Kiswahili

Kuulainisha Moyo Wako

23 Aprili 2022
Jumamosi katika Oktava ya Pasaka
Masomo ya Leo

Video

Sikiliza kwa Kiingereza

Lakini baadaye, wale Kumi na Mmoja walipokuwa mezani, aliwatokea na kuwakemea kwa kutokuamini kwao na ugumu wa mioyo yao, kwa sababu hawakuwa wamewaamini wale waliomwona baada ya Yeye kufufuliwa.  Marko 16:14

Kwa nini Mitume hawakuamini kwamba Yesu alikuwa amefufuka kutoka kwa wafu?  Walikuwa wameona kwa macho yao wenyewe miujiza mingi sana ya ajabu aliyotenda Yesu.  Waliishi naye siku baada ya siku kwa miaka mitatu.  Walimsikia akihubiri na kufundisha kwa mamlaka na neema kamilifu.  Na sasa, baada ya Yeye kufufuka kutoka kwa wafu, mioyo yao ilikuwa migumu na hawakuamini mara moja.  Ilibidi Yesu awatokee na kuwapa uthibitisho huo wauone kwa macho yao wenyewe.

Hangaiko hili walilopitia Mitume ni la kawaida sana.  Ni hangaiko linalotokana na ugumu wa moyo.  Walitaka kuamini, lakini hawakuweza kujiruhusu kuupokea Ufufuko kwa uhuru na kwa imani ya kweli mpaka walipopata uthibitisho fulani.  Hawakutambua kwamba uthibitisho wote waliohitaji ulikuwa tayari ndani yao.

Mara nyingi sana Yesu anatualika tuwe na imani na tumwamini, na tukubali mambo mengi kwa msingi wa imani.  Zawadi ya imani ni kama mwali mdogo ndani ya mioyo yetu ambao kwa uzembe tunauacha wazi upeperushwe na upepo.  Uzembe huu unaacha mwali wa imani uzimike kabla haujakua.

Lengo la safari yetu ya Kikristo ni kuuruhusu mwali huo wa imani uwe moto unaowaka kwa nguvu kama Mungu anavyotaka.  Na hilo linawezekana!  Inawezekana kabisa kuuruhusu mwali huo uwe moto unaoteketeza kila kitu kiasi kwamba hakuna chochote kinachoweza kuuzima.  Je, uko tayari kufanya unachopaswa kufanya ili mwali huo uangaze kwa nguvu?  Nasi tunafanyaje hivyo?

Njia ya kufikia moto huu wa imani unaowaka kwa nguvu ndani yetu inahusiana na jinsi tunavyoitunza cheche ile ambayo tayari ipo.  Tunapaswa kuutunza na kuukuza mwali huo mdogo.  Tunapaswa kuishughulikia kwa uangalifu mkubwa imani yetu inapokuwa bado changa.  Ni lazima tuilinde na tuilishe ili ikue.  Kwa sehemu, tunafanya hivyo kwa kuepuka uzembe katika maisha yetu ya sala.

Sala ndiyo ufunguo wa kumruhusu Mungu akue ndani yetu.  Yeye yupo humo, akizungumza nasi na kutuita tuamini.  Kila tunapokuwa na shaka, au kuifanya mioyo yetu kuwa migumu, tunauacha mwali huo mdogo wazi katika hali za hewa zinazoweza kuuzima.  Lakini kila tunapouelekezea mwali huo uangalifu wetu wote, tunauwezesha ukue na uwake imara.  Kusali, kusikiliza, kutafuta, kupenda na kuamini ndizo njia za kuifikia imani ambayo Mungu anataka kutujalia.  Na kama Mitume wangeiruhusu tu zawadi hiyo ya imani, iliyopandwa ndani kabisa mwao, ikue kwa kuilainisha mioyo yao, wangeamini haraka na kwa urahisi kwamba Yesu alikuwa hai bila kuhitaji kumwona kwa macho yao wenyewe.

Tafakari leo juu ya ukweli kwamba hatumwoni Kristo Mfufuka kwa macho ya mwili, lakini tunao uwezo uleule waliokuwa nao Mitume wa kumjua na kumpenda.  Unafanya nini kila siku ili upendo huu na ujuzi huu wa Kristo vikue?  Unafanya nini katika maisha yako ya imani ili mwali huu uwe moto unaowaka kwa nguvu na kuteketeza kila kitu?  Jitoe upya leo kwa sala, nawe utaona imani yako kwa Kristo ikikua na kung’aa!

Bwana, ninakupenda na ninakuamini.  Nisaidie kuuchochea mwali wa imani iliyopandwa moyoni mwangu uwe moto mkali unaoteketeza kila kitu.  Nisaidie kukujua na kukupenda ili kukujua na kukupenda huko kunibadilishe.  Itakase nafsi yangu kwa moto huu na uniweke huru na kila ugumu wa moyo.  Yesu, nakutumainia.

Siku ya Tisa: Novena ya kujiandaa kwa Jumapili ya Huruma ya Mungu

Zaidi kuhusu Pasaka

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Watakatifu/Sikukuu za Leo

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu

Picha zilizoangaziwa hapo juu:  Kutokea Wakati Mitume Wako Mezani na Duccio di Buoninsegna, kupitia Wikimedia Commons


  Subscribe to our YouTube channel  
  to be notified about new content.