Februari 12, 2021
Ijumaa ya Juma la Tano la Wakati wa Kawaida
Masomo ya Leo

Walishangaa kupita kiasi wakasema, “Amefanya mambo yote vizuri. Anawafanya viziwi wasikie na mabubu waseme.” Marko 7:37
Maneno haya yanahitimisha simulizi la Yesu kumponya mtu aliyekuwa kiziwi na pia mwenye shida ya kusema. Mtu huyo aliletwa kwa Yesu, naye Yesu akamchukua faraghani, akapaza sauti akisema, “Efatha!” (yaani, “Funguka!”), na mtu huyo akaponywa. Ingawa hii ilikuwa zawadi ya ajabu kwa mtu huyo na tendo la huruma kubwa kwake, pia inafunua kwamba Mungu anataka kututumia kuwavuta wengine Kwake.
Kwa uwezo wetu wa kiasili, sote hatuwezi kuisikia sauti ya Mungu anaposema. Tunahitaji zawadi ya neema kwa ajili ya hili. Kwa hiyo, kwa uwezo wetu wa kiasili, hatuwezi pia kusema kweli nyingi ambazo Mungu anataka tuziseme. Simulizi hili linatufundisha kwamba Mungu anatamani pia kuyaponya masikio yetu ili tuisikie sauti Yake ya upole na kuzifungua ndimi zetu ili tuweze kuwa wasemaji Wake.
Lakini simulizi hili halihusu tu Mungu kusema na kila mmoja wetu; pia linafunua wajibu wetu wa kuwaleta kwa Kristo wengine wasiomjua. Rafiki za mtu huyo walimleta kwa Yesu. Naye Yesu akamchukua mtu huyo faraghani. Hili linatupa mwanga kuhusu jinsi tunavyowasaidia wengine kuifahamu sauti ya Bwana wetu. Mara nyingi tunapotaka kumshirikisha mwingine Injili, huwa tunaelekea kuzungumza naye na kujaribu kumshawishi kwa hoja aelekeze maisha yake kwa Kristo. Ingawa nyakati fulani hili linaweza kuzaa matunda mema, lengo halisi tunalopaswa kuwa nalo ni kumsaidia aende kukaa faraghani na Bwana wetu kwa muda, ili Yesu aweze kumponya.
Ikiwa masikio yako yamefunguliwa kweli na Bwana wetu, basi ulimi wako pia utafunguliwa. Na ni ikiwa tu ulimi wako umefunguliwa ndipo Mungu ataweza kuwavuta wengine Kwake kupitia wewe. La sivyo, tendo lako la kueneza Injili litategemea juhudi zako peke yako. Kwa hiyo, ikiwa kuna watu katika maisha yako ambao hawaonekani kuisikiliza sauti ya Mungu na kufuata mapenzi Yake matakatifu, basi kwanza kabisa jitoe wewe mwenyewe kumsikiliza Bwana wetu. Acha masikio yako yamsikie. Na utakapomsikia, itakuwa ni sauti Yake itakayosema kupitia wewe kwa namna anayotamani kuwafikia wengine.
Tafakari leo tukio hili la Injili. Watafakari hasa rafiki za mtu huyo wanapohamasishwa kumleta kwa Yesu. Mwombe Bwana wetu akutumie kwa namna hiyo hiyo. Katika sala, watafakari wale walio katika maisha yako ambao Mungu anataka kuwaita Kwake kupitia upatanishi wako, nawe ujiweke katika utumishi wa Bwana wetu ili sauti Yake iweze kusema kupitia wewe kwa namna anayoichagua.
Yesu wangu mwema, tafadhali fungua masikio yangu nisikie yote unayotaka kuniambia, na tafadhali ufungue ulimi wangu ili niwe msemaji wa neno Lako takatifu kwa wengine. Ninajitoa Kwako kwa ajili ya utukufu Wako, nami ninaomba unitumie kulingana na mapenzi Yako matakatifu. Yesu, nakutumainia kabisa.
Sasa unaweza kutufuatilia kwenye Gab na MeWe
Tafakari juu ya Huruma ya Mungu
Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu
Picha iliyoangaziwa hapo juu: Uponyaji wa kiziwi na bubu




