Kiswahili

Kulitangaza Neno la Mungu kwa Uhuru

Alhamisi, Machi 28, 2019

Alhamisi ya Juma la Tatu la Kwaresima

Masomo ya Leo

Watakatifu Wote wa Leo

Sikiliza kwa Kiingereza

Yesu alikuwa akimfukuza pepo aliyekuwa bubu, na pepo huyo alipotoka, yule mtu aliyekuwa bubu akaanza kusema, na umati wa watu ukashangaa.  Luka 11:14

Ni nini kinachokuzuia kulitangaza Neno la Mungu kwa uwazi, unyofu na ufasaha?  Kuna watu wengi sana wanaoihitaji Injili kwa dharura.  Kuna watu wengi sana ambao wamechanganyikiwa maishani na kujikuta wakifuata njia isiyo sahihi, njia inayoelekea kwenye mkanganyiko mkubwa zaidi na maangamizi.  Nasi tunabaki kimya wanapoifuata njia hii.  Kwa nini?

Injili hapo juu inazungumza kuhusu mtu aliyekuwa bubu kwa sababu ya pepo.  Yesu alipomfukuza pepo huyo, yule mtu aliyekuwa bubu akaanza kusema, na wengi wakashangaa.  Yaelekea sana kwamba mtu huyu alikuwa amepagawa kabisa na pepo huyo, na ukandamizaji alioupata ulimnyima hata uwezo wa kusema.  Alipowekwa huru kutoka katika nguvu hizo za pepo, alianza kusema kwa uhuru.

Ingawa huenda tusipate kuathiriwa na nguvu za pepo kwa kiwango hicho hicho, mara nyingi tunazuiwa na kukandamizwa na roho bubu za namna hiyo.  Mwovu mara nyingi hujaribu kutushawishi kwa namna inayotufanya tuogope kuitangaza Injili kwa uhuru, kwa unyofu na bila kukawia kwa wale wanaouhitaji zaidi ujumbe ambao Mungu anataka wafikishiwe.  “Roho bubu” mara nyingi zinaweza kutuzuia, kutuchanganya au kutujaza hofu fulani nafasi inapojitokeza ya kumshirikisha mwingine imani yetu.  Ingawa huenda isiwe kawaida kuanguka kabisa chini ya nguvu zake, hata hivyo mara nyingi tunaendelea kuathiriwa na kuzuiwa nazo.

Tafakari leo kuhusu uhalisi wa roho hizi ovu na jitihada zake za kutunyamazisha, zikituzuia kutangaza ujumbe wa ukweli ambao watu wengi sana wanahitaji kuusikia.  Hatupaswi kuogopa nguvu zake.  Yesu ana mamlaka kamili juu ya roho zote hizo, na hatasita kukomesha athari zake juu yetu tukimruhusu.  Anataka kutuweka huru ili tutangaze ujumbe Wake wa upendo bila kujizuia, kusudi wengine wapate kumjua Yeye na upendo Wake mkamilifu.  Mruhusu akutumie kama chombo kimojawapo cha ukweli na upendo.

Bwana, nyakati fulani ninatawaliwa na hofu unaponialika kusema maneno Yako ya upendo kwa wenye uhitaji.  Ninahisi kana kwamba nimefungwa ulimi, nisijue la kusema.  Tafadhali uniweke huru, Bwana mpendwa, ili niwe chombo kitakatifu cha Neno Lako na kuitangaza kwa ujasiri kweli Yako kwa wale wenye uhitaji mkubwa.  Yesu, nakutumainia.

Siku 40 Chini ya Msalaba – Tafakari ya Ishirini na Mbili – “Tazameni, Mfalme Wenu!”

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Mengine kwa Ajili ya Kwaresima