Kiswahili

Faraghani na Yesu

Julai 18, 2021
Jumapili ya Kumi na Sita ya Mwaka (Mwaka B)
Masomo ya Leo

Video

Sikiliza kwa Kiingereza

“Njooni faraghani mahali pasipo na watu, mpumzike kidogo.”  Marko 6:31a

Huu ni mwaliko ambao huenda tunahitaji kuusikia zaidi sana kuliko tunavyotambua.  Nao ni mwaliko ambao wengi wanaona vigumu kuukubali kutoka kwa Yesu.  Lakini uupokee kama mwaliko wa moja kwa moja unaotolewa kwako na Bwana wetu.  Msikie akikuambia hivi: “Wewe, mwanangu, tafadhali njoo faraghani mahali pasipo na watu, upumzike kidogo.”

Kuna jambo linaloponya na kusaidia sana linalotokana na ukimya na nyakati za kuwa faraghani.  Ukimya na kuwa faraghani hutuwezesha kuelekeza tena fikira zetu kwenye mambo muhimu.  Mara nyingi maishani tunalemewa na shughuli nyingi.  Mara nyingi “shughuli nyingi” ni njia anayotumia yule mwovu kutuchosha na kutupotosha.  Zinatuzuia kuisikia sauti ya Mungu iliyo ya upole, iliyo wazi na inayotuburudisha.  Basi, Mungu anakualikaje uende faraghani ukapumzike?

Kiini cha mwaliko huu ni shauku iliyo moyoni mwa Yesu kwamba tupumzike kutoka katika mizigo inayotulemea bila sababu.  Ni kweli kwamba kuna mambo mengi mema ambayo Mungu anatuita tuyafanye na ambayo yanaweza kutuchosha sana.  Lakini huu “uchovu mtakatifu” si jambo baya.  Kwa kweli, “kuchoka sana” kwa kutimiza mapenzi ya Mungu huimarisha imani yetu na kutujaza furaha.  Na furaha hiyo hupunguza uzito wa mzigo wetu.

Sababu kuu ya kuhitaji “kwenda faraghani” na “kupumzika” ni kwamba kuna mambo mengi maishani ambayo si sehemu ya mapenzi ya Mungu.  Hii ni mizigo tunayojitwika bila sababu.  Zaidi ya kitu kingine chochote, tunahitaji kupumzika kutoka katika mizigo hii.

Kwenda faraghani kuwa na Yesu peke yako ni njia ya kuelekeza tena fikira zako kwenye mambo muhimu na kuondoa mambo yanayosongamanisha maisha.  Ni njia ya kujinasua kutoka katika misukumo na mazoea yetu yanayotuvuta mbali na mapenzi ya Mungu yanayoleta furaha.  Basi, fikiria mwaliko huu.  Fikiria jinsi ya kuuitikia kwa vitendo.  Je, unaweza kupata angalau dakika kumi leo ili uende mahali penye ukimya upumzike mikononi mwa Yesu?

Tafakari leo jinsi ulivyo tayari na ulivyo na hiari ya kukubali mwaliko wa Yesu wa kuja kupumzika pamoja Naye na ndani Yake.  Jitolee kufanya hivyo.  Amua leo kutenga muda wa kuwa faraghani.  Katika muda huo wa kuwa faraghani, tafuta sauti ya Mungu tulivu, ya upole na isiyo na kelele.  Acha utulivu na amani ya uwepo wa Mungu vikusaidie kuona mambo kwa uwazi na kuelekeza fikira zako kwenye mambo muhimu katika maisha yako yenye shughuli nyingi.

Bwana, nisaidie nikusikie ukiniita nipate muda wa mapumziko na amani.  Nisaidie nikutafute na kuukubali mwaliko Wako wa upole.  Yesu, nakutumainia.

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Tafakari za Maandiko Matakatifu kwa Kipindi cha Mwaka

Watakatifu/Sikukuu Zote

Mtakatifu wa Siku – Mtakatifu Kamilo de Lellis, Padre—Kumbukumbu ya Hiari nchini Marekani (Huadhimishwa Julai 14 nje ya Marekani)
Haiadhimishwi kama kumbukumbu ya kiliturujia mwaka huu kwa sababu inaangukia Jumapili

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu

Picha iliyoangaziwa hapo juu: Yesu Akiwafundisha Watu Kando ya Bahari, iliyochorwa na James Tissot, kupitia Wikimedia Commons