Kiswahili

Kuifurahia Zawadi ya Imani

Julai 19, 2023
Jumatano ya Wiki ya Kumi na Tano ya Kipindi cha Mwaka
Masomo ya Leo

Video

Sikiliza kwa Kiingereza

Wakati huo Yesu akasema kwa sauti: “Ninakusifu Wewe, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa ingawa umewaficha wenye hekima na wasomi mambo haya, umewafunulia wale wenye moyo kama wa watoto.”  Mathayo 11:25

Kifungu hiki kinatofautiana kabisa na kile kinachokitangulia, ambamo Yesu aliikemea miji ya Korazini, Bethsaida na Kafarnaumu kwa kutotubu na kutomwamini. Mara tu baada ya kutoa makemeo hayo, Yesu aliinua macho Yake mbinguni na kumsifu Baba kwa kuwafunulia mafumbo yaliyofichika ya Ufalme wa Mbinguni wale waliokuwa na “moyo kama wa mtoto.”

Mojawapo ya mambo yanayoihatarisha zaidi imani safi yenye moyo kama wa mtoto ni majivuno ya kiakili. Wale wanaojiona kuwa “wenye hekima na wasomi” mara nyingi hushawishika kutegemea uwezo wao wenyewe wa kufikiri ili kufikia hitimisho na kuamua wanachoamini maishani. Tatizo ni kwamba, ingawa mambo ya imani yetu yanapatana kikamilifu na akili, yanazidi yale ambayo akili ya binadamu pekee inaweza kuhitimisha. Hatuwezi kumfahamu Mungu kwa uwezo wetu wenyewe. Kwa hilo tunahitaji zawadi ya imani, nayo zawadi ya imani huanza kwa Mungu kuwasiliana nasi kiroho, akitufunulia Yeye ni nani na kilicho cha kweli. Ni wale tu wenye moyo kama wa mtoto, yaani, wale walio wanyenyekevu, wanaoweza kusikia Mungu akiwasiliana nao kwa namna hii na kumwitikia.

Kifungu hiki pia kinatufunulia kwamba Yesu huifurahia sana imani hii yenye unyenyekevu. Anampa Baba wa Mbinguni “sifa” anapoiona imani kama hii, kwa sababu Yesu anajua kwamba imani hii inatoka kwa Baba.

Katika maisha yako, ni muhimu kutafakari mara kwa mara kama unafanana zaidi na wenye hekima na wasomi au na wale wenye moyo kama wa mtoto. Ingawa Mungu ni fumbo lisilo na kikomo na lisiloweza kufahamika kikamilifu, ni lazima tumjue. Nayo njia pekee ya sisi kumjua Mungu ni Yeye kujifunua kwetu. Na Mungu atajifunua kwetu tu ikiwa tutadumu katika unyenyekevu na kuwa na moyo kama wa mtoto.

Tunapofikia imani yenye moyo kama wa mtoto, ni lazima pia tumwige Yesu katika sifa alizompa Baba kwa ajili ya imani aliyoiona katika maisha ya wafuasi Wake. Sisi pia tunapaswa kuwaangalia wale wanaodhihirisha wazi kumjua Mungu kwa namna hii safi kwa zawadi ya imani. Tunapoiona imani hii ikiwekwa katika matendo, tunapaswa kufurahi na kumsifu Baba. Na hatupaswi kumsifu tu tunapoiona imani hai ndani ya wengine, bali pia tunapoiona zawadi ya imani ikikua ndani ya nafsi zetu wenyewe. Tunapaswa kukuza ndani yetu mshangao mtakatifu kwa yale ambayo Mungu anafanya ndani yetu, na kuyafurahia yale tunayoyaonja.

Tafakari leo jinsi Yesu anavyomsifu Baba anapoiona imani ikizaliwa mioyoni mwa wafuasi Wake. Yesu anapokutazama, anafanya nini? Je, anakukemea? Au Moyo Wake Mtakatifu unafurahi na kutoa sifa kwa yale anayoyaona. Ufurahishe Moyo wa Kristo kwa kujinyenyekeza kiasi kwamba nawe uhesabiwe miongoni mwa wale wenye moyo kama wa mtoto, wanaomjua na kumpenda Mungu kweli.

Bwana wangu mwenye furaha, Wewe unaangalia kwa makini utendaji wa neema katika kila moyo wa mwanadamu. Unaposhuhudia Sauti ya Baba ikisema na watoto Wako, unafurahi kwa hayo unayoyaona. Bwana mpendwa, ninaomba moyo wangu mwenyewe uwe sababu ya furaha Yako na ya Wewe kumsifu Baba wa Mbinguni. Tafadhali sema nami na unisaidie kuamini kwa moyo wangu wote. Yesu, nakutumainia.

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Tafakari za Maandiko Matakatifu kwa Kipindi cha Mwaka

Watakatifu/Sikukuu za Leo

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu

Picha iliyoangaziwa hapo juu: Yesu Anapanda Mlimani Peke Yake Kusali, iliyochorwa na James Tissot, kupitia Wikimedia Commons