Kiswahili

“Nina Kiu!”

Machi 29, 2024

Ijumaa Kuu ya Mateso ya Bwana Mwaka B

Masomo ya Leo

Zaidi kwa Juma Takatifu

Video

Sikiliza kwa Kiingereza

Baada ya hayo, Yesu, akijua kwamba sasa kila kitu kilikuwa kimemalizika, alisema ili Maandiko yatimizwe, “Nina kiu.” Palikuwa na chombo kilichojaa divai ya kawaida. Basi wakaweka sifongo iliyolowekwa katika divai kwenye kitawi cha hisopo, wakaipeleka mdomoni Mwake. Yesu alipokwisha kuipokea ile divai, alisema, “Imekwisha.” Akainamisha kichwa, akaikabidhi roho Yake. Yohane 19:28–30

Tafakari juu ya kiu ya Yesu. Ingawa kiu Yake ya kimwili bila shaka ilikuwa yenye maumivu makali sana aliponing’inia Msalabani, akiimwaga damu Yake ya thamani juu ya ulimwengu, kiu ya kiroho ambayo Bwana wetu aliihisi ilikuwa kubwa zaidi sana kuliko kiu Yake ya kimwili. Kiu Yake ya kiroho ni kiu kwa ajili yako, kwa ajili ya roho yako, kwa ajili ya wokovu wako. Aliponing’inia Msalabani, Yesu hakujifikiria Mwenyewe, mateso Yake wala hali Yake ya kimwili iliyokuwa ya kusikitisha sana. Badala yake, alikufikiria wewe na wote ambao alikuwa akitoa uhai Wake kwa ajili yao.

Zaburi 69:22 inasema, “Badala yake walinipa sumu iwe chakula changu; na kwa kiu yangu wakanipa siki.” Yesu alitimiza kifungu hiki cha Maandiko alipokuwa na kiu Msalabani. Siki inamwakilisha kila mmoja wetu kwa namna ya ishara. Siki aliyopewa Bwana wetu Msalabani ilikuwa divai iliyoharibika. Kwa lugha ya ishara, kila mmoja wetu ni divai hii iliyoharibika. Usafi wa ubinadamu wetu umeharibiwa na dhambi ya asili. Kwa hiyo, sisi si watu ambao Mungu alikusudia tuwe kwa asili. Lakini katika hali yetu ya kuanguka dhambini, tuna uwezo wa kuikata kiu ya kiroho ya Yesu.

Unapofikiria maisha yako mwenyewe, unaona nini? Je, unaweza kujiona kama divai iliyoharibika? Huenda kujifikiria hivyo kunakufanya ujihisi umedhalilika kidogo. Lakini unyenyekevu ni mzuri, hasa tunapoelewa kwamba Bwana wetu anatamani tuwe karibu Naye katika hali yetu ya kuvunjika. Msalabani, Yesu hakulilia divai bora kuliko zote, iliyo safi na yenye ladha nzuri zaidi. Alipokuwa na kiu Msalabani, alitamani kiu Yake ikatwe na wewe, katika hali yako ya udhaifu na kuvunjika, jinsi ulivyo, ili aweze kukumiminia huruma Yake inayotakasa.

Mara tu Yesu alipoionja divai chachu, alipaza sauti, “Imekwisha.” Kwa namna ya ishara, hili linaonyesha jinsi kiu ya nafsi Yake inavyokatwa nawe kila unapomgeukia katika uhitaji wako. Inastaajabisha kutafakari ukweli kwamba una uwezo wa kuufariji Moyo wa Yesu na kuikata kiu Yake kwa namna hii. Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu wa Lisieux alipenda sana ibada iliyolenga kuufariji Moyo wa Yesu. Alipokuwa mtoto, alipewa kadi ya sala iliyokuwa na picha ya Yesu gerezani, akilitazama ua moja dogo lililokuwa nje. Teresia alijiona kuwa lile ua moja dogo lililopewa utume wa kuufariji Moyo wa Yesu kwa kumtembelea mara kwa mara katika gereza la tabernakulo.

Kwa mtazamo wa kiroho, ule wakati wa kiu ya Yesu Msalabani unapenya nyakati zote na unaendelea leo. Kila unapomjia katika uhitaji wako, hasa unapokuja mbele Yake katika Ekaristi, anakutazama na kukuita, akikualika umfariji kwa kumtolea unyenyekevu na hali ya kuvunjika ya maisha yako.

Leo makanisa yetu yako matupu. Sakramenti Takatifu imeondolewa. Kwa hiyo, tunapaswa kujitahidi kuikata kiu ya Bwana wetu kwa kuwa na kiu ya uwepo Wake wa kimungu utakaorejea siku ya Pasaka, Misa Takatifu itakapoadhimishwa tena. Leo ni siku ya kukua katika hamu yetu ya uwepo wa Bwana wetu maishani mwetu. Tunapaswa kujiruhusu tuhisi uchungu wa kutokuwepo Kwake, tupitie kifo Chake, na tuomboleze mateso Yake. Tunapofanya hivyo, tunapaswa kufungua mioyo yetu kwa shauku kubwa ya kiroho ya kuupokea tena Mwili Wake uliovunjwa na Damu Yake ya thamani. Kufanya hivyo hakutatuandaa tu ili kiu yetu wenyewe ikatwe, bali pia kutatuwezesha kuikata kiu ya Moyo wa Bwana wetu.

Tafakari leo juu ya Yesu Msalabani. Mtazame Yeye anapokutazama wewe. Ona jinsi Moyo Wake unavyokutamani. Jua kwamba alitoa uhai Wake kwa ajili yako, ili uweze kupokea zawadi ya maisha mapya. Jua pia kwamba kuifungua kwako nafsi yako kwa zawadi hii ya uhai Wake uliotolewa kwa ajili yako kutaufariji Moyo wa Bwana wetu na kuufikisha utume Wake wa kimungu wa wokovu kwenye utimilifu. Ikate kiu ya Bwana wetu leo ili aweze kusema tena, “Imekwisha.”

Bwana wangu mwenye kiu, Moyo Wako Mtakatifu unanitamani kwa upendo usio na mwisho wala usioweza kufahamika kikamilifu. Unatamani nije Kwako, nipokee upendo Wako na kuikata kiu Yako. Ninapokutazama katika hali Yako ya mateso, ninaifungua nafsi yangu Kwako na kwa zawadi ya Damu Yako ya Thamani iliyomwagika kwa ajili yangu. Kufunguka kwangu Kwako kukufariji ninapopokea upendo Wako wa kimungu. Yesu, nakutumainia.

Siku ya Thelathini na Tisa Tafakari:
Siku 40 Jangwani & Siku 40 Msalabani

Siku ya Kwanza: Novena ya kujiandaa kwa Jumapili ya Huruma ya Mungu
Ijumaa Kuu ndiyo siku ya kwanza ya Novena ya Huruma ya Mungu

Zaidi kwa Juma Takatifu

Tafakari ya sala kwa Ijumaa Kuu

Njia ya Msalaba

Rozari – Mafumbo ya Uchungu (pamoja na Maandiko Matakatifu)

Somo la Ijumaa Kuu

Leo Hii Utakuwa Pamoja Nami
Shairi la Wiki Takatifu

Sala ya Mkulima wa Efeso
Shairi la Wiki Takatifu

Siku 40 Chini ya Msalaba

Sala Mbele ya Msalaba Wenye Sanamu ya Yesu

Sala ya Kujisalimisha

Sala ya Kujiachilia

Sala kwa Ajili ya Walio Toharani

Upendo Mkubwa Zaidi kwa Mungu

Uchunguzi wa Dhamiri

Rozari ya Kuomba Huruma ya Kumsamehe Mwingine

Litania ya Unyenyekevu

Tafakari za Kila Siku juu ya Huruma ya Mungu

Litania ya Huruma ya Mungu ya Mtakatifu Faustina

Kuitumainia Huruma ya Mungu

Sala kwa Mwaka wa Huruma

Rozari ya Huruma ya Mungu

Watakatifu/Sikukuu za Leo

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu

Picha zilizoangaziwa hapo juu: Mchoro wa kusulubiwa kwa Yesu Kristo, kupitia Adobe


  Subscribe to our YouTube channel  
  to be notified about new content.