Mei 13, 2022
Ijumaa ya Juma la Nne la Pasaka
Masomo ya Leo
Mama Yetu wa Fatima—Kumbukumbu ya Hiari

Sikiliza kwa Kiingereza
“Katika nyumba ya Baba yangu mna makao mengi. Kama sivyo, je, ningaliwaambia kwamba ninakwenda kuwaandalia mahali? Nami nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena na kuwachukua kwangu, ili nilipo mimi, nanyi mwepo.” Yohane 14:2–3
Mara kwa mara ni muhimu tuelekeze mawazo yetu kwenye uhalisi wenye utukufu wa Mbinguni! Mbinguni ni halisi na, Mungu akipenda, siku moja sisi sote tutaungana huko na Mungu wetu aliye Utatu. Kama tungeelewa vizuri Mbinguni, tungepatamani kwa upendo wa kina na wenye kuwaka, na tungepatazamia kwa hamu kubwa, huku tukijawa na amani na furaha kila tunapopafikiria.
Hata hivyo, kwa bahati mbaya, kwa baadhi ya watu wazo la kuondoka duniani na kukutana na Muumba wetu linatisha. Huenda ni hofu ya mambo tusiyoyajua, utambuzi kwamba tutawaacha wapendwa wetu, au pengine hata hofu kwamba Mbinguni hakutakuwa mahali petu pa mwisho pa pumziko.
Sisi Wakristo tunapaswa kujitahidi kukuza upendo mkubwa kwa Mbinguni kwa kupata uelewa sahihi, si wa Mbinguni penyewe tu, bali pia wa kusudi la maisha yetu duniani. Mbinguni hutusaidia kupanga maisha yetu ipasavyo na kudumu katika njia inayoelekea kwenye heri hii ya milele.
Katika kifungu kilicho hapo juu, tunapewa taswira ya Mbinguni yenye kufariji sana. Ni taswira ya “nyumba ya Baba.” Taswira hii inafaa kuitafakari kwa sababu inafunua kwamba Mbinguni ni nyumbani kwetu. Nyumbani ni mahali salama. Ni mahali ambapo tunaweza kuwa jinsi tulivyo, kupumzika, kuwa pamoja na wapendwa wetu, na kuhisi kwamba ndipo mahali petu. Sisi ni wana na binti za Mungu, naye ameamua kwamba mahali petu ni huko pamoja Naye.
Kutafakari taswira hii ya Mbinguni kunapaswa pia kuwafariji wale waliofiwa na mpendwa wao. Kuagana naye kwa sasa ni jambo gumu sana. Na ni jambo linalopaswa kuwa gumu. Uchungu wa kufiwa na mpendwa unaonyesha kwamba kuna upendo wa kweli katika uhusiano huo. Na hilo ni jema. Lakini Mungu anataka pia hisia za kuondokewa na mpendwa zichanganyike na furaha tunapotafakari uhalisi wa mpendwa wetu kuwa pamoja na Baba nyumbani Kwake milele. Furaha yake huko ni kubwa kuliko tunavyoweza kuwazia, nasi siku moja tutaitwa kushiriki furaha hiyo.
Tafakari leo taswira hii ya Mbinguni: nyumba ya Baba yetu. Tulia ukiitafakari taswira hiyo na umruhusu Mungu aseme nawe. Unapofanya hivyo, acha moyo wako uvutwe kuelekea Mbinguni ili hamu hii ikusaidie kuongoza matendo yako hapa na sasa.
Bwana wa Mbingu na Nchi, ninatamani kweli kuwa pamoja Nawe milele Mbinguni. Ninatamani kufarijiwa, kutulizwa na kujazwa furaha nyumbani Kwako. Nisaidie daima kuweka jambo hili kuwa lengo langu maishani na kukua kila siku katika hamu ya kufika mahali hapa pa mapumziko ya mwisho. Yesu, nakutumainia.
Tafakari juu ya Huruma ya Mungu
Mtakatifu wa Siku – Mama Yetu wa Fatima
Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu




