Jumapili, 28 Aprili 2019
Jumapili ya Huruma ya Mungu
Siku ya Nane katika Oktava ya Pasaka

Yesu, nakutumainia.
Ni siku iliyojaa neema iliyoje! Hii ni siku ya nane na ya mwisho ya Oktava ya Pasaka. Katika siku hii ya nane ya Pasaka tunaadhimisha Jumapili ya Huruma ya Mungu. Ni siku ambayo malango ya huruma yanafunguliwa wazi kabisa, na Mungu anatukirimia mengi kuliko tunavyoweza hata kutumainia.
Jumapili ya Huruma ya Mungu imeadhimishwa kwa miaka mingi kama ibada binafsi. Lakini katika mwaka 2000, Papa Mtakatifu Yohane Paulo II, ambaye mwenyewe alikuwa chombo cha pekee cha huruma ya Mungu, aliiingiza sikukuu hii katika kalenda rasmi ya Kanisa alipomtangaza Sista Faustina kuwa mtakatifu.
Mtakatifu Faustina alikuwa mwanashirika wa Shirika la Masista wa Mama Yetu wa Huruma huko Krakow, Poland. Alifariki mwaka 1938. Alitoka katika familia ya wakulima maskini walioishi maisha ya kawaida, alipata elimu ya msingi kwa miaka mitatu tu, na alifanya kazi za hali ya chini kabisa katika nyumba yake ya kitawa. Lakini pia alikuwa mtu mwenye maisha ya kifumbo, aliyebahatika kupokea mafunuo mengi binafsi kutoka kwa Bwana wetu, ambayo aliyaandika katika shajara yake ya Huruma ya Mungu.
Anaandika kuhusu tukio alilopitia tarehe 22 Februari 1931:
Jioni, nilipokuwa chumbani mwangu, nilimwona Bwana Yesu akiwa amevaa vazi jeupe. Mkono mmoja ulikuwa umeinuliwa akibariki, na mwingine ulikuwa ukiligusa vazi kifuani. Kutoka kwenye uwazi wa vazi kifuani zilitoka miale miwili mikubwa, mmoja mwekundu na mwingine wenye rangi hafifu. Kwa ukimya nilimkazia Bwana macho; roho yangu ilijawa na hofu, lakini pia na furaha kubwa. Baada ya muda Yesu akaniambia, ‘chora picha kulingana na mfano unaouona, yenye maandishi: Yesu, nakutumainia.’
Baadaye, Yesu alimweleza katika maono mengine:
“Mwale wenye rangi hafifu unawakilisha Maji yanazozifanya roho kuwa zenye haki; mwale mwekundu unawakilisha Damu ambayo ni uhai wa roho. Miale hii miwili ilitoka katika vilindi vya Huruma Yangu yenye upole mkuu wakati ule Moyo Wangu uliokuwa katika uchungu ulipofunguliwa kwa mkuki Msalabani….Heri yule atakayekaa katika hifadhi ya miale hiyo, kwa maana mkono wa haki wa Mungu hautamkamata.”
Yesu alimwambia tena kuhusu hamu Yake ya kwamba Sherehe ya Huruma ya Mungu ianzishwe:
“Siku hiyo (siku ya 8 ya Pasaka kila mwaka) vilindi vyote vya huruma Yangu yenye upole viko wazi. Nazimiminia bahari nzima ya neema roho zile zinazokaribia chemchemi ya huruma Yangu. Roho itakayokwenda kuungama na kupokea Komunyo Takatifu itapata msamaha kamili wa dhambi na kuondolewa kabisa kwa adhabu. Siku hiyo malango yote ya Mungu ambamo neema hutiririka yanafunguliwa. Roho yoyote isiogope kunikaribia, hata kama dhambi zake ni nyekundu kama bendera. Huruma Yangu ni kuu sana kiasi kwamba hakuna akili, iwe ya mwanadamu au ya malaika, itakayoweza kuifahamu kikamilifu kwa umilele wote.”
Tunapoadhimisha Jumapili ya Huruma ya Mungu, tafakari kwa kina wingi wa zawadi hii ambayo Mungu anatamani kutumiminia. Upendo ambao Mungu wetu mwenye huruma kamilifu anatupenda hauna kikomo. Na leo, katika siku hii ya nane ya Pasaka, tunapaswa hasa kutambua kwamba malango ya Mbinguni yamefunguliwa kwetu kwa upana usiowazika. Mgeuzie macho Bwana wetu mwenye huruma na uwe tayari kupokea yote anayotamani kukujalia.
Bwana wa Huruma, nisaidie leo kuanza kuelewa maana halisi ya huruma. Nisaidie kwanza kuifungua roho yangu kwa huruma unayotaka kunijalia. Ninapopokea Huruma Yako ya Kimungu, nisaidie pia kuwa chombo cha huruma hiyo ili wote waione. Yesu, nakutumainia.
Zaidi kuhusu Sikukuu ya Huruma kutoka kwa Yesu kwa Mtakatifu Faustina
Kuhusu Jumapili ya Huruma ya Mungu
Indulgensia ya Jumapili ya Huruma ya Mungu
Litania ya Huruma ya Mungu ya Mtakatifu Faustina
Tafakari za Kila Siku juu ya Huruma ya Mungu
Rozari – Mafumbo ya Utukufu (pamoja na Maandiko Matakatifu)





