22 Oktoba 2021
Ijumaa ya Juma la Ishirini na Tisa la Mwaka
Masomo ya Leo
Mtakatifu Yohane Paulo II, Papa—Kumbukumbu ya Hiari

Sikiliza kwa Kiingereza
“Kwa nini hamjiamulii wenyewe yaliyo sawa? Ukienda pamoja na hasimu wako mbele ya hakimu, jitahidi kusuluhisha jambo hilo mkiwa njiani; la sivyo, hasimu wako atakukabidhi kwa mwamuzi, naye mwamuzi atakukabidhi kwa askari, na askari atakutupa gerezani. Nakuambia, hutatoka humo mpaka uwe umelipa senti ya mwisho.” Luka 12:57–59
Mababa wa Kanisa wanatoa tafsiri nyingi tofauti za kifungu hiki. Miongoni mwao, Mtakatifu Beda anasema kwamba “hasimu” wetu anaweza kuonekana kuwa ni Neno la Mungu, kwa maana kwamba Neno la Mungu linapigana dhidi ya udhaifu na dhambi zetu. Tunapolisikiliza Neno la Mungu, Bwana wetu atatufanya tutambue makosa yetu ili tuweze kupatanisha maisha yetu na Ukweli wa Neno la Mungu Mwenyewe.
Unapolitafakari Neno takatifu la Mungu kwa ujumla wake, ni jambo gani linalokufanya utambue makosa yako zaidi? Wakati mwingine tunajaribu kupuuza misukumo hiyo ya dhamiri zetu. Tunatafuta visingizio vya matendo yetu na kupuuza yale ambayo Mungu anatuambia. Je, kuna mafundisho yoyote ya Yesu unayoyakumbuka ambayo yamekuchoma moyoni kweli? Ikiwa yapo, hii ni neema, na ni fursa ya kutekeleza fundisho la Bwana wetu katika kifungu kilicho hapo juu. Mungu hatufanyi tutambue makosa mioyoni mwetu ili atuhukumu adhabu. Bali, akiwa hasimu wa dhambi zetu, anatufanya tutambue makosa yetu ili tuweze ‘kujitahidi kusuluhisha jambo hilo tukiwa njiani.’ Dhamiri ni zawadi ya ajabu kutoka kwa Bwana wetu na inaweza kufananishwa na kifungu hicho hapo juu. Ni aina ya mahakama ambamo Bwana wetu hatamani kulazimika kutupatia adhabu. Badala yake, anatamani tulitafakari kwa makini Neno Lake takatifu, tusikilize yale anayosema, na tumalize suala la dhambi zetu kwa kutubu mara moja.
Miongoni mwa mafundisho mengi ya Bwana wetu, mara nyingi fundisho linalotuvuta fikira, hata kwa namna ya kutushtua, ndilo tunalohitaji kulizingatia zaidi. Mara nyingi Mungu hutufikishia mafundisho Yake yanayohitaji kushughulikiwa haraka zaidi kwa kutufanya tuhisi hatia isiyoweza kukanushwa. Tukiisikiliza misukumo hii ya dhamiri, basi hatutakuwa na haja yoyote ya kusimama mbele ya Hakimu. Lakini tusipoisikiliza, tukiifukia misukumo hii, tukiidharau na kuipuuza, basi Bwana wetu ataona ni lazima aendelee kutusukuma. Tutaanza kuipata hukumu Yake, na tutaona athari za kutokuwa katika upendeleo Wake. Na mwishowe, tukishindwa kutubu dhambi nzito zaidi katika maisha yetu, basi tutawajibishwa hata kwa dhambi zilizo ndogo kabisa. Tutatakiwa ‘kulipa senti ya mwisho.’
Tafakari leo wazo hili: Neno la Mungu, yaani yote ambayo Bwana wetu ametufundisha, ni hasimu wa dhambi iliyo katika nafsi yako. Hasimu huyu mwema na mtakatifu anakutakia mema tu. Jitoe kulisoma daima Neno takatifu la Mungu ili uwe tayari sikuzote kusikia yote ambayo Mungu anataka kukuambia, na ili uweze kupatana na Bwana wetu kabla hajalazimika kutoa hukumu Zake.
Hakimu wangu mwenye huruma kuu, unatamani nisikilize Neno Lako takatifu, lililofunuliwa kupitia Maandiko Matakatifu, ili nipokee kwa huruma Yako kuu utambuzi wa dhambi yangu. Ninaomba niwe tayari kusikia sikuzote yote unayotamani kuniambia ili niweze kuitikia kwa moyo wa ukarimu na matumaini, nikipatana daima na Wewe na wengine katika safari yangu ya maisha. Iamshe dhamiri yangu kwa Neno Lako takatifu, Bwana mpendwa. Yesu, nakutumainia.
Novena kwa Mtakatifu Yuda
Kwa Hali na Mashauri ya Kukatisha Tamaa
Husaliwa wakati wowote wa mwaka, hasa 19–27 Oktoba
Tafakari juu ya Huruma ya Mungu
Tafakari za Maandiko Matakatifu kwa Kipindi cha Mwaka
Mtakatifu wa Siku – Mtakatifu Yohane Paulo II, Papa
Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu
Picha iliyoangaziwa hapo juu: Mfano wa Hakimu Asiye wa Haki, kazi ya Ndugu Belousov



