Kiswahili

Kuvua Roho Pamoja na Yesu

Aprili 22, 2022
Ijumaa katika Oktava ya Pasaka
Masomo ya Leo

Video

Sikiliza kwa Kiingereza

“Tupeni wavu upande wa kulia wa mashua, nanyi mtapata kitu.” Basi wakautupa, nao hawakuweza kuuvuta kwa sababu ya wingi wa samaki.  Yohane 21:6

Kila mvuvi angependa kupata uzoefu ambao Yesu aliwajalia Mitume katika kifungu cha hapo juu.  Mitume walikuwa wamevua samaki usiku kucha bila kupata kitu.  Kisha, asubuhi, Yesu alionekana ufuoni, lakini hawakutambua kuwa ni Yeye.  Ndipo akawapa agizo rahisi la kutupa wavu wao upande wa kulia wa mashua.  Nao wakapata samaki wengi sana kiasi kwamba hawakuweza kuwavuta ndani ya mashua.  Ulikuwa uvuvi wa kufurahisha namna gani!

Uvuvi huu wa samaki ulikuwa zaidi sana ya fadhila tu kutoka kwa Yesu ili kuwasaidia katika kazi yao.  Ulikuwa na maana kubwa ya kiishara.  Maana kuu ya ishara hiyo ni kwamba Yesu alikuwa akiwapa Mitume wito mpya.  Wasingekuwa tena wakivua samaki tu, bali sasa walipaswa kuvua roho.  Na jambo muhimu ni kwamba kama wangejaribu kufanya hivyo kwa juhudi zao wenyewe, wangeambulia patupu.  Lakini kama wangefanya hivyo kwa agizo la Bwana, kwa namna anayotaka na kwa wakati Wake, basi juhudi zao zingezaa matunda mema tele.  Zaidi ya walivyoweza kuwazia!

Muujiza huu wa Yesu unaanza kuwafunulia Mitume (na sisi pia) agizo la kuihubiria dunia Injili.  Ufunuo huu unatokea baada ya Ufufuko Wake, Yesu anapowapa Mitume maagizo Yake ya mwisho ya kutekeleza utume Wake wa wokovu.  Katika muujiza huu tunapaswa kuona wito wetu wenyewe wa kueneza Habari Njema.  Na katika muujiza huu ni lazima tuone agizo la kueneza Habari Njema kwa agizo la Yesu pekee, kwa namna anayotaka na kwa wakati Wake.

Wakati mwingine Wakristo huwa na mawazo mengi “mazuri” ya kueneza Injili.  Lakini jambo la msingi ni kujinyenyekeza mbele za Mungu na kutambua kwamba hatuwezi kueneza Habari Njema ya Injili isipokuwa Bwana anatuongoza na kutuelekeza.  Hili linatuambia kwamba tunapaswa kumngojea na kumruhusu aseme.  Ni lazima tuisikilize sauti Yake na kuitikia tu anapotuongoza.  Uinjilishaji ni kuitikia wito wa Yesu badala ya kuwa jambo tunalofanya kwa juhudi zetu wenyewe.  Huu ndio ujumbe mkuu wa tukio hili la kimiujiza.

Tunapoendelea na sherehe yetu ya Siku ya Pasaka, huu ni wakati mzuri kwa kila mmoja wetu kutafakari wajibu wake mwenyewe wa kuinjilisha.  Sote tuna wito wa kushiriki katika kazi hii ya Yesu.  Itakuwa na sura tofauti kwa kila mmoja wetu kulingana na wito na utume wetu.  Lakini swali halisi ni hili: “Je, ninaitikia wito wa Yesu wa kuinjilisha kwa namna anavyonielekeza?”  Hili ni swali muhimu.  Tunapaswa kujua kwamba utume maalumu ambao Yesu anatupa haujakabidhiwa mtu mwingine yeyote.  Naye kwa kweli anataka kututumia.

Tafakari leo juu ya agizo hili ambalo Bwana wetu aliwapa Mitume, na umsikie akikupa agizo hilohilo, akikuita “kuvua roho” kulingana na mapenzi Yake matakatifu.  Mruhusu Bwana aseme nawe wiki hii, nawe uwe tayari kupokea mwongozo Wake.  Mungu anataka kukutumia, kwa hiyo hakikisha unamruhusu!

Bwana wangu unayetoa amri, ninatamani kweli unitumie.  Ninatamani kweli kueneza Injili kulingana na mapenzi Yako.  Nisaidie kuitikia wito kwa ujasiri, na nisaidie kusikiliza kwa unyofu mwongozo unaonipa.  Unitumie, Bwana mpendwa, kuziokoa roho nyingi kwa ajili ya Ufalme Wako.  Yesu, nakutumainia.

Siku ya Nane: Novena ya kujiandaa kwa Jumapili ya Huruma ya Mungu

Zaidi kuhusu Pasaka

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Watakatifu/Sikukuu za Leo

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu

Picha kuu hapo juu: Uvuvi wa Kimuujiza wa Samaki iliyochorwa na Raphael, kupitia Wikimedia Commons


Kinapatikana kama kitabu cha kielektroniki na kitabu chenye jalada laini:

Amazon –  Barnes and Noble – Google Play – iTunes

Tafakari za Kila Siku kuhusu Huruma ya Mungu:
Siku 365 pamoja na Mtakatifu Faustina


  Subscribe to our YouTube channel  
  to be notified about new content.