26 Oktoba 2022
Jumatano ya Juma la Thelathini la Kipindi cha Mwaka
Masomo ya Leo

Sikiliza kwa Kiingereza
“Ndipo atawaambia, ‘Sijui mnakotoka. Ondokeni Kwangu, ninyi nyote mtendao maovu!’” Luka 13:27
Yesu anaweka wazi kwamba kuna watu watakaomjia wakijihakikishia kwamba wataingia Mbinguni, lakini kujiamini kwao huko kutakabiliwa na maneno haya ya kutisha: “Sijui mnakotoka. Ondokeni kwangu.”
Kujitumainia kupita kiasi ni dhambi hatari. Ni hatari kwa sababu mbili. Kwanza, watu wanapojitumainia kupita kiasi, wanaishi huku wakikataa kuutambua ukweli. Kuhusiana na Mungu, kujitumainia kupita kiasi kunamaanisha kwamba watu wanatenda kana kwamba wana uhusiano na Mungu ilhali hawana. Wanaweza kusema mambo matakatifu, kutenda kana kwamba ni watakatifu na hata kuamini kwamba ni watakatifu, ilhali kwa kweli hawamjui Bwana wetu hata kidogo. Hivyo, kujitumainia kupita kiasi ni kuishi huku mtu akikataa kuutambua ukweli.
Pili, kujitumainia kupita kiasi ni hatari kwa sababu mtu anayejitumainia hivyo hatatubu dhambi yake mwenyewe. Hii ni kwa sababu kukataa kwake kuutambua ukweli kunamfanya asiweze kukiri dhambi yake. Bila kukiri dhambi yake, hawezi kisha kukiri kwamba anahitaji kubadilika. Anaendelea kuzama katika mawazo yake potovu na dhambi yake.
Yesu anatoa fundisho hili si ili kuonyesha kwamba Yeye ni mkali kwa wale wanaojiamini kupita kiasi; bali analitoa kama tendo la huruma kuu kwa wale walionaswa katika dhambi hii. Ufunuo huu wenye kushtua unahitajika ili kumzindua mtu na kumweka huru kutoka katika dhambi hii. Katika hali hii, hofu ya kusikia maneno haya kutoka kwa Yesu siku moja ndiyo itakayowasaidia wale walionaswa katika kujiamini kupita kiasi wajinasue na kuukabili ukweli.
Tafakari leo kuhusu namna yoyote ambayo husemi au kuukubali ukweli kuhusu wewe mwenyewe, iwe kwako mwenyewe au kwa wengine. Acha mshtuko wa matokeo ya mwisho ya kujitumainia kokote kupita kiasi maishani mwako ukuzindue ujinasue katika dhambi hii, ili uweze kujinyenyekeza mbele za Mungu sasa, kabla hujachelewa mno. Kumbuka jinsi Bwana wetu anavyokupenda kwa dhati, na uruhusu upendo huo ukusaidie kuyakabili maisha yako kwa unyofu na uadilifu.
Bwana wangu mwenye upendo, nakupenda sana na ninaomba upendo wangu uwe daima wa kweli, wa dhati na kamili. Nisaidie kuona katika maisha yangu njia zozote ambazo nashindwa kukupenda kwa moyo wangu wote. Nakukabidhi maisha yangu bila kujibakizia chochote, Bwana mpendwa. Yesu, nakutumainia.
Novena kwa Mtakatifu Yuda
Kwa Hali na Matatizo ya Kukatisha Tamaa
Husaliwa wakati wowote wa mwaka, hasa Oktoba 19–27
Filamu ya Makala kuhusu Mtakatifu Mama Teresa—2&3 Novemba!
Tafakari juu ya Huruma ya Mungu
Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu
Picha Iliyoangaziwa: Hukumu ya Kristo na Antoine Wiertz, kupitia Wikimedia Commons




