Kiswahili

Kusitasita

28 Septemba 2022
Jumatano ya Wiki ya Ishirini na Sita ya Kipindi cha Mwaka
Masomo ya Leo

Mtakatifu Wenseslao, Shahidi—Kumbukumbu ya Hiari

Watakatifu Lorenzo Ruiz na Wenzake, Mashahidi—Kumbukumbu ya Hiari

Video

Sikiliza kwa Kiingereza

Na mwingine akasema, “Nitakufuata, Bwana, lakini kwanza niruhusu nikawaage watu wa familia yangu nyumbani.” Yesu akamjibu, “Hakuna mtu anayeweka mkono wake kwenye jembe la kukokotwa na kutazama yaliyobaki nyuma anayefaa kwa Ufalme wa Mungu.” Luka 9:61-62

Wito wa Yesu hauna masharti. Anapotuita, tunapaswa kuitikia kwa kuyasalimisha kabisa mapenzi yetu na kwa ukarimu mwingi.

Katika kifungu cha Maandiko hapo juu, Mungu alitaka mtu huyu amfuate Yesu mara moja na kwa moyo wote. Lakini mtu huyo anasitasita, akisema anataka kwenda kwanza kuiaga familia yake. Ombi hilo linaonekana kuwa la kueleweka. Lakini Yesu anaweka wazi kwamba anaitwa kumfuata Yeye mara moja na bila kusitasita.

Hakika, si kwamba kuna ubaya wowote katika kutaka kuiaga familia yake. Yaelekea familia ingetazamia afanye hivyo. Lakini Yesu anatumia nafasi hii kutuonyesha kwamba kipaumbele chetu cha kwanza lazima kiwe kuitikia wito Wake, wakati anapotuita, kwa namna anayotuita, na kwa sababu Yeye anatuita. Katika wito huu wa ajabu, ambao pia una fumbo, wa kumfuata Kristo, lazima tuwe tayari kuitikia bila kusitasita.

Fikiria kama mmoja wa watu katika simulizi hili angekuwa tofauti. Fikiria kama mmoja wao angemjia Yesu na kusema, “Bwana, nitakufuata, nami niko tayari na nina nia ya kukufuata Wewe sasa hivi bila masharti.” Huo ndio utayari kamili unaotarajiwa. Na kweli, wazo hilo ni la kujitoa kabisa.

Katika maisha yetu wenyewe, yaelekea hatutapokea wito wa kujitoa kabisa kwa kuacha kila kitu papo hapo na kwenda kumtumikia Kristo katika namna fulani mpya ya maisha. Lakini jambo la msingi ni utayari wetu! Je, uko tayari?

Ikiwa uko tayari, utaanza kutambua kwamba Yesu anakuita kila siku kutimiza utume Wake. Na ikiwa uko tayari, kila siku utaona kwamba utume Wake ni wa utukufu na unazaa matunda kupita kiasi. Jambo la msingi ni wewe kusema “Ndiyo” bila kusitasita na bila kuchelewa.

Tafakari leo juu ya utayari wako wa kumfuata Yesu. Jiweke katika kifungu hiki cha Maandiko na utafakari jinsi ambavyo ungemwitikia Yesu. Yaelekea utaona hali ya kusitasita. Na ukiona hali hiyo moyoni mwako, jitahidi kuikabidhi kwa Bwana ili uwe tayari kwa yote ambayo Bwana wetu anakukusudia.

Bwana, kwa kweli nakupenda na ninataka kukufuata.  Nisaidie kushinda kila hali ya kusitasita maishani mwangu ninaposema “Ndiyo” kwa mapenzi Yako matakatifu.  Nisaidie kuitambua sauti Yako na kuyapokea yote unayosema kila siku.  Yesu, nakutumainia.

Siku ya Saba: Novena kwa Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu (wa Lisieux) – Ua Dogo

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Watakatifu/Sikukuu Zote

Watakatifu wa Leo –

Mtakatifu Wenseslaus, Shahidi

Watakatifu Laurenti Ruiz na Wenzake, Mashahidi

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu

Picha Iliyoangaziwa: Mtu Anayelima kwa Plau, ya James Tissot, kupitia Wikimedia Commons