Kiswahili

Kung’aa kwa Nuru Angavu

Jumatatu, Septemba 23, 2019

Jumatatu ya Juma la Ishirini na Tano la Kipindi cha Kawaida

Masomo ya Leo

Mtakatifu Pio wa Pietrelcina (Padre Pio), Padri – Kumbukumbu

Sikiliza kwa Kiingereza

“Hakuna mtu anayewasha taa na kuifunika kwa chombo au kuiweka chini ya kitanda; bali huiweka juu ya kinara ili wanaoingia waone nuru.”  Luka 8:16

Sote tunahitaji “kuiona nuru.”  Njia moja ya jambo hilo kutokea ni pale wengine wanapokuwa kwetu nuru angavu za Kristo.  Na njia moja ambayo wale wanaotuzunguka “wanaiona nuru” ni pale tunapokuwa kwao mifano angavu ya nuru ya Kristo.

Kifungu hiki kinaonyesha wajibu wetu wa kuwa nuru ya Kristo kwa ulimwengu wenye uhitaji.  Kifungu hiki kinaweka wazi kwamba tunapowasha mwali wa Kristo mioyoni mwetu, Kristo huangaza kupitia kwetu ili wengine wamwone.  Yesu anasema kwamba “Hakuna mtu anayewasha taa na kuificha…”  Kwa maneno mengine, ikiwa huangazi kwa nuru ya Kristo, si kwa sababu unamficha, bali ni kwa sababu Yeye hawaki ndani ya roho yako.  Anapowaka ndani ya roho yako, nuru hiyo haiwezi kuzuiliwa.

Ukweli huu wa msingi ni msaada mkubwa kwetu katika kutambua hali ya uhusiano wetu na Kristo.  Kimsingi, ikiwa Yesu anaishi ndani yetu, ikiwa tunaishi katika uhusiano wa kweli wa upendo Naye, basi tutaweza kuona matokeo yake katika maisha ya wale wanaotuzunguka.  Tutaweza kuona nuru hiyo ikiwaangazia wengine. Matokeo ya Kristo kuangaza kupitia sisi yatakuwa kama kioo cha nafsi zetu wenyewe.

Tafakari leo kuhusu wale wanaokuzunguka, ukijiuliza upendo wako kwa Kristo una matokeo gani katika maisha yao.  Je, unawaona wengine wakivutwa kumpenda Kristo kwa njia yako?  Ikiwa sivyo, tazama ndani ya moyo wako mwenyewe na ujitahidi kuuwasha upya moto wa upendo wa Mungu.

Bwana, njoo uwake ndani yangu, ukiwasha moyo wangu kwa moto wa upendo Wako.  Natamani moyo wangu uwe moto uwakao kwa nguvu, ambao kupitia huo wengi watavutwa Kwako.  Unitumie, Bwana mpendwa, kama upendavyo.  Yesu, nakutumainia.

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Mtakatifu wa Siku – Mtakatifu Pio wa Pietrelcina (Padre Pio)