Machi 11, 2024
Jumatatu ya Wiki ya Nne ya Kwaresima
Masomo ya Leo

Sikiliza kwa Kiingereza
Kulikuwa na afisa wa mfalme ambaye mwanawe alikuwa mgonjwa huko Kafarnaumu. Aliposikia kwamba Yesu alikuwa amefika Galilaya kutoka Yudea, alimwendea na kumwomba ashuke akamponye mwanawe, aliyekuwa karibu kufa. Yesu akamwambia, “Msipoona ishara na maajabu, hamtaamini.” Yohane 4:46–48
Hatimaye Yesu alimponya mwana wa yule afisa wa mfalme. Na yule afisa aliporudi na kukuta mwanawe amepona, tunaambiwa kwamba “yeye na watu wote wa nyumbani mwake waliamini.” Baadhi ya watu walimwamini Yesu baada tu ya Yeye kufanya miujiza. Kuna mafundisho mawili tunayopaswa kupata kutokana na hili.
Kwanza kabisa, ukweli kwamba Yesu alitenda miujiza unashuhudia Yeye ni nani. Yeye ni Mungu mwenye huruma tele. Akiwa Mungu, Yesu angeweza kutarajia imani kutoka kwa wale aliowahudumia bila kuwapa “uthibitisho” wa ishara na maajabu. Hii ni kwa sababu imani ya kweli haitegemei ushahidi wa nje, kama vile kuona miujiza; bali, imani halisi hutegemea ufunuo wa ndani kutoka kwa Mungu, ambao kwa njia yake anajifunua kwetu Yeye mwenyewe, nasi tunaamini. Kwa hiyo, ukweli kwamba Yesu alitenda ishara na maajabu unaonyesha jinsi alivyo mwenye huruma nyingi. Aliwajalia miujiza hii, si kwa sababu mtu yeyote aliistahili, bali kwa sababu tu ya ukarimu Wake mkuu, ili kusaidia kuchochea imani katika maisha ya wale walioona vigumu kuamini kwa kutegemea tu kipawa cha ndani cha imani.
Pamoja na hayo, ni muhimu kuelewa kwamba tunapaswa kujitahidi kukuza imani yetu bila kutegemea ishara za nje. Kwa mfano, fikiria kama Yesu asingefanya muujiza wowote kamwe. Ni wangapi wangemwamini? Labda wachache sana. Lakini kungekuwa na baadhi ambao wangeamini, na wale walioamini wangekuwa na imani yenye kina na uhalisi wa pekee. Kwa mfano, fikiria kama huyu afisa wa mfalme asingepata muujiza kwa mwanawe, lakini hata hivyo akachagua kumwamini Yesu kwa njia ya zawadi ya ndani ya imani inayoleta mabadiliko.
Katika maisha ya kila mmoja wetu, ni muhimu tujitahidi kukuza imani yetu, hata kama haionekani kwamba Mungu anatenda kwa njia zenye nguvu na zilizo wazi. Kwa kweli, imani yenye kina zaidi huzaliwa katika maisha yetu tunapochagua kumpenda Mungu na kumtumikia, hata mambo yanapokuwa magumu sana. Kuwa na imani katikati ya magumu ni ishara ya imani halisi kabisa.
Tafakari leo juu ya kina cha imani yako mwenyewe. Maisha yanapokuwa magumu, je, bado unampenda Mungu na kumtumikia? Hata asipokuondolea misalaba unayoibeba? Jitahidi kuwa na imani ya kweli nyakati zote na katika kila hali, nawe utastaajabia jinsi imani yako inavyokuwa halisi na kukutegemeza.
Yesu wangu mwenye huruma, upendo Wako kwetu unapita yote tutakayoweza kufahamu. Ukarimu Wako ni mkuu kweli. Nisaidie nikuamini na kuyakubali mapenzi Yako matakatifu wakati wa heri na wakati wa shida. Nisaidie hasa kuwa tayari kupokea kipawa cha imani, hata wakati ambapo uwepo Wako na utendaji Wako katika maisha yangu vinaonekana kuwa kimya. Nyakati hizo, Bwana mpendwa, ziwe nyakati za mabadiliko ya kweli ya ndani na za neema. Yesu, nakutumainia.
Siku ya Ishirini na Tatu Tafakari:
Siku 40 Jangwani & Siku 40 Msalabani
Novena kwa Mtakatifu Yosefu. Husaliwa kuanzia Machi 10-18.
Novena ya Rozari ya Miezi Tisa pamoja na Kardinali Burke
Tafakari juu ya Huruma ya Mungu
Tafakari za Maandiko Matakatifu kwa Kipindi cha Kwaresima
Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu
Picha zilizoangaziwa hapo juu: Kristo na Akida, iliyochorwa na Paolo Veronese, Wikimedia Commons




