Kiswahili

Kukabiliana na Kukataliwa

Septemba 23, 2020
Jumatano ya Wiki ya Ishirini na Tano ya Kipindi cha Mwaka
Masomo ya Leo

Mtakatifu Pio wa Pietrelcina (Padre Pio), Padri—Kumbukumbu

Sikiliza kwa Kiingereza

“Na wale wasiowakaribisha, mnapoondoka katika mji huo, kung’uteni mavumbi miguuni mwenu kuwa ushuhuda dhidi yao.”  Luka 9:5

Haya ni maneno ya ujasiri kutoka kwa Yesu.  Pia ni maneno yanayopaswa kututia ujasiri tunapokabiliwa na upinzani.

Yesu alikuwa ametoka kuwaambia wanafunzi Wake waende kutoka mji mmoja hadi mwingine wakihubiri Injili.  Aliwaagiza wasichukue chakula wala mavazi ya ziada safarini, bali wategemee ukarimu wa wale wanaowahubiria.  Naye alitambua kwamba baadhi yao hawatawapokea.  Kwa wale ambao kwa kweli watawakataa wao na ujumbe wao, wanafunzi wanapaswa “kung’uta mavumbi” miguuni mwao wanapoondoka katika mji huo.

Hii ina maana gani?  Inatufundisha hasa mambo mawili.  Kwanza, tunapokataliwa tunaweza kuumia.  Kwa hiyo, ni rahisi kwetu kununa na kuendelea kuwaza kwa uchungu juu ya kukataliwa na kuumizwa huko.  Ni rahisi kukaa tukiwa na hasira na, kwa hiyo, kuruhusu kukataliwa huko kutudhuru hata zaidi.

Kung’uta mavumbi miguuni mwetu ni namna ya kusema kwamba hatupaswi kuruhusu maumivu tuliyopata yatuathiri.  Ni namna ya kutamka wazi kwamba hatutaongozwa na maoni na nia mbaya za wengine.  Huu ni uamuzi muhimu wa kufanya maishani tunapokabiliwa na kukataliwa.

Pili, ni namna ya kusema kwamba lazima tuendelee mbele.  Hatuna budi kushinda maumivu yoyote tuliyo nayo, lakini pia tunahitaji kuendelea mbele na kuwatafuta wale watakaopokea upendo wetu na ujumbe wetu wa Injili.  Kwa hiyo, kwa namna fulani, himizo hili la Yesu halihusu kwanza kukabiliana na kukataliwa na wengine; bali, linahusu hasa kuwatafuta wale watakaotupokea na kuupokea ujumbe wa Injili ambao tumeitwa kuutoa.

Tafakari leo juu ya maumivu yoyote ambayo bado umeyabeba moyoni mwako kwa sababu ya kukataliwa na wengine.  Jitahidi kuyaachilia na ujue kwamba Mungu anakuita uwatafute wengine kwa upendo ili uweze kuwashirikisha upendo wa Kristo.

Bwana, ninapokataliwa na kuumizwa, nisaidie kuachilia hasira yoyote niliyo nayo.  Nisaidie kuendelea na utume wangu wa upendo na kuendelea kuwashirikisha Injili Yako wale watakaoipokea.  Yesu, nakutumainia.

Siku ya Pili: Novena kwa Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu wa Lisieux – Ua Dogo

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Watakatifu/Sikukuu Zote

Mtakatifu wa Siku – Mtakatifu Pio wa Pietrelcina (Padre Pio), Padri

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu

Picha – Kristo mbele ya Herode, iliyochorwa na Duccio di Buoninsegna