hali hii.

Machache yanasemwa katika Injili ya Marko kuhusu wito huu wa Lawi, ambao pia umeandikwa katika Injili ya Mathayo (Mathayo 9:9). Lawi, ambaye pia anajulikana kama Mathayo, alikuwa akiendelea na kazi yake ya kukusanya ushuru katika kituo chake cha ushuru. Inaonekana kwamba Yesu alimwambia Lawi maneno haya mawili tu yaliyo rahisi: “Nifuate.” Kutokana na maneno haya mawili, Lawi anaacha maisha yake ya awali na kuwa mfuasi wa Yesu. Kwa nini Lawi afanye jambo kama hilo? Ni nini kilichomshawishi kumfuata Yesu? Ni wazi kwamba kulikuwa na jambo kubwa zaidi ya mwaliko wa maneno mawili tu kutoka kwa Yesu lililomshawishi kuitikia.

Kilichomshawishi Lawi kilikuwa neema maalumu ya Mungu iliyoleta ndani ya roho yake “ufahamu ulio wazi usioacha nafasi ya shaka.” Kwa namna fulani, Lawi alijua tu kwamba Mungu alikuwa akimwita aache maisha yake ya awali na kuyakumbatia maisha haya mapya. Hakukuwa na mazungumzo marefu, wala kupima faida na hasara, wala kufikiria jambo hilo kwa muda mrefu. Lawi alijua tu, naye akaitikia.

Ingawa ni nadra kupata ufahamu wa namna hii ulio wazi katika maisha, ni muhimu kutambua kwamba wakati mwingine Mungu hutenda kwa namna hii. Wakati mwingine Mungu husema kwa uwazi kiasi kwamba tunakuwa na hakika kabisa na tunajua kwamba lazima tutende. Hii ni zawadi kubwa inapotokea! Na ingawa si kila mara Mungu husema nasi kwa kutupa ufahamu wa kina ulio wazi mara moja namna hii, ni muhimu kukiri kwamba nyakati nyingine Mungu husema nasi kwa namna hii.

Tafakari leo kuhusu wito huu wa Lawi. Fikiria kwa kina uhakika huu wa ndani aliopewa wakati ule. Jaribu kuwaza alichokipitia na yale ambayo wengine huenda walifikiria kuhusu uamuzi wake wa kumfuata Yesu. Uwe tayari kuipokea neema hii pia; na ikiwa wakati wowote utahisi kana kwamba Mungu anasema nawe kwa uwazi wa namna hii, uwe tayari na mwenye nia ya kuitikia bila kusita.

Bwana wangu mpendwa, nakushukuru kwa kutuita sote tukufuate bila kusita. Nakushukuru kwa furaha ya kuwa mwanafunzi Wako. Nipe neema ya kuyajua daima mapenzi Yako kwa maisha yangu na unisaidie kukuitikia kwa kujikabidhi kabisa Kwako na kwa matumaini. Yesu, nakutumainia.

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Watakatifu/Sikukuu za Leo

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu

Picha iliyoangaziwa hapo juu: Kuitwa kwa Mtakatifu Mathayo, na Giovanni Paolo Panini