Kiswahili

Kusamehe na Kusamehewa

17 Machi 2020
Jumanne ya Juma la Tatu la Kwaresima
Masomo ya Leo

Mtakatifu Patriki, Askofu—Kumbukumbu ya Hiari

Sikiliza kwa Kiingereza

Mtumishi yule akaanguka chini, akamsujudia, akisema, “Univumilie, nami nitakulipa yote.” Bwana wa mtumishi yule akamhurumia, akamwachia na kumsamehe deni.  Mathayo 18:26–27

Hii ni hadithi kuhusu kusamehe na kupokea msamaha.  Jambo la kuvutia ni kwamba mara nyingi ni rahisi zaidi kusamehe kuliko kuomba msamaha.  Kuomba msamaha kwa unyofu kunahitaji kuikiri dhambi yako kwa uaminifu, jambo ambalo ni gumu kufanya.  Ni vigumu kukubali kuwajibika kwa makosa tuliyofanya.

Katika mfano huu, mtu anayeomba avumiliwe kuhusu deni lake anaonekana kuwa mnyofu.  “Alianguka chini” mbele ya bwana wake akiomba huruma na uvumilivu.  Naye bwana wake akamwonea huruma kwa kumsamehe deni lote, jambo lililozidi hata kile ambacho mtumishi alikuwa ameomba.

Lakini je, mtumishi huyo alikuwa mnyofu kweli au alikuwa tu hodari wa kujifanya?  Inaonekana kwamba alikuwa hodari wa kujifanya, kwa sababu mara tu aliposamehewa deni hilo kubwa, alikutana na mtu mwingine ambaye kwa kweli alikuwa akimdai fedha, na badala ya kumsamehe kama yeye alivyosamehewa, “Alimkamata na kuanza kumkaba koo, akidai, ‘Nilipe unachonidai.’”

Msamaha, ikiwa ni wa kweli, lazima uguse kila sehemu ya maisha yetu.  Ni jambo ambalo tunapaswa kuliomba, kulitoa, kulipokea na kulitoa tena.  Hapa kuna mambo machache ya kutafakari:

  • Je, unaweza kuitambua dhambi yako kwa uaminifu, kuisikitikia dhambi hiyo, na kumwambia mwingine, “Ninaomba msamaha”?
  • Unaposamehewa, hilo linakuathirije?  Je, linakufanya uwe na huruma zaidi kwa wengine?
  • Je, nawe unaweza kuwasamehe na kuwahurumia wengine kwa kiwango kilekile unachotarajia kupata kutoka kwa Mungu na kwa wengine?

Ikiwa huwezi kujibu “Ndiyo” kwa maswali haya yote, basi hadithi hii imeandikwa kwa ajili yako.  Imeandikwa kwa ajili yako ili ikusaidie kukua zaidi katika karama za huruma na msamaha.  Haya ni maswali magumu kukabiliana nayo, lakini ni muhimu tukabiliane nayo ikiwa tunataka kuwekwa huru kutoka katika mizigo ya hasira na kinyongo.  Hasira na kinyongo hutulemea sana, na Mungu anataka tuwe huru kutoka katika hayo.

Tafakari leo juu ya maswali haya yaliyo hapo juu na uchunguze matendo yako katika sala.  Ukiona unasita kuyakabili maswali haya, basi zingatia jambo linalokugusa, lipeleke katika sala, na uiruhusu neema ya Mungu iingie ili kuleta wongofu wa kina zaidi katika sehemu hiyo ya maisha yako.

Bwana, ninaikiri kweli dhambi yangu.  Lakini ninaikiri katika mwanga wa neema na huruma Yako iliyo tele.  Ninapopokea huruma hiyo maishani mwangu, tafadhali unifanye nami niwe na huruma kama hiyo kwa wengine.  Nisaidie kusamehe kwa hiari na kikamilifu, bila kubakiza chochote.  Yesu, nakutumainia.

Siku 40 Chini ya Msalaba – Tafakari ya Ishirini – Kutokuwa na Hatia kwa Mwanakondoo wa Mungu

Nyenzo za Kwaresima

Sala ya Kupambana na Janga la Virusi vya Korona

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Watakatifu/Sikukuu za Leo

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu