Kiswahili

Fanya Uamuzi wa Kujitoa Kabisa, Leo

17 Februari 2024
Jumamosi baada ya Jumatano ya Majivu
Masomo ya Leo

Watakatifu Saba Waanzilishi wa Shirika la Watumishi wa Maria—Kumbukumbu Isiyo ya Lazima

Video

Sikiliza kwa Kiingereza

Yesu alimwona mtoza ushuru aitwaye Lawi ameketi kwenye kituo cha ushuru. Akamwambia, “Nifuate.” Naye akaacha kila kitu, akainuka na kumfuata. Luka 5:27–28

Lawi alikuwa na maisha mazuri. Alipata kipato kizuri na alikuwa na kazi ya kudumu ya kutoza ushuru. Lakini kwa mara moja, aliacha hayo yote ili amfuate Yesu, na maisha yake yakabadilika mara moja na kuwa bora.

Simulizi hili fupi la wito wa Lawi ni la kulitilia maanani. Ingawa yaelekea tayari umeamua kumfuata Kristo, uamuzi huo unahitaji kuimarishwa kila siku. Na ushuhuda wa Lawi unapaswa kukuhamasisha kufanya hivyo.

Mara nyingi, tunapohisi Mungu anatuita tuzidishe uhusiano wetu Naye na kumkaribia zaidi, tunapohisi kwamba anataka tumfuate kwa ukamilifu zaidi, huenda tukasita na kusitasita. Ni kawaida kwa watu kutaka kuutafakari kwa kina uamuzi kama huo na kupima “faida na hasara” kabla ya kupiga hatua kwa imani. Lakini usifanye hivyo. Ushuhuda wa uamuzi wa Lawi wa kuacha mara moja kila kitu kingine na kumfuata Kristo umetolewa kwetu ili kutualika tufanye vivyo hivyo.

Yesu anakualikaje leo kuiga jinsi Lawi alivyojitoa kabisa? Anakuita uache nini ili umtumikie kwa ukamilifu zaidi, kwa upendo na kwa moyo wote? Ikiwa hujui jibu la swali hilo, hata hivyo mwambie Bwana wetu “Ndiyo.” Mwambie kwamba unataka kumwiga Lawi na kwamba unataka kujitoa kwa moyo wote kuyafuata mapenzi Yake matakatifu kikamilifu na bila kusita.

Pia ni jambo la kuvutia kuona kwamba mara tu Lawi alipoamua kumfuata Yesu, aliandaa karamu nyumbani kwake kwa ajili ya Yesu na watoza ushuru wengine. Lawi hakuogopa kuwajulisha wengine kuhusu uamuzi wake, naye alitaka kuwapa rafiki zake nafasi ya kufanya vivyo hivyo.

Tafakari leo kuhusu Lawi na wito wake. Na unapoanza kipindi hiki cha Kwaresima, tumia wito wa Lawi na jinsi alivyouitikia kama fursa ya kumsikia Yesu akikuita. Huenda huitwi “kuacha kila kitu” kwa maana halisi, lakini hata hivyo onyesha utayari wako wa kufanya hivyo. Usiweke masharti yoyote katika uamuzi wako wa kumfuata Bwana wetu, nawe utashukuru milele kwa kuwa ulifanya hivyo.

Bwana wangu mpendwa sana, unawaita watoto Wako wote wakufuate bila kujibakiza. Unatuita tuwe tayari na wenye nia ya kuacha yote ambayo maisha haya yanaweza kutupatia ili tupate mengi zaidi. Nipe neema ninayohitaji ya kukutumainia kiasi cha kukuambia “Ndiyo” leo, kesho na siku zote. Maisha yangu ni Yako, Bwana mpendwa. Unitendee utakavyo. Yesu, nakutumainia.

Tafakari za Siku ya Nne:
Siku 40 Jangwani & Siku 40 Msalabani

Nyenzo za Kwaresima

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Tafakari za Maandiko Matakatifu kwa Kipindi cha Kwaresima

Watakatifu/Sikukuu Zote

Mtakatifu wa Siku – Waanzilishi Saba Watakatifu wa Shirika la Waserviti

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu

Picha iliyoangaziwa hapo juu: Kuitwa kwa Mtakatifu Mathayo, iliyochorwa na Giovanni Paolo Panini, kupitia Wikimedia Commons