Kiswahili

Umealikwa

Novemba 5, 2024
Jumanne ya Wiki ya Thelathini na Moja ya Kipindi cha Kawaida
Masomo ya Leo

Андрей Николаевич Миронов (A.N. Mironov), CC BY-SA 4.0, kupitia Wikimedia Commons

Video

Sikiliza kwa Kiingereza

“Mtu mmoja aliandaa karamu kubwa, akawaalika watu wengi. Wakati wa karamu ulipofika, alimtuma mtumishi wake awaambie walioalikwa, ‘Njooni, kila kitu sasa kiko tayari.’ Lakini wote, mmoja baada ya mwingine, wakaanza kutoa visingizio.”  Luka 14:16–18

Je, wakati mwingine unatoa visingizio vya kutotimiza mapenzi ya Mungu? Je, unauacha mwaliko Wake wa kushiriki karamu kwenye meza Yake kuu? Zaidi ya yote, mwaliko ambao Mungu ametupa wa kushiriki katika “karamu kubwa” hii ni mwaliko wa kushiriki Misa Takatifu na kusali. Ukweli kwamba baadhi ya watu hutoa visingizio mara kwa mara vya kutokubali mwaliko huo unaonyesha kwamba hawaelewi walichoalikwa kushiriki. Wengine huhudhuria kimwili, lakini ndani ya mioyo yao wako mbali na karamu wanayohudhuria.

Katika mfano huu, walioalikwa hawakufika, mmoja baada ya mwingine. Kwa hiyo mtu aliyeandaa karamu akatuma mwaliko kwa “maskini na wenye ulemavu, vipofu na viwete.” Hapa wanarejelewa wale Wayahudi wa wakati wa Yesu waliotambua kwamba walihitaji zawadi ya wokovu. Ni wale waliotambua udhaifu na dhambi zao na kujua kwamba Yesu ndiye aliyekuwa jibu.

Baada ya maskini, wenye ulemavu, vipofu na viwete kuja karamuni, nafasi bado ilikuwepo. Kwa hiyo mtu huyo akawatuma watumishi wake kuwaalika wale waliokuwa “kwenye barabara kuu na kando ya ua wa vichaka,” jambo linalorejelea Injili kuhubiriwa kwa watu wa mataifa ambao hawakuwa na asili ya Kiyahudi.

Leo, karamu hii inaendelea kutolewa. Hata hivyo, kuna Wakatoliki wengi waliolegea katika imani ambao wanakataa kuja. Wapo wanaoona kwamba wana shughuli nyingi mno maishani kiasi kwamba hawawezi kutenga muda wa sala na wa Misa Takatifu. Hao ni wale waliozama sana katika shughuli za kidunia kiasi kwamba wanaona faida ndogo tu kwao wenyewe katika kujitoa kushiriki adhimisho la Ekaristi Takatifu.

Ikiwa unatamani kuwa miongoni mwa wanaohudhuria karamu ya Bwana wetu, lazima ujitahidi kujiona kuwa mmoja wa maskini, wenye ulemavu, vipofu na viwete. Lazima utambue hali yako ya kuvunjika ndani, udhaifu wako na dhambi zako. Usisite kujiona namna hii, kwa sababu hao ndio ambao Yesu anawapelekea mwaliko wenye shauku kubwa mno. Shauku Yake hiyo ni hamu inayotawala nafsi Yake yote ya kutufanya tushiriki upendo Wake. Anataka kuwapenda na kuwaponya wenye mahitaji. Sisi ndio wenye mahitaji hayo.

Tunapokuja kwenye Karamu ya Bwana wetu kwa njia ya sala, uaminifu kwa Neno Lake, na kwa kushiriki kwetu Sakramenti, tutatambua kwamba anataka wengine wajiunge nasi katika karamu Yake. Kwa hiyo, lazima pia tujione kuwa wale watumishi wanaotumwa kwenye barabara kuu na kando ya ua wa vichaka, ambako tutawakuta wale wasiofuata mapenzi ya Mungu. Lazima waalikwe. Ingawa huenda wasijisikie kuwa wana nafasi humo, Mungu anataka wawe katika karamu Yake. Ni lazima sisi tuwaalike.

Tafakari leo mambo mawili. Kwanza, tafakari kisingizio chochote unachotumia mara kwa mara Mungu anapokualika kusali, kuimarisha imani yako, na kushiriki Ekaristi. Je, unaitikia mara moja na kwa hamu? Au unatoa visingizio mara nyingi zaidi kuliko unavyotaka kukiri? Tafakari pia wajibu uliopewa na Mungu wa kwenda kwa watu waliopotea zaidi ili kuwaalika kwenye karamu ya Mungu. Bwana wetu anataka kila mtu ajue kwamba amealikwa. Mwache akutumie kufikisha mwaliko Wake.

Bwana wangu mkarimu, umenialika kushiriki utukufu wa Karamu Yako kuu. Unanialika kila siku kusali, kuimarika katika imani yangu, na kushiriki Ekaristi Takatifu. Nijalie nikuitikie daima na kamwe nisitoe visingizio vya kukataa mialiko Yako. Tafadhali nitumie pia, Bwana mpendwa, kufikisha mwaliko Wako kwa wale wenye mahitaji makubwa zaidi. Yesu, nakutumainia.

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Watakatifu/Sikukuu za Leo

Tafakari za Maandiko Matakatifu kwa Kipindi cha Mwaka

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu