Julai 13, 2025
Jumapili ya Kumi na Tano ya Kipindi cha Mwaka (Mwaka C)
Masomo ya Leo
Taswira ya Kiafrika ya “Msamaria Mwema” iliyochorwa na Tim Kubacki, leseni CC BY 2.0
Sikiliza kwa Kiingereza
“Mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, kwa nafsi yako yote, kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote, na jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.” Luka 10:27
Mwandishi mmoja alimwuliza Yesu alipaswa kufanya nini ili aurithi uzima wa milele. Yesu alimwuliza mwandishi huyo Sheria ya Musa ilifundisha nini. Maneno yaliyo hapo juu yalikuwa jibu la mwandishi huyo. Kimsingi, alikuwa akinukuu Kumbukumbu la Torati 6:4, sala iliyokuwa ikisaliwa kwa kawaida na Wayahudi na kuonwa kuwa muhtasari wa Sheria yote ya Musa kama inavyopatikana katika Amri Kumi.
Zingatia kwamba muhtasari huu wa Sheria hautoi katazo kama vile “Usi…” Badala yake, unatoa amri ya kutenda, ukisema, “Mpende…” Upendo ni utimilifu wa Sheria ya Agano la Kale, na pia utimilifu wa Sheria Mpya ya Kristo. Tunapompenda Mungu kwa nafsi yetu yote, upendo huo hufurika na kuwafikia viumbe wote wa Mungu, akiwemo jirani yetu.
Katika Injili hii, mwandishi huyo anaendelea kumwuliza Yesu jirani yake ni nani. Yesu anajibu kwa kusimulia Mfano wa Msamaria Mwema. Katika mfano huo, kulikuwa na mtu aliyepigwa na kuachwa kando ya barabara akiwa karibu kufa. Kuhani na Mlawi walipita hapo na kumpuuza mtu huyo. Lakini Msamaria mmoja alipita hapo na kumtunza mtu huyo, akampeleka katika nyumba ya wageni na kuahidi kulipia gharama za kumwuguza hadi apone. Simulizi hilo linahitimishwa kwa kumtambua Msamaria kuwa ndiye aliyemtendea mhanga huyo kama jirani.
Kimapokeo, mhanga wa wanyang’anyi katika simulizi hili ameonekana kuwa Adamu. Adamu anawakilisha wanadamu walioanguka dhambini. Msamaria anamwakilisha Yesu aliyewatunza wanadamu walioanguka dhambini, akatuponya dhambi na kutupatia yote tuliyohitaji. Kwa hiyo, kulingana na mfano huu, Yesu ametutendea kama jirani, nasi tunapaswa kumpenda kama tunavyojipenda wenyewe. Lakini Yesu pia anasema, “Nenda ukafanye vivyo hivyo.” Huu ni utume waliopewa wanadamu walioanguka dhambini, ambao sasa wameponywa dhambi, ili wawaendee wengine, wakitenda kama Yesu mwenyewe, wakiwapelekea neema ya uponyaji waliyopewa na kuwajalia wengine neema hiyo kwa ukarimu.
Wakati mwingine tunaweza kuuona upendo kuwa hisia au msisimko wa moyo. Ingawa mara nyingi upendo huambatana na mihemko na hisia fulani, upendo ni zaidi ya hayo. Ni tendo. Katika mfano huu, kama Msamaria angemtazama tu mhanga huyo na kumsikitikia, akamhurumia lakini kisha akaendelea na safari yake, asingekuwa ameonyesha upendo. Mapendo ni tendo na yanadai mengi kutoka kwetu. Ikiwa tunataka kuitimiza amri hii ya kwanza na kuu zaidi ya kumpenda Mungu na jirani, basi hatuwezi kungoja hadi tujisikie kupenda ndipo tutende. Badala yake, tunapaswa kutenda sasa bila kusita. Huu ndio upendo.
Tafakari leo kuhusu asili ya kweli ya upendo. Upendo, katika namna yake iliyo bora kabisa, ni uamuzi wa kufanya lililo bora zaidi kwa wengine—kuwasaidia kuwa huru kutoka dhambini na kuwa chombo cha maongozi ya Mungu katika maisha yao. Ni kushiriki katika upendo uleule ambao Mungu ametuonyesha katika Kristo Yesu kwa kutoa uhai Wake kwa wokovu wetu. Sote tumeitwa kujitoa kwa upendo huohuo usio na ubinafsi na wenye kujitolea sadaka. Kufanya hivyo ni sharti la kushiriki kwa utukufu katika uzima wa milele.
Bwana wangu mwenye upendo, umewapa wanadamu walioanguka dhambini kila kitu. Umetuweka huru kutoka dhambini na kutupatia yote tunayohitaji. Umetutendea kama jirani wa kweli kwa kila namna. Tafadhali nijalie neema ninayohitaji ili nikuige Wewe na kushiriki katika upendo Wako kwa wengine. Na nitende kwa kweli, wala nisisite kamwe kuwajalia wengine mapendo ambayo nimeitwa kuwa nayo. Yesu, nakutumainia.
Tafakari za Maandiko Matakatifu kwa Kipindi cha Mwaka
Tafakari juu ya Huruma ya Mungu
Mtakatifu wa Siku – Mtakatifu Henriko
Haadhimishwi kama ukumbusho wa kiliturujia mwaka huu kwa kuwa inaangukia Jumapili
Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu




