Kiswahili

Tamanio la Ndani Kabisa la Moyo Wako

24 Januari 2024

Kumbukumbu ya Mtakatifu Fransisko wa Sales, Askofu na Mwalimu wa Kanisa

Masomo ya Leo

Video

Sikiliza kwa Kiingereza

“Wale waliopandwa kati ya miiba ni wa aina nyingine. Hao ni watu wanaolisikia neno, lakini mahangaiko ya dunia, mvuto wa utajiri na tamaa za mambo mengine huingia na kulisonga neno, nalo halizai matunda.” Marko 4:20

Maelezo haya kutoka katika Mfano wa Mpanzi yanaonekana kuelezea watu wanaozidi kuongezeka katika ulimwengu wetu leo. Watu wa kundi la kwanza wanaotajwa katika mfano huu wana imani haba au hawana imani kabisa, nao wanawakilishwa na mbegu iliyopandwa njiani ambayo huliwa upesi na shetani. Watu wa kundi la pili wana imani kidogo mwanzoni, nao wanawakilishwa na mbegu iliyopandwa kwenye ardhi yenye miamba. Kifungu kilicho hapo juu kinawakilisha kundi la tatu la watu ambao ni kama mbegu zilizopandwa katika udongo mzuri lakini pia ziko katikati ya miiba. Wa kundi la nne ni wale walio kama udongo wenye rutuba, na Neno la Mungu hustawi na kuota mizizi mirefu katika maisha yao. Hebu tulitafakari kwa undani zaidi kundi la tatu la watu.

Kuna maovu matatu yanayolisonga Neno la Mungu katika maisha yetu: “mahangaiko ya dunia, mvuto wa utajiri na tamaa za mambo mengine.” Katika nyakati zetu hizi, kuna wengi wanaokabiliwa na wasiwasi wa aina mbalimbali, wanaotawaliwa na tamaa ya mali na kujikuta wakitamani mambo mengine mengi. Katika hali zote tatu, vishawishi hivi vya ndani huishia kuizidi nguvu Kweli safi ya Neno la Mungu katika maisha yao.

Wasiwasi ni tatizo lililoenea leo. Na ingawa mara nyingi hili ni pambano la kisaikolojia, linaweza pia kuwa na mizizi ya kiroho. Wasiwasi ni hali ya kuhangaika kupita kiasi, kuwa na hofu kuhusu mambo mengi ya maisha na kutokuwa na utulivu kuhusu wakati ujao. Katika hali hii, Yesu mwenyewe na Kweli ya ujumbe wa Injili visipotawala na kuyaongoza maisha yetu, tunabaki peke yetu “kutafuta namna ya kuyamudu.” Na hali hii ya kuwa peke yetu karibu daima itatufikisha katika kupoteza matumaini, hofu na kukosa amani ya ndani.

Watu wengi wanaopambana na wasiwasi hutafuta daima tiba yake. Na mara nyingi mojawapo ya mahali wanapoitafuta ni katika faraja ya udanganyifu ya mali au katika “tamaa za mambo mengine.” Hebu fikiria kama ungeshinda kiasi kikubwa sana cha fedha. Je, hilo lingeondoa mahangaiko yako maishani? Ingawa unaweza kushawishika kufikiri kwamba lingeweza, ndani kabisa sote tunajua kwamba huo ni uongo. Mali kamwe si chanzo cha kutegemewa cha kuridhika maishani. Hali ni hiyo hiyo kwa karibu kila kitu kingine “tunachokitamani” maishani. Kitu kimoja tu ndicho kinachoweza kuturidhisha. Na hicho ni Mungu.

Tafakari leo juu ya mambo katika maisha yako yanayoonekana kuchukua nguvu za akili yako. Unahangaikia nini, unatumainia nini, unatamani nini kwa dhati? Ni nini ambacho unaamini kimakosa kwamba kitakuondolea mapambano yako ya ndani? Unakitamani nini? Tenga muda leo kujikumbusha ukweli usiopingika kwamba Mungu, mapenzi Yake matakatifu na yote aliyoyafunua kuwa ya Kweli ndivyo chanzo pekee cha kuridhika. Jitahidi kuiacha Kweli hiyo izame ndani kabisa ya moyo wako ili Kweli za Mungu zikue na kuzaa matunda mema mengi unayoyatamani kwa dhati.

Bwana wangu mwenye huruma, nisaidie kuwa wazi kikamilifu kwa Neno Lako takatifu ili mbegu ya Neno Lako ipandwe ndani kabisa ya moyo wangu. Daima nikatae uongo na udanganyifu mwingi wa ulimwengu ili niweze kuwekwa huru kutoka katika mahangaiko na anasa za maisha zinazopita. Nitafute tu furaha ya kina na yenye kunitia nguvu inayotokana na maisha yaliyokabidhiwa Kwako kikamilifu, ili niishi katika amani na neema ya mapenzi Yako matakatifu. Yesu, nakutumainia.

Novena ya Siku 9 kwa Ajili ya Uhai
Januari 19–27
Siku ya sita: Januari 24

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Watakatifu/Sikukuu Zote

Mtakatifu wa Siku – Mtakatifu Fransisko wa Sales, Askofu na Mwalimu wa Kanisa

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu

Picha iliyoangaziwa hapo juu: Mfano wa Mpanzi (Septemba), na Marten van Valckenborch