Kiswahili

Udongo Wenye Rutuba

20 Julai 2022
Jumatano ya Wiki ya Kumi na Sita ya Kipindi cha Mwaka
Masomo ya Leo

Mtakatifu Apolinari, Askofu na Shahidi—Kumbukumbu ya Hiari

Video

Sikiliza kwa Kiingereza

“Lakini mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo wenye rutuba, zikazaa matunda, mara mia moja au sitini au thelathini. Mwenye masikio na asikie.” Mathayo 13:8-9

“Masikio” anayoyazungumzia Yesu ni zaidi sana ya masikio yetu ya mwili. Anazungumzia maisha yetu ya ndani ambayo kwayo tunaweza kusikia, kuelewa, kukubali na kuchagua mapenzi Yake matakatifu. Anatuambia Neno Lake kwa njia nyingi. Swali la kutafakari ni kama tunasikiliza na tuko tayari kuliruhusu Neno Lake lipenye ndani yetu au la. Ni kwa kulisikiliza Neno Lake kwa makini tu ndipo tunaweza kuyakumbatia mapenzi Yake.

Nafsi zetu lazima ziwe kama udongo wenye rutuba. Hii ni taswira tunayoifahamu kutoka katika Maandiko Matakatifu, lakini ni taswira inayostahili kutengewa muda mwingi wa kuitafakari. Si rahisi kupata udongo wenye rutuba katika nafsi zetu. Ni rahisi zaidi kuwa udongo mkavu, wenye miiba, wenye miamba na usiopokea mbegu. Lakini kukuza ndani yetu rutuba ya kweli na udongo wenye kuzaa kunahitaji utunzaji na uangalifu mkubwa. Hili linafanyikaje?

Mojawapo ya hatua muhimu zaidi za kuanzia, ili kuandaa udongo wenye rutuba ndani ya nafsi zetu, ni kujitahidi kuwa na unyenyekevu wa kweli. Kiini cha unyenyekevu ni kuona ukweli kuhusu sisi ni nani na, hasa, kutambua uhitaji wetu wa neema ya Mungu katika maisha yetu. Kukiri kwa unyenyekevu kwamba hatuna nguvu bila neema ya Mungu ni jambo la lazima ili kuandaa udongo wenye rutuba ndani yetu.

Kutoka hapo, lazima tufikie hatua ya kumtumainia Mungu kabisa. Tukianza kwa kujinyenyekeza na kutambua kwamba tunamhitaji Mungu kabisa, tutakuwa tayari kumtumainia anaposema. Na atakaposema, tutasikiliza na kutii kwa furaha. Ni hapo tu ndipo matunda mema ya huruma Yake yanaweza kumiminwa katika maisha yetu na, kupitia sisi, katika maisha ya wengine.

Tafakari leo kuhusu maisha yako ya ndani. Kuna nini humo? Je, yanafanana zaidi na ardhi kavu yenye miamba? Au unajitahidi mara kwa mara kuilisha nafsi yako na kuiandaa kupokea Neno takatifu la Mungu? Jitahidi kuwa na utayari wa ndani ulio kama udongo wenye rutuba, naye Bwana atahakikisha kwamba maisha yako yanazaa matunda mema.

Bwana wa utajiri wa kweli, unisaidie kuwa udongo wenye rutuba kweli kwa ajili ya Neno Lako takatifu kabisa. Nipokee yote unayosema, nayo mbegu ya imani ipandwe ndani kabisa ya nafsi yangu. Isaidie imani hii ikue na kuzaa baraka unazotaka kunijalia. Yesu, nakutumainia.

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Watakatifu/Sikukuu Zote

Mtakatifu wa Siku: Mtakatifu Apolinari

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu

Picha Iliyoangaziwa: Kristo Mpandaji wa Mbegu Njema, Flikr